Skip to main content

LSF: 'CHAPO CHAPENI KAZI'

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA::

MFUKO huru wa msaada wa kisheria ‘LSF’ umeutaka uongozi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ kufanyakazi zao kwa umakini mkubwa, ili kuendeleza sifa yao ya utendaji kazi.

 

Ushauri huo umetolewa na Afisa Program Mwandamizi kutoka mfuko huo Zanzibar, Alphonce Marandu Gura, wakati akizungumza na watendaji wa ‘CHAPO’ ofisini kwao mjini Chake chake, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kujitambulisha kwa jumuia za wasaidizi wa sheria kisiwani Pemba.

 

Alisema, anayotaarifa ya uchapaji kazi wa watendaji wa CHAPO, hivyo amewakumbusha kuendelea kufanyakazi kwa uweledi na ushirikiano, ili waendelee kujijengezea saifa kwao na jamii kwa ujumla.

 

Alisema, CHAPO ni tegemeo kubwa la wananchi wa wilaya ya Chake chake, hivyo lazima waelewa thamani hiyo, na kuithamini katika kazi zao za kila siku.

 

Alieleza kuwa, kazi ya kuihudumia jamii ni nzito na inakuwa na changamoto kadhaa, na wakati mwengine bila ya kuwepo kwa ufadhili, hivyo ni wajibu wakaendelea kulijua hilo.

 

‘’Mimi kwa mujibu wa maelezo yenu na ripoti zenu, niwapongeze kwa kuendelea kuchapa kazi kubwa na ngumu ya kutoa elimu, msaada na ushauri wa kisheria kwa jamii bila ya malipo,’’alieleza.

 

Hata hivyo Afisa huyo Program Mwandamizi wa ‘LSF’ ofisi ya Zanzibar Alphonce Marandu Gura, aliihimiza ‘CHAPO’ kutuma ripoti zao kwa wakati na zilizokamilika, ili iwe rahisi kuzifanyia uchambuzi.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema ujio wa mtendaji huyo wa ‘LSF’ umewapa ari, nguvu na hamasa ya kufanyakazi zaidi.

 


Mkurugenzi huyo, alimuahidi Afisa huyo kuyafanyia kazi maelekezo na ushauri wake, na hasa eneo la kutuma ripoti kwa wakati na iliyokamilika, kwani wamekuwa wakipata mafunzo juu ya namna ya kuandika ripoti.

 

‘’Sisi kwanza tushukuru kwa ugeni huu kutoka ‘LSF’ kuja kujitambulisha kwetu, baada ya mtendaji aliyekuwepo kumaliza muda wake, na huyu mpya tutashirikiana nae kikamilifu,’’alisema.

 

Mshika mfedha wa ‘CHAPO’ Riziki Hamad Ali, alisema changmoto iliyopo kwa sasa, ni ukosefu wa mafunzo zaidi ya kujengewa uwezo, juu ya mifumo ya matumizi na ulipaji fedha kwa njia ya kisasa.

 

Afisa sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Pemba Bakar Omar Ali, aliwakumbusha watendaji wa CHAPO, kufanyiakazi kwa vitendo, kila aina ya mafunzo waliopewa.

 


Kwa upande wake Msaidizi mratibu wa ‘CHAPO’ Khadija Said Khalfan, alisema shughuli za kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria zinakwenda vizuri kwa jamii ya wilaya ya Chake chake.

 

‘’Hapa CHAPO iendelee kujengewa uwezo zaidi, ili ifike pahala iweze kujisimamia wenyewe, badala ya ilivyo sasa kutegemea wafadhili kwa kila kitu,’’alishauri.

 

Afisa Ufuatilia wa zone ya Pemba, Hamisa Bakar Hamad ameutaka uongozi wa ‘CHAPO’ kuendelea kushirikiana na mtendaji huyo wa ‘LSF’ ili kila upande ufanikishe kazi zake.

 

Alieleza kuwa, kila baada ya muda watendaji hubadilika, ingawa tasisi huwa ni ile ile, hivyo kama walivyokuwa wakifanyakazi na mtendaji wa LSF na aliyemaliza muda wake, nI vyema na kwa huyo mpya kushirikiana nae.

 

Hata hivyo ameutahadharisha uongozi wa CHAPO wasijaribu kufanya matumizi ya aina yoyote ambayo hayamo kwenye mpango kazi wao mkuu.

 




Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba, ‘CHAPO’ ambayo shughuli zake kuu ni kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria bila ya malipo, inawahudumia wananchi wa shehia 32 zilizomo kwenye majimbo ya Chake chake, Wawi, Ole, Chonga na Ziwani.

               Mwisho   

 

 

Comments