Na Salma Lusangi
NAIBU waziri Wizara Maji, Nishati na Madini
(WMNM) Zanzibar Shabaani Ali Othman ameagiza uongozi wa wizara hiyo kufikisha huduma
ya maji safi na salama haraka katika Shehia ya Kizimbani Jimbo la Bububu,
Wilaya Maghari ‘B’ ili kuwaondolea tatizo liliyopo.
Akizungumza na wakaazi wa eneo hilo,
alisema haiwezekani wananchi wakose maji kwa muda wa miezi minne hivyo aliitaka
Uongozi wa Wizara yake kuhakikisha wakaazi wa shehia hiyo wanafungiwa mashine
ya kusukumia maji katika kisima cha rasilihema ili wapate huduma hiyo.
Alisema ikiwa changamoto kubwa ya maji
katika eneo hilo inatokana na mashine ya kusukumia maji kuungua hivyo Wizara
yake inajukumu la kufunga mashine nyengine ili wananchi wapate huduma hiyo.
Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ) kupitia wizara hiyo inatekeleza miradi mikubwa ya maji ili
kuowandolea wananchi tatizo la maji safi na salama ikiwa ni ahadi ya Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi
hivyo sio muda mrefu miradi hiyo itakamilika.
“Haiwezikani miundombinu ya maji ipite eneo
hili wananchi wa Kizimbani wasipate maji, nimekuja na Katibu Mkuu na watendaji
wa ZAWA ili wasikie malalamiko yenu na kuyafanyia kazi, hivyo mashine za maji
zikifika tu Katibu Mkuu nakuagiza kisima cha rasilihema kifungwe mashine ya
maji.” Alisema Othman.
Aidha alisema Maji Zanzibar (ZAWA) inajukumu la kurudisha miundombinu ya maji kwa wananchi ambayo imekatwa wakati wa ulazaji wa mabomba ya maji ikiwa ni utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji Zanzibar.
Pia Naibu waziri huyo aliwataka wakaazi wa
eneo hilo kutunza miundombini ya maji ambayo imepita katika eneo hilo kwasababu
miradi ya maji itakapo kamilika mwezi wa Disemba Mwaka huu, kusiwe na
changamoto ya ukosefu wa miundombinu ya maji hali ambayo itapelekea usumbufu
katika kukamilika kwa miradi hiyo.
Comments
Post a Comment