NA ZUHURA JABIR, ZANZIBAR @@@ Wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya familia, jamii na taifa. Kwa miaka mingi, juhudi mbalimbali zimefanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na taasisi za kiraia ili kuhakikisha wanawake wanapata haki sawa za kushiriki katika uongozi na maamuzi ya maendeleo. Pamoja na hatua hizo, bado wanawake wengi hukutana na changamoto zinazowazuia kufikia nafasi za uongozi kutokana na mila na desturi, mitazamo hasi ya kijamii, ukosefu wa fursa za elimu na uwezeshaji wa kiuchumi. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, pamoja na marekebisho yake, na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 zinatambua usawa wa watu wote mbele ya sheria bila ubaguzi wa kijinsia. Aidha, Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolinda haki za wanawake, ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW), Itifaki ya Maput...