NA
HAJI NASSOR, PEMBA::
ASKARI
mpelelezi wa kituo cha Polisi wilaya ya Chake chake Lailat Mgindo Nassor, amedai
mahakamani kuwa, taulo aliyoitaja mtoto, kuwa alikuwa ameivaa mtuhumiwa, kabla
ya kumbaka, ndio aliyoikuta chumbani mwake, wakati wa upekuzi.
Alidai kuwa, kielelezo
chengine kilichompa uhakika kuwa, mzee huyo wa miaka 76, ndie aliyembaka mtoto
huyo wa miaka 13 ni kukimbilia mkoani Tanga, mara baada ya walalamikaji kutoa
taarifa kituo cha Polisi.
Askari huyo mpelelezi, alidai
hayo mbele ya mahakama maalum ya makosa ya udhalilishi ya mkoa wa kusini
Pemba, wakati akitoa ushahidi wake, huku akiongozwa na wakili wa serikali, Ali
Amour Makame.
Alidai kuwa, wakati familia
ya mtoto huyo ilipofika kituo cha Polisi kutoa taarifa, walifika nyumbani kwa
mtuhumiwa huyo kwa ajili ya kumkamata, ingawa alishatoroka na kwenda mkoani
Tanga.
‘’Nilijua kuwa alikuwa
mkoani Tanga, maana Jeshi la Polisi liliwakamata watoto wake na kuwaweka ndani,
ingawa wiki mbili baadae, mtuhumiwa alifika kituo cha Polisi mwenyewe, na
watoto wake kuachiwa,’’alidai.
Aidha askari huyo mpelelezi
alidai kuwa, baada ya kufika kituo cha Polisi Mei 30 mwaka huu, waliambatana na
mtoto aliyedai kubakwa hadi nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Mtoni wilaya ya
Chake chake, kwa upelelezi zaidi.
Aliendelea kudai kuwa, baadhi
ya vielelezo kama vile taula, mashuka na seruni ambazo mtoto alizitaja,
walizikuta chumbani mwa mtuhumiwa.
‘’Mtoto alitupitisha mlango
wa nyuma, ambako kuna migomba na ndio mlango aliopitishiwa na mtuhumiwa kabla
ya kubakwa siku ambayo alida alimuita kwa ajili ya kumtuma dukani,’’alidai.
Kwa upande wake shahidi
daktari wa hospitali ya Chake chake Fatma Kassim Ali alidai kuwa, baada ya
kumfanyia uchunguuzi mtoto huyo, aligundua kuwa anamichaniko na mipasuko
mikongwe kwenye sehemu yake ya siri ya mbele.
Alidai kuwa, michaniko hiyo
inaweza kusababishwa na mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuingiliwa, kuchanika
kwa kufanya mazoezi au kuingizwa kitu mithili ya vijiti au kidole.
‘’Ni kweli mtoto nilimgundua
na michaniko kwenye sehemu zake za siri, lakini inaonesha ni ya zamani kama
mwaka mmoja uliopita, maana kama ni mipya damu au unyevu unyevu wengekuwepo
unaoashiria maumivu,’’alidai.
Awali mara baada ya
mtuhumiwa huyo kuwasili mahakamani hapo akitokea rumande, Mwendesha mashataka
kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa mashataka Ali Amour Makame, alidai kuwa shauri
hilo, lipo mahakamani kwa ajili ya kusikiliza mashahidi.
Mara baada ya mashahidi hao
wawili kumaliza ushahidi wao, na kutimiza idadi ya mashahidi wanne, Hakimu wa
mahakama hiyo Muumini Ali Juma, aliupa nafasi upande wa utetezi kuwauliza
maswali mashahidi hao.
‘’Kwanini Jeshi la Polisi
liliwakamata watoto wa mtuhumiwa je, ilikuwa kosa lao ni nini, wakati mtoto
aliyedai kubakwa alimtaja baba mzazi wa watoto hao,’’wakili wa utetezi Abeid
Mussa Omar alimuuliza askari mpelelezi mahakamani hapo.
Aidha wakili huyo wa utetezi,
alimuuliza shahidi muuguzi, sababu ya kumchukuguuza mtoto aliyefikishwa hospitali,
wakati yeye hana cheo cha udaktari, na kujibu kuwa anayomafanzo juu ya
uchunguuzi wa wahanga wa aina hiyo.
Mara baada ya kumaliza
ushahidi wao, hakimu wa mahakama hiyo Muumini Juma Ali, aliliagharisha shauri
hilo Novemba 7, mwaka huu, huku upande wa mashataka ukifunga ushahidi wake, na
siku ambayo mahakama itatoa uamuzi juu ya kesi hiyo.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa
huyo Khamis Juma Chumu ‘soda’ (76) mkaazi wa Mtoni wilaya ya
Chake chake, alidaiwa kumtorosha mtoto wa kike miaka 13, wakati akienda kuchota
maji mferejini, na kumpeleka nyumbani kwake.
Kufanya hivyo ni kosa,
kinyume na kifungu 113 (1) (a) cha sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018,
sheria ya Zanzibar.
Kosa la pili ni la ubakaji, ambalo
anadaiwa kulifanya Mei 15, mwaka huu, ambapo anadaiwa kumbaka mtoto huyo majira
ya saa 4:15 asubuhi, eneo la Mtoni wilaya ya Chake chake.
Kufanya hivyo ni kinyume, na
kifungu 108 (1), (2) (e) na kifungu cha 109 (1) cha sheria ya Adhabu nambari 6
ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment