NA HAJI NASSOR, PEMBA
KAMANDA wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, amesema leo Mei 9, mwaka huu atatoa taarifa rasmi, juu ya kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana ya Polisi, daktari wa Kituo cha Afya Gombani Is-haka Rashid Hadid, anayetuhumiwa kwa ubakaji.
Alisema, kwa vile alikuwa katika mapumziko mafupi, haelewi jambo lolote linaloendelea kwa mtuhumiwa huyo, juu ya kuendelea kushikiliwa kwake kituoni hapo.
Alieleza kuwa, leo Mei 6 (jana), hajapata taarifa za ndani za mtuhumiwa, huyo na kuwataka wananchi na wanaharakati, wasubirie hadi Jumatatu ijayo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Kamanda huyo, alisema hana taarifa zozote za kupewa dhamana mtuhumiwa ndani ya kituo chake cha Polisi au kuendelea kuwepo.
‘’Ilikuwa mimi sipo kazini kwa muda, kuanzia anakamatwa hadi anafikishwa Polisi, kwa sasa siwezi kueleza jambo lolote kwa mtuhumiwa huyo, hadi Jumatatu,’’alieleza.
Aidha Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa sasa hawezi kutoa ufafanuzi wowote, juu ya taarifa zilizopo, kwa mtuhumiwa huyo.
‘’Kama amepata dhamana au bado yupo Polisi, nitafuatilia na kujua kwa kina, na Jumatatu ya Mei, 9 ndio nitatoa taarifa rasmi,’’alisema.
Awali Kamanda huyo, alikiri kushikiliwa kwa daktari huyo wa Kituo cha Afya Gombani wilaya ya Chake chake Is-haka Rashid Hadid, kwa tuhma za kumtorosha na kumbaka mgonjwa wake, ambae ni mtoto.
Mtoto huyo kabla ya kufanyiwa kitendo hicho April 21 mwaka huu, alidai kwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu, na baadae daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu.
"Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele sehemu zangu za siri, lakini dakati huyo akaniambia mpaka aje mwenzake, kwa hiyo kesho (siku ya pili yake), atakuja kunichukua, ili akanipe dawa nyingine", alidai mtoto.
Alisema kuwa, siku ya pili alipigiwa simu na mtuhumiwa na kumeleza kuwa, akirudi skuli amsubiri kwa rafiki yake, mpaka atakapotoka kazini, ili akamchukue kwa ajili ya kumpatia dawa nyingine,
‘’Alikuja kunichukua nikijua naenda kupewa dawa nyingine, kumbe alinipeleka hadi nyumbani kwake Kangangani wilaya ya Wete, na baada ya kunichunguuza virusi vya Ukimwi, alinifungia ndani kwa siku tano na kunibaka,’’alisimulia.
Kaimu Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba, Dk. Yussuf Hamad Iddi,alikiri kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, kwa mfanyakazi wao, ambae ni daktari wa kituo cha Afya Gombani, wilaya ya Chake chake.
Alisema hana taarifa rasmi, lakini baada ya kufuatilia wamebaini kuwa daktari huyo hajaacha kazi, bali anashikiliwa kwa tuhma za kutorosha na kubaka.
Tukio linalofafana hilo, liliwahi kutokea Novemba 21, mwaka 2019, katika hospitali ya Chake chake, baada ya daktari wa kitengo cha Atrasaund, kudaiwa kumuomba rushwa ya ngono mjamzito, kama sharti la kumpa huduma.
Aidha Disemba 18, mwaka mwaka 2019, TBC 1, iliripoti Afisa Muuguzi msaidizi wa kituo cha Afya Mamba, mkoani Katavi kushikiliwa na Jeshi la Polisi, kwa tuhuma za kumbaka mjamzito, wakati alipokuwa akimsaidia kujifungua.
Mwisho
Comments
Post a Comment