MIAKA 62 YA MAGEUZI MAKUBWA YA SEKTA YA AFYA KUTOKA UHABA, MARADHI NA VIFO VINAVYOZUILIKA HADI HUDUMA ZA KISASA KISIWANI PEMBA.
HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@ Mapinduzi ya 12 Januari 1964 ni tukio la kihistoria lililobadili mwelekeo wa maisha ya Mzanzibari katika nyanja zote za kijamii. Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikuwa ni Mapinduzi ya uhai yakitambua kuwa bila afya bora, hakuna maendeleo, hakuna elimu, wala hakuna uchumi. Miaka 62 ya mapinduzi hayo, sekta ya afya Zanzibar nzima inasimama kama ushahidi usiopingika kwamba Mapinduzi yamelinda maisha ya wananchi kwa vitendo. KABLA YA MAPINDUZI Kiuhalisia kwa upande wa kisiwa cha Pemba kabla ya Mapinduzi matukufu ya 1964, huduma za afya zilikuwa katika hali ya kusikitisha. Kwa vile Zanzibar nzima ilikuwa na hospitali kuu moja tu ya Mnazi Mmoja ni wazi kuwa kwa upande wa Pemba ilikuwa na huduma finyu sana za afya. Hakukuwa na hospitali kuu badala yake kulikuwa na hospitali 2 ya Chake chake na Wete, kwa upande wa vituo vya afya vilikuwa ni 14 tu huku vikiwa havina dawa wala wataalamu wa kutosha. ...