NA HANIFA SALUM, PEMBA
AFISA Mdhamini ofisi ya Rais Fedha na Mipango Pemba, Abdul-wahab Said Abubakar amezitaka taasisi za umma, kuhakikisha zinatayarisha nyaraka zote za watumishi wao, wanaotarajiwa kustaafu, ili waweze kupata haki zao kwa haraka kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar 'ZSSF'.
Aliyasema hayo alipokuwa akifungua, mkutano maalumu kwa wastaafu watarajiwa, uliofanyika katika ukumbi wa ZSSF Tibirinzi Chake chake Kisiwani Pemba.
Alisema kuwa, wastaafu wanahitaji matayarisho maalumu kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa kisheria ambao utasaidia kupata stahiki zao kwa wakati sahihi mara tu watakapostaafu.
"Sote tunafahamu kwamba watumishi wa umma wameitumikia serikali, na kuchangia kurithisha elimu kwa watumishi wengine sasa ni vizuri stahiki zao ziandaliwe mapema ili kuwasaidia kufikia malengo waliojiwekea baada ya kustaafu", alisema.
Aidha, Mdhamini huyo aliwataka wastaafu hao watarajiwa kuendelea kuwahimiza watumishi wengine katika maeneo wanayofanyia kazi wafanye kazi kwa bidii na kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya taifa lao.
Nae, Meneja wa ZSSF Pemba Said Salim Maalim alisema, ukomo wa kufanya kazi kwa watumishi wa umma unahitaji matayarisho na mandalizi ya mapema ndio maana ZSSF ikaandaa mafuzo ambayo yatawasaidia wastaafu hao kuwa katika mazingira mazuri watakaporudi kwenye jamii.
Alisema, kwa sasa mfuko umeweka taratibu maalumu za upatikanaji wa mafao kwa wastaafu kwa haraka kutokana na kutumia mifumo ya kisasa ya utowaji huduma ambapo msataafu hupata mafao yake ndani ya siki 14.
Mapema, kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha uhusiano na elimu ZSSF Raya Hamdani Khamis, alieleza lengo la kuwapa taaluma wastaafu hao watarajiwa ni kuwasaidia kuweza kujua maeneo ya kupata na kuyatumia mafao yao.
Akiwasilisha mada kwa wastaafu watarajiwa hao Daktari kutoka Hospitali ya Chake chake Rahila Salum Omar aliwataka wajenge utaratibu wa kupima afya zao ili kuweza kubaini changamoto zinazoikabili miili yao na kuifanyia matibabu kwa haraka.
Kwa upande wao wastaafu hao waliishauri ZSSF kuweka hospitali maalumu ya wastaafu Pemba ambayo itatoa huduma za matibabu kwao kama ilivyo kwa nchi nyengine.
Katika mkutano huo wa wastaafu watarajiwa walipatiwa mafunzo na maelekezo kuhusu kupata mikopo kupitia benki mbali mbali ikiwemo PBZ benki, CRDB benki, Amana benki na Tanzania Commercial benki.
MWISHO.
ReplyForward |
Comments
Post a Comment