NA HANIFA SALIM, PEMBA UCHUMI wa buluu ni shughuli za kiuchumi zinazohusu matumizi bora ya rasilimali za bahari kwa ajili ya kuimarisha au kukuza pato la wavuvi na taifa. Kuna nafasi kubwa na nzuri ya kuifanya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuwa na uchumi mzuri zaidi kwa kuifanyia maarifa zaidi ‘ Blue Economy’ . Elimu na mafunzo katika uchumi buluu inapaswa kuratibiwa vizuri ili kukuza ukuaji wa sekta ya bahari, kwa hivyo unaweza kutoa moja ya fursa kubwa zaidi kwa mafanikio ya biashara. Sio kitu cha ajabu kwa Zanzibar kusikia neno uchumi wa buluu, ambapo ikiwa na maana kuwa ni shughuli zote za uendelezaji na ukuzaji wa uchumi kupitia matumizi bora ya rasilimali zote muhimu za bahari. Dhana nzima ya uchumi wa buluu ni pana, ambayo imebeba shughuli zote za msingi zinazofanywa katika bahari kama vile, uvuvi wa aina mbali mbali ikiwemo raslimali zote zitokanazo na bahari. Ikiwemo uvuvi wa kibiashara na usio wa kibiashara katika kina kirefu na kifupi cha maji...