HANIFA
SALIM, PEMBA:::
NI
mwendo wa takribani kilomita 2.5 kwa usafiri wa gari binasfi, kutoka mjini
Chake chake hadi kijiji cha Pembeni ya Muangaza kilichoko jimbo la Ziwani wilaya
ya Chake chake.
Kijiji hicho kiko Magharibi mwa kisiwa cha Pemba, kina
wakaazi zaidi ya 800, ambao wanajishughulisha na kazi mbali mbali ikiwemo ujasiriamali,
kilimo na uvuvi.
Wengine na hasa wanawake wamjitupa kwenye ubunifu
wa kutengeneza vyombo mbali mbali kwa kutumia rasilimali ya udongo maalumu.
Sikuwa na nia ya kwenda kufanya utalii wa ndani
katika kijiji hicho, bali nilikuwa na shauku kubwa ya kuangalia ubunifu na
usarifu wa udongo unaofanywa na wanawake hao.
Wananawake wa kijiji cha Pembeni ya Mwangaza,
wakubwa na wadogo wanajishughulisha na kazi hiyo, hatimae kuzalisha ajira kwao
na watu wengine.
Wanawake wa kijiji hicho hutumia muda wao mwingi
kwa ajili ya kufanya kazi hiyo, ambayo huwapatia kipato cha kuendeleza maisha
yao ya kila siku.
Ikiwemo kuwapatia watoto mahitaji yao muhimu ya
kielimu na matibabu, kutokana na ubunifu huo bila ya kumtegemea baba ‘mume’
ambae nae ana majukumu mengine.
Kazi hiyo imeweza kuwapa maslahi makubwa akina mama
wa kijiji hicho, na hatimae kupatikana ule msemo unaosema ‘kazi ni kazi alimradi mkono uwende
kinywani’.
Licha ya mafanikio ambayo wanaendelea kuyapata
wanawake hawa kwa ufinyanzi wa vyomvo vya udongo, lakini waliona ili kufikia
ndoto zao ni kuanzisha kikundi cha ushirika.
‘ZINA MOLA’
Ushirika huo ulioanzishwa mwaka 2020, baada ya
kurudi kwenye maonesho yaliofanyika Chamanangwe Pemba, kina wanachama tisa ‘9’
wanawake wakiwa wanane na wanamme mmoja.
“Tulipokwenda katika maonesho ya chakula Chamanangwe
wilaya ya Wete, tulipata fursa ya kuonesha bidhaa zetu kama wajasiriamali
tukajifunza mambo mengi ndiporudi tulianzisha ushirika huu”, anasema Katibu
Mtumwa Amour Juma.
Kwenye ushirika huo, wanajishughulisha na
utengenezaji wa vyombo mbali mbali vya matumizi ya nyumbani, kama vile mitungi,
vyetezo, mikungu, vijungu, majiko, sahani na vikombe.
“Tunanufaika sana na hichi kikundi, licha ya
changamoto tunazozipata, lakini tunazichukuwa kama ni fursa kwetu ya kusonga
mbele kimaendeleo, kwani inatusaidia kupunguza nguvu ya ukali wa maisha,”
anasema.
Kazi hiyo ndio inayowaendeshea maisha yao ya kila
siku kwa kujipatia mahitaji yao ya lazima kama vile chakula, kulipia ada na
matibabu pamoja na kuweka hakiba zao benki.
Wanaiona faida ya ufinyanzi, na ndio maana
wanaendelea na kazi hiyo inayowapatia kipato, mbali ya matumizi waliyonayo
lakini wanahakiba ya zaidi ya shilingi milioni 2.5 benki.
Katika kuhakikisha wanafanya kazi yao vizuri, wanasema
wamezalisha zaidi ya vyombo 1000 kwa ajili ya kuuza kwenye masoko mbali mbali,
licha ya kuwa hawana soko la uhakika.
Mwanaushirika Hadia Muhidini Haji anasema,
anaishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono, wajasiriamali kwa kila hatua ambazo
wanapitia.
Anasema, ufinyanzi wao ni katika kipindi cha jua kali,
tu kwani kipindi cha mvua hawawezi kufanya kazi zao kutokana na kukosa ofisi
ambayo wangeweza kuweka bidhaa zao.
Kwa siku huchoma wastani wa vyombo 200 hadi 250,
katika hatua za uchomaji wa vyombo huchukuwa muda wa siku mbili hadi tatu.
Bidhaa zao wanauza kwa jumla na reja reja kwa bei
tofauti ambapo mikungu na vyungu huuza kwa bei ya shilingi 2,500 hadi 3000 na
vietezo shilingi 4000.
“Kutokana na utengenezaji wa kietezo kuwa mgumu
zaidi ya mkungu au chengine lazima bei yake iwe tofauti, kwani kietezo
kinachukua muda wa wiki moja kukitengeneza hadi kumalizika,” anasema.
Anaiomba serikali kuendelea kuwaangalia
wajasiriamali kwa moyo wa huruma, kuwapatia mikopo ili wafanye biashara zao kwa
kurejesha na wengine wapatiwe fursa ya kukopa.
Nae Furaha Kheir Juma (76) mlezi wa kikundi hicho
anasema, utamaduni huo ambao wanauwendeleza ni urithi kutoka kwa wazee wao
ambao wakiufanya.
Anasema, unapotengeneza vyombo hivyo unafinyanga
udongo na kuutoa vijiwe vyote, unaweka dizaini unayotaka baadae unavieka juani
kwa ajili ya kukauka na kushikana.
“Baadae unapoona kimekauka kuna vifaa vinaitwa Muwale, Kuungo na kisahani hivi kwa kutengenezea kwa kupamba unavotaka baada ya kutulia kuna kuungo unaekea sawa na kiwe kwenye muonekano mzuri,” anasema.
Bidhaa kutokana na utengezaji wake ni kwa kutumia udongo hawawezi kuuza nje ya visiwa vya Zanzibar, kwani katika usafirishaji wanaweza kupata hasara kubwa kinyume na ambavyo wanategemea.
Serikali katika kuwaunga mkono imekuwa ikiwapatia
misaada mbali mbali ikiwemo, elimu ya uhifadhi wa fedha, mafunzo ya kibiashara
na namna ya kulinda bidhaa zao.
Bidhaa zao wanauza kwa wafanyabiashara, matajiri
mbali mbali na zinapotokea fursa za maonesho wanauza zaidi, lakini baada ya
Serikali kujenga vituo vya wajasiriamali matumaini yao kupata soko la uhakika.
“Hatuwezi kuajiriwa sote serikalini kutokana na idadi
yetu kuwa wengi, lakini kujiongeza kwetu kwa kusarifu udongo kumeweza kutupatia
mafanikio makubwa,’’anasema.
“Na hatuna wasi wasi wa matumizi madogo madogo” ni
kauli ya mama mmoja ambae nilikutana nae katika kijiji hicho ambacho hadi sasa
kimebarikiwa kuwa na rangi ya kijani kibichi.
Anasema, changamoto ambazo zinawakabili ni pamoja
na utafutaji wa malighafi za kuchomea vyombo vyao (Magubi-kozi) ambayo
inapatikana katika wilaya ya Mkoani, usafiri ambapo hulazimika kukodi magari
binafsi, na ofisi.
Ameiomba serikali iwasaidie mashine ya kukandia
udongo kutolea vijiwe ambao hulazimika kukanda kwa kutumia vifua jambo ambalo
linaweza kupelekea ubovu wa afya zao.
Baada ya hapo huvieka ndani vikauke kwa unyevu
unyevu wa joto kwani vinapokiekwa juani vinaweza kukapasuka na kula hasara,
kinachoekwa juani kwenye bidhaa za udongo ni mkungu pekee.
Anasema, vijana wengi wa sasa hawajui umuhimu wa
kutumia vyungu na vyombo vya udongo wamezoea kutumia masufuria ambayo anasema
maradhi mengi ya tumbo hutokana nayo.
Wazee wao wa zamani wakinywa chai katika vikombe
vya udongo (Mabunguu), mabakuli ya kukunia nazi wakitengeneza kwa udongo, ya
kuvumbikia maziwa na hata wali na muhogo wakipika ndani ya vyungu.
Kuna tofauti kubwa kati ya chakula kinachopikwa
ndani ya chungu na sufuria, mchuzi unaopikwa ndani ya chungu huwa na ladha tamu
zaidi kuliko sufuria.
Anaishauri jamii irudi katika kutumia utamaduni na
asili ya vyombo vya udongo ambavyo havina madhara na kuacha kutumia masufuria
ambayo yanatengenezwa kwa kutumia bati.
Mtoto Hamida Juma Amour (17) ni mjasiriamali mtoto
ambae amerithi ubunifu wa kusarifu vyombo vya udongo kutoka kwa bibi yake
anasema, anajivunia kujua fani hiyo ambayo wengine hawaijui.
Anasema tangu anasoma alikuwa anajifunza ujuzi huo
kwa wazazi wake na baada ya kumaliza kusoma kidato cha nne alijiunga na ujuzi
huo ambao kwa sasa anajivunia kuupata.
“Ili kuona sisi tunaiendeleza asili ya Kijiji hichi
cha Pembeni ambayo tuliirithi kutoka kwa bibi zetu basi tutaiendeleza
kuhakikisha vizazi vyetu vinajifunza na kuwarithisha wengine,” anasema.
WATEJA
WA VYOMBO VYA UDONGO
Mwanajuma Khamis Hamad wa Chake chake anasema,
amekua akivutiwa na vyombo vilivyotengenezwa na rasilimali ya udongo kutokana
na kuwa chakula chake ni chenye ladha pekee.
Asha Rajab Mohamed wa Machomane anasema, amekua
akinunua vifaa hivyo na kuuza katika duka lake na kujipatia umaarufu mkubwa.
‘’Wazee wetu wa zamani walikua wakitumia vyombo vya
udongo wakipika vyakula vyote kwenye masufuria na vyungu lakini sasahivi
utamaduni umepotea, nawashauri akina mama turejeshe hii asili yetu,’’ anasema.
TAMWA
Afisa Miradi kutoka Chama cha waandishi wanawake
Tanzania TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba Asha Mussa Omar, anasema hawana shida na
hilo, ingawa wanategemea zaidi miradi.
Anasema, kama ikitokezea wamepata mradi,
watawaingiza kwenye mchakato, ili nao wafikie ndoto zao kama walivyo wanawake
wengine.
‘’Kwa sasa hatuna mradi kwa ajili ya kuwanunulia
mashine ya kuchakata udongo, lakini kama wanahitajia uwezeshwaji mwengine
wafike ofisini,’’anasema.
SERIKALI
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2022/2023
ndani ya baraza la wawakilishi Waziri wa Afisi ya Rais Kazi uchumi na uwekezaji
Mudrik Ramadhan Soraga anasema, mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa
kushirikiana na taasisi za kifedha, umejipangia kutoa mikopo 2,000.
Anasema, mikopo hiyo ina thamani ya shilingi bilioni
3 kwa vikundi vya kiuchumi katika sekta zote za kiuchumi, kuangalia fursa mpya
ambazo zinaweza kutekelezwa na wananchi.
Aidha katika bajeti hiyo waziri Soraga ameahidi,
kuendelea na juhudi za kutunisha fedha ili mfuko uendelee kuwasaidia
wajasiriamali wengi zaidi.
‘’Pia kuimarisha mashirikiano na uratibu wa shughuli
za mikopo nafuu hapa nchini pamoja na kuimarisha mashirikiano na taasisi
zinazotoa mikopo nafuu,’’ anasema.
Jumla ya vyama vya ushirika 1,848 vimesajiliwa na
kati ya hivyo Unguja 709 na Pemba 1,139 pamoja na vyama vya uzalishaji na
utoaji wa huduma 910, vinavyojishughulisha na utengenezaji sabuni, SACCOS, ukataji
miwa, uvuvi, ufugaji kaa, kilimo pamoja na usafi wa mazingira.
MWISHO.
Comments
Post a Comment