Vikausha damu vya mjamzito hivi hapa, umo mchele, udongo, mkaa, chaki Uwezekano wa kuzaliwa watoto wenye udumavu, utapiamlo ni mkubwa
‘’KILA
ninapobeba mimba nimezoea kula mchele kwa wingi naweza kusamehe pilau au
biriani,’’ ndio maneno ya mwanzao ya Bahati Mohamed Ali (sio jina lake halisi).
Nilimfuma akiwa barazani kwake,
mjini Ole wilaya ya Chake chake, pembeni yake akiwa na kibakuli cha mwazi, kwa
umbali utaona amejaza chakula aina ya pepe, kumbe ni mchele wa Mbeya.
Hujichotea kidogo kidogo na
kuushindilia mdomoni mwake, huku akiendela kupiga storia na wenzake, bila ya
kujali kuwa ujauzito alionayo na mchele huo hauna mwisho mwema.
Kawaida yake akiwa mjamzito, kila
anapoamka asubuhi anaroweka mchele upatao robo kilo hivi…na baada ya kumaliza
kupika, yeye huchukua mchele wake kutafuna (kula).
Wakati mwenza wake na watoto wao,
wanakula chakula cha mchana, Bahati yeye hukaa pembeni na kibakuli chake cha mchele
akiendelea kubahatisha afya yake.
‘’Mimba nyengine hupenda sana
kutafuna mchele wa Mbea na nyengine hupenda mchele wa mapembe, kwa kweli huwa
nina hamu (kileo), kwani ikiwa nitakosa sipati hata usingizi,’’anasema Bahati.
Siku zote akiwa mjamzito, faradhi
yake ya chakula cha mchana huipunguza kwa ajili ya kula mchele mbichi, uliolainika
kwa maji, na kisha siku hiyo kwake kuihesabu imeshapita.
Anakiri kuwa, wanapofika kituo
cha Afya, moja ya jambo wanalosisitizwa wasilitumie ni mchele, udongo, chaki
wakielezwa kuwa vinakausha damu yake na mtoto.
‘’Mimi najua kuwa unapokula vitu
kama hivi ikiwa na mimba havikuathiri lakini nikienda kliniki kupima damu
imepungua, kumbe itakuwa ni huu mchele,’’ anasema.
Kumbe sio tu Bahati pekee,
anayebahatisha afya akiwa na ujauzito, bali ni wanawake wengi wenye tabia hiyo,
huku wakidhani kuwa hakuna madhara yeyote yanayoweza kuwapata.
Mama mmoja mkaazi wa Bopwe Wete
ambae hakutaka jina lake litajwe anasema, yeye anapokuwa mjamzito hupenda sana kula
udongo na hupata tabu sana ikiwa ataukosa.
‘’Huwa unauzwa kwenye baadhi ya
maduka, kwa hiyo unaponimalizikia nanunua mwingine, mpaka najifungua na ndio
akili yangu inakaa sawa,’’ anahadithia.
‘’Siku moja nilienda sehemu
ambayo naficha udongo wangu lakini sikuukuta kwa iyo akili yangu ikawa haipo
sawa na ni usiku wa 4:30, nilimtoa mume wangu akaununue na alikwenda, huwa kama
nimechanganyikwa vile,’’ anasimulia.
Anaeleza kuwa, mume wake alikuwa
na kawaida ya kumkataza kula udongo na ndio maana siku hiyo akamtoa usiku
akaununue, kwani alihisi kuwa aliutupa yeye.
Maryam Khamis mkaazi wa Micheweni
yeye anasema, mimba ya mtoto wake wa pili, aliwahi kuingiwa na hamu (kileo) ya kula
mawe ya jasi na alikuwa hawezi kulala kama hajatafuna.
‘’Kwa kweli mimba ni kitu chingine
kwa sababu, mimi ilinijia hiyo karibu na kujifungua na baada ya kujifungua moyo
wangu ulitulia, mpaka leo hii,’’anaeleza.
Anasema, wajawazito wanapokwenda
kliniki wanaaswa wasitumie vitu hivyo, ingawa mimba zinawapelekesha kiasi
kwamba, hawataki kuufanyia kazi ushauri wa daktari.
Aisha Omar Salum ambae ni Mkunga
na Muuguzi wa kituo cha Afya Maziwang’ombe anasema, hali hiyo huwatokea baadhi
ya wajawazito, kutokana na upungufu mkubwa wa madini ya chuma na zinki.
Hivyo ubongo unawapelekesha
kutafuta vile vitu ambavyo ataweza kupata madini hayo, jambo ambalo sio sahihi,
kwani kuna vyakula kama vya mazao ya baharini ambavyo akitumia anapata madini
hayo.
“Huwa sio yeye bali ni ubongo unamuamrisha
kula kitu Fulani, na hiyo inatokana kwenye mwili wake kumekosekana kitu, ndio
maana inampelekea kutamani,”anasema.
Mkunga huyo anasema, mjamzito
kutumia vitu visivyo vyakula sio sahihi kwa sababu, anaweza kupata madhara yeye
na mtoto wake, ikwemo upungufu wa damu.
Mjamzito anapokuwa na upungufu wa
damu, hata mtoto wake pia hukumba, kwa sababu wakati ule kila kitu anategemea,
kutoka kwa mama yake.
“Kutokana na hali hiyo mtoto
hakui vizuri kimwili na kiakili na hatimae, anaweza kuzaliwa akiwa na udumavu
na kukosa ufahamu,” anaelelza.
Daktari huyo anafafanua kuwa, mjamzito
anaetumia vitu hivyo, anaweza kuzaa, mtoto ambae atakuwa na uhaba wa damu,
ambapo huhitajika kuingiziwa damu papo hapo, jambo ambalo sio zuri.
Dk. Rahila Salim Omar ambae ni
Mratibu wa kliniki za huduma na tiba kwa wanaoishi na VVU Pemba anasema,
vyakula visivyo vyakula kama udongo, mkaa, chaki, mchele na mengine
yanayofanana nayo, si vyema kula kwa mama mjamzito.
Kwani vitu hivyo vinasababisha
madhara kwa mama na mtoto, ikiwa ni pamoja na upungufu wa damu, kuzaliwa mtoto
ambae ana udumavu.
‘’Tunajitahidi kuwafahamisha
wajawazito kuwa vitu hivi havina faida kwao, lakini hii inakuwa kama ni kileo,
hivyo ni vigumu kumshauri mama huyu na akakusikiliza,’’ anaeleza.
Anaeleza, wajawazito wengi
wanakula vitu ambavyo sio sahihi kwa afya, jambo ambalo humsababishia kukosa
damu na hatimae kuzaa mtoto akiwa na matatizo mengi.
Afisa Mtendaji wa Maabara ya Afya ya Jamii Pemba Said Mohamed Ali anasema
kuwa, walifanya utafiti mwaka 2011/2012
kujua sababu zinazomfanya mama mjamzito kula vitu hivyo, ambapo waligundua kuwa
ni ukosefu wa madini ikiwemo ya chuma na culsium.
Anasema, ukosefu wa madini ya
chuma inasababisha mtu kuwa na safura na ndio maana mjamzito anapokosa, inamjia
ale kitu ambacho atayapata, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara kiafya.
‘’Madhara yanayopatikana
inategemea na vitu anavyokula, vyengine haviwapi madhara na vyengine vinawapa
madhara, lakini huwezi kujua ni kipi kisicho madhara, ,’’ anaeleza.
Ali Hassan Bakar mkaazi wa Limbani
Wete anasema, akinamama wajawazito wanapoamua kula kitu Fulani, hakuna ambae
ataweza kumzuia, jambo ambalo linawapa wakati mgumu sana wanaume.
‘’Na sisi huwa tunaamini kweli
kutokana na kuwa akishakujifungua anakuwa sawa na wala hatumii tena vitu hivyo,
kwa hiyo ikiwa anataka udongo sisi ndio wanunuzi wakuu kwa kweli’’, anasema
baba huyo.
Mkaazi wa Chanjaani Chake Chake Suleiman
Khamis Said anaeleza kuwa, mwanamke anapokuwa katika hali ya ujauzito, anakuwa
hayupo sawa kiakili na hata kimwili.
NINI KIFANYIKE?
Dk. Aisha anawashauri akinamama
wajawazito kuweka vitu mbada kama chipis za muhogo, chauro na njugu ili pale
inapowajia hamu ya kula, wavitumie badala ya mawe na udongo.
Aisha anawashauri akinamama hao kula vyakula
vya mboga, matunda na maji mengi ili kuimarisha afya yake na mtoto atakaezaliwa.
Dk. Rahila anawashauri mama
wajawazito kuacha tabia ya kula vitu hivyo na badala yake wale vyakula vyenye
lishe, ili awe salama tangu siku ya kutunga mimba, mpaka kumlea mtoto.
Anasema kuwa, endapo mama
mjamzito atakosa lishe bora, hata mtoto anapozaliwa anaweza kupata udumavu na
utapiamlo, hivyo wanaume waelewe umuhimu virutubisho kwa wenza wao.
Afisa Mtendaji wa Maabara ya Afya
ya Jamii Wawi Chake chake, ‘PHL’ Pemba anawashauri
mama wajawazito wasitumie vitu hivyo, ambavyo havina faida kwao.
‘’Elimu kwa jamii inahitajika
kuhusu afya ya uzazi, ili wanawake wanapokuwa wajawazito waweze kuimarika kiafya,’anaushauri.
MWISHO.
Comments
Post a Comment