NA HAJI
NASSOR, PEMBA
WANAWAKE
wenye ulemavu kisiwani Pemba, wamewataka wazazi na walezi wa watoto
wenyeulemavu, kutokubali kurubuniwa kwa fedha au kitu chochote cha mali, mara
baada ya watoto wao, kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Walisema wadhalilishaji wamekuwa wakitumia mwanya wa
umaskini wa wazazi na watoto hao, mara wanapogundulika kuwatendea udhalilishaji
watoto wenye ulemvu, kama sehemu ya kuwarubuni, ili kesi hizo zisiendelee.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati
tofauti, walisema wakati umefika sasa kwa wazazi na walezi kutokubali kuingizwa
kwenye mtengo wa kuua kesi, kwa masharti ya kupewa mali.
Mjumbe wa kamati tendaji ya Jumuiya ya wanawake wenye
ulemavu Zanzibar ‘JUWAUZA’ Hidaya Mjaka Ali alisema, kutokana na wazazi na
walezi wenye watoto wenye ulemavu kuishi katika umaskini wa kipato, ndio maana
wadhalilishaji wamekuwa wakitumia, fursa hiyo.
Alieleza kuwa, wadhalilishaji wanapoona kesi imewaelekea,
huanza kuwarubuni kwa kuwaomba radhi, na kisha hufuatiwa na kiasi fulani cha
fedha, famili ya mtoto, ili kuipoza kesi hiyo.
‘’Kwanza kama hali zetu za kipato ni duni tuzikubali kwa
kuishi nazo, lakini tusitafute kupunguza ukali wa maisha kwa fedha za watoto
waliodhalilishwa,’’alieleza.
Hata hivyo mjumbe huyo wa ‘JUWAUZA’ aliwakumbusha wazazi
na walezi hao kushirikiana kikamilifu na vyombo vya ulinzia na usalama, wakati
inpotokezea udhalilishaji kwa watoto wao.
Nae mjumbe wa ‘JUWAUZA’ wilaya ya Micheweni Fatma Ramadhan
Shaib alisema, bado wazazi na walezi wanadhani inapotokezea mtoto kudhalilishwa,
suluhisho ni kukaa chini ya kuimaliza kienyeji.
‘’Haingii akili kuwa mtoto mwenye ulemavu
ameshadhalilishaji, na kisha kwa umaskini wa wazazi au walezi wakubali kuchukua
fedha, au kupewa ardhi ili kesi imazike, hili sio sahihi,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mjumbe huyo wa ‘JUWAUZA’ aliviomba
vyombo vya kusimamia sheria, kulisaidia kundi la watu wenye ulemavu, kutokana
na mazingira yao.
Nae Mwakilishi wa watu wenye ulemavu kisiwani Pemba
kwenye baraza la taifa la vijana Zanzibar, Katija Mbarouk Ali alisema utamduni
wa kuyamaliza kienyeji, umekuwa ukijitokeza hasa ikitokezea aliyefanyiwa
vitendo ya udhalilishaji, ni mtoto kiziwi.
‘’Mara nyingi wadhalilishaji wamekuwa wakiwadhalilishaji
watoto wenye ulamvu na hasa wenye ulemavu wa uziwi au viungo wakijua hawawezi
kufuatilia wala kutoa ushahidi mahakamani,’’alieleza.
Kwa
upande wake Afisa Mipango wilaya ya Chake chake, Kassim Ali Omar, amesema
watoto wenye ulemavu wamekuwa wakifanywa kama mtaji na baadhi ya wazazi na
walezi inapotokezea udhalilishaji.
‘’Wazazi
na walezi waelewe kuwa, haki za watoto wao wanazomikononi mwao, hivyo kama
wakiamua bora kuchukua fedha au mali nyingine kuua kesi, wanawakosesha haki
watoto hao,’’alieleza.
Afisa Elimu na Mafunzo ya Amali wilaya ya Chake chake,
Bur-han Khamis Juma alisema, wapo wanafunzi wenye ulamavu wamekuwa wakikosa
mtiririko mzuri wa masomo, hasa baada ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
‘’Ni vyema katika vyombo vya sheria kama vile mahakama,
kuwe na adhabu ya zaida kwa wale washtakiwa, watakaotiwa hatiani kwa
kuwadhalilisha watoto wenye ulemavu,’’alishauri.
Hata Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari wanawake
Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said, alisema pamoja na
yote, hayo ni vyema kwa wazazi kuzingatia umuhimu wa kutoa ushahidi mahakamani.
‘’Zipo kesi kadhaa zimekuwa zikifutwa mahakamani, kwa
sababu ya wahusika kutofika mahakamani, na hivyo kurejesha nyuma jitahada
zinazochukuliwa,’’alifafanua.
Naibu mrajisi wa mahakama kuu Pemba Faraj Shomar Juma,
alisema moja ya jukumu la wazazi na walezi, ni kuhakikisha wanawawekea ulinzi
watoto wao, kama sheria ilivyotamka.
‘’Ukiangalia sheria ya Mtoto nambari 6 ya Zanzibar ya
mwaka 2011, inahimiza ulinzi kwa mzazi au mlezi kwa lengo la kumkinga na
majanga likiwemo la udhalilishaji,’’alifafanua.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud,
akizungumza hivi karibu na kamati ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili,
alisema jambo kubwa ni kuhakikisha jamii inashirikiana.
Mwisho
Comments
Post a Comment