NA HAJI NASSOR, PEMBA::: IDARA ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, ofisi ya Pemba, imewakumbusha wanafunzi wa madrassa za qur-an kisiwani Pemba, kujitenga mbali na watu wanaowanesha dalili za vitendo vya udhalilishaji, ikiwa ni pamoja na kuwawekea picha chafu kupitia simu zao. Kauli hiyo imetolewa leo Januari, 7 2023 kwa nyakati tofauti, na mwakilishi wa Idara hiyo Mohamed Massoud Said, wakati akizungumza na wanafunzi wa madarassa za Vikunguni na Machomane wilaya ya Chake chake, kwenye ziara maalum, ya kutoa elimu ya kupambana na matendo hayo. Alisema, moja ya dalili ya mtu anaetaka kumdhalilisha mtoto huanza kwa kumuonesha picha za ngono, kumnunulia zawadi, kumpa fedha, na kuendelea kwa maneno ya ushawishi juu ya udhalilishaji. Alisema ni jukumu lao, kwanza kutoshirikiana na watu wa aina hiyo, hata ikiwa ni wazazi wao, au kutoa taarifa kwa watu wengine, kabla ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji. Mwakilishi huyo wa Idara ya Katiba na msaada wa kisheria, ...