NA HAJI NASSOR, PEMBA:
WANAWAKE wenye ulemavu wa shehia za
Michungwani na Wesha wilaya ya Chake Chake Pemba, wamelezea kuchoshwa na vifo
vya watoto wao wachanga na sulubu ya kujifungua njiani, wakati wanapopelekwa
hospitali, kutokana na uchakavu wa muda mrefu wa barabara yao.
Walisema,
imekuwa ni kawaida kwa mwaka kupata vifo vya watoto wachanga kati ya viwili
hadi vitatu, au akinamama wajawazito kupata matatizo wakati wanapojifungua
kutokana kuchelewa kufika hospitali za Wesha na ya Chake Chake.
Wakizungumza
na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali, walisema barabara yao imekua
ikichangia kwa asilimia 100 vifo vvya watoto wachanga na wazazi, kutokana na
uchakavu wake unaokwamisha gari kupita kwa kasi.
Walisema,
matatizo zaidi huwakumba katika kipindi cha mvua, kwa vile barabara hiyo, hujaa
mashimo yenye kina kirefu ambayo hairuhusu hata gari ya Ng’ombe kupita kwa
utulivu.
Mmoja kati
ya wanawake hao mwenye ulemavu wa viungo Raya Salim Khamis, alisema suala la wao
na wagonjwa wengine kwenye kijiji chao kupata misuko suko inayotokana na
barabara yao, ni jambo la kawaida hasa
kila inapofika kipindi cha mvua.
Alisema yeye
mwaka 1990, aliwahi kubebwa kwa gunia kutokana Birikau hadi barabara kuu, na alipofika
katikati ya safari, alijifungua.
“Kwa
uchakavu wa barabara yetu kwa mwaka huo, nilimpoteza mtoto wangu na mimi mwenye
nilipata ulemavu wa mguu uliosababishwa na uchungu mzito, kwa kule kuchelewa
kufika hospitali,’’alisema.
Nae Halima
Kassim Juma mwenye ulemvu wa uziwi, alisema sasa zaidi ya miaka 40 amekuwa
akishuhudia dhiki ya barabara yao, jambo ambalo hata yeye ameshawahi kupoteza
mtoto, baada ya kujifungua kwake nyakati za usiku.
“Niliumwa na
uchungu wa kujifungua nyakati za usiku mkubwa, na nikajifungua nyumbani na
asubuhi nilipelekwa hospiatali na mwangu alifariki, baada ya kupoteza damu
nyingi,’’alieleza.
Aidha mama
huyo alisema, alianza yeye kubebwa kwa magunia na vitanda kupelekwa hospitali
kwa kifungua, na sasa zamu imekuwa ya watoto wake wanapokuwa wajawazito.
Hata hivyo
Hussan Yussuf Hamad (39) wa Tondooni shehia ya Wesha, alisema tokea afahamu
yeye barabara yao imekuwa na usumbufu, jambo linalowapa dhiki hasa wajawazito
na wa wagonjwa.
“Baba yangu
alikuwa ni mgonjwa wa pumu na alikuwa akibebwa kwa kitanda kutoka hapa kijijini
hadi barabara kuu, na sasa ni muda mrefu hadi leo, kadhia
ikiendelea,’’alieleza.
Massoud Seif
Massoud na Khamis Ali Said walisema dhiki ya barabara hiyo, imekuwa ni jambo la
kawaida kwao, na waathirika ni wanawake hasa wenye ulemavu.
Walisema,
kila Mbunge na Mwakilishi anayefika kijijini kwao, huwaahidi kuwatengenezea
barabara hiyo kwa kiwango cha kifusi, ingawa baada ya kupata nafasi hizo
hushindwa kutekeleza.
Naibu sheha
wa shehia ya Michungwani wilaya ya Chake Chake Amina Hamad Fakih, alisema
hawajakata tamaa, lakini wameanza kupata wasi wasi na utekelezaji wa ahadi za
viongozi juu ya ujenzi wa barabara yao.
Alisema,
amekuwa akishirikiana na sheha mwenzake wa shehia ya Wesha kupeleka taarifa
kila wakati ofisi ya wilaya na baraza na mji wa Chake Chake juu ya ubovu wa
barabara hiyo, ingawa bado wanaendelea kuteseka.
Mkuu wa
wilaya ya Chake Chake Rashid Hadid Ali, alisema kwa sasa barabara hiyo pamoja
na nyingine zilizomo wilayani humo, zimeshaingizwa kwenye mpango wa kujengwa
kwa kiwango cha lami.
Alisema
barabara za Birikau- Kijangwani, Wesha Ndagoni na ile ya Gombani- Michungwani
zinaangalia kwa karibu na tayari hata kwenye mpango wa wilaya, zimeshawekewa
mkakati wa kujengwa kwa kiwango cha lami.
“Kwa mfano
kama sisi Mei 22, mwaka huu baada ya kuharibika vibaya barabara hiyo,
tulishirikiana na baraza la Mji na wizara husika ya barabara, kuifanyia
matengenezo na sasa iko vizuri,’’aleleza.
Hivi
karibuni Afisa Mdhamini wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Pemba Ibrahim
Saleh Juma, alisema kwa barabara za ndani wahusika wakuu ni halmashauri au
mabaraza ya miji, ingawa wakati mwengine huzijenga hata kwa kiwango cha lami.
Barabara ya
Kijangwani- Birikau iliyomo baina ya majimbo ya Chake Chake na Ziwani ambayo
ina urefu wa wastani wa kilomita 3.7 imeasisiwa zaidi ya miaka 50 iliyopita,
ingawa bado kwa siku za mvua hairuhusu gari kupita.
Mwisho
Comments
Post a Comment