NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ WANANCHI wa shehia ya Mtambwe kusini wilaya ya Wete Pemba, wamesema kwa sasa huduma ya maji safi na salama katika vijij vyao, inapatikana kwa urahisi, tofauti na hapo zamani. Walisema, kwa sasa wamekuwa na wakati mzuri wa kujipangia shughuli zao mbali mbali za kimaisha, na wala upatikanaji wa huduma hiyo, sio changamoto inayowatengulia rataiba zao za kimaisha. Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika kijijini hapo, walisema kwa sasa huduma hiyo, iko karibu vijiji vyote, tena bila ya mgao, jambo ambalo limechangia kufikia malengo yao. Walieleza kuwa, upatikanaji wa huduma hiyo kwa miaka minne mfululizo sasa, unawapa uhakika wa maisha yao, hasa kwa vile kila mmoja, anaendesha shughuli zake kwa urahisi. Salma Hamad mkaazi wa kijiji cha Kivumoni, alisema kwa sasa huduma hiyo iko vyema na haina shida kwao, ikilinganisha na miaka 20 iliyopita. ‘’Awali sisi wananchi wa kikijiji cha Kivumoni shehia ya Mtambwe kusini, tukifuata maji masafa ya m...