NA HAJI NASSOR, PEMBA MKURUGENZI wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, amesema msako mkali unakuja kuwabaini watu na taasisi, zinazofanyakazi za kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria, pasi na kujisajili kama sheria inavyotaka. Alisema, Sheria ya namba 13 ya mwaka 2018 ya Msaada wa Kisheria Zanzibar, inamtaka mtu yeyote au taasisi inayotaka kujishughulisha na kazi hiyo, kwanza kujisajili, ili kuwa halali kufanya kazi hiyo. Alieleza kuwa, Idara imebaini wapo watu na hata taasisi zinaendelea kutoa ushauri, msaada na elimu ya kisheria, bila ya kujisajili, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria hiyo. Mkurugenzi Hanifa, aliyasema hayo Septamba 16, 2023 ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta ya Makoyo Wawi Chake chake Pemba, wakati akijibu hoja za baadhi wa wahusika wa msaada wa kisheria, kwenye mkutano wa nusu mwaka, ambao umeandaliwa na Idara hiyo, kwa kushirikiana na UNDP. Alieleza kuwa, msako utanzia katika wilaya za Wete, Micheweni, ...