NA HAJI
NASSOR, PEMBA:
MYORORO
wa thamani katika kuinua kipato cha wajasiriamali, chachu kubwa ni uwepo
miundombinu ya uhakika wa barabara.
Ambayo huwaunganisha wajasiriamali hao na wateja wao, iwe
walioko kwenye masoko makuu au wale mmoja mmoja katika vitongoji na vijiji, au mitaa.
Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa rais Zanzibar (marehemu) Maalim
Seif Sharif Hamad, aliwahi kusema kuwa, mnyororo wa thamani huanzia kwenye
kilimo, uvunaji, soko la uhakika, ubora wa bidhaa na miundombinu ya uhakika ya
barabara.
Kilomita 35 za barabara zilijengwa kwa kiwango cha lami kwa
ufadhili wa watu wa Marakeni kupitia mradi ‘MCC’ zikijumuisha ile ya
Kipangani-Kangagani, Chwale-Kojani, Mzambarau takao-Pandani Finya na ile ya
Bahanasa- Mtambwe.
BAADA YA
UJENZI WA BARABARA HIZO
Kuanzia mwaka 2014, wanawake walichangamkia kuanzisha vikundi
vya ushirika, ili kutanua pato lao, kupitia kazi wanazozifanya.
Wakati aliyekwuwa rais wa Zanzibar wa awamu ya sita Dk. Ali
Mohamed Shein, akizifungua barabara hizo, alisema anataka kuona, kuimarika kwa
uchumi wa wananchi, kwa kuwepo barabara hizo.
Na hata aliyekuwa Kaimu balozi wa Marekani nchini Tanzania wakati
huo Virginia Blaser, alisema uwepo wa barabara hizo, iwe ni daraja la
kuwaunganisha kibiashara, wananchi walioko mjini na vijijini.
‘’Leo tunazindua barabara hizi, kwa wananchi pamoja na kuwa na
usafiri wa uhakika, lakini ziwe chachu za kukuza na kuendelea ama kuanzisha
biashara,’’anasema.
WANAHARAKATI
Siti Habibu Mohamed, anasema wanawake ndio washirika wakuu wa
kuleta maendeleo, sambamba na kukuza pato lao, ambapo uwepo wa barabara hizo za
‘MCC’ zimewasaidia.
‘’Wapo wanauchumi kadhaa wanaamini kuwa, uwepo wa barabara
kunauhusiano mkubwa na wanawake kukuza pato lake, maana pia ndio wahanga wa
changamoto za kutofikia ndoto zao,’’anasema.
Walikuwa wakiwahamasisha wanawake kujikusanya pamoja na
kuanzisha vikundi vya ujasiriamali, ikiwemo ufugaji na kilimo, ingawa walikuwa
wagumu, lakini baada ya mwaka 2014, sasa wamehamasika.
Afisa Miradi kutoka Chama cha waandishi wa habari wanawake
Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba, Asha Mussa Omar anasema, awali ilikuwa
ni changamoto kwao kuwafikia wanawake, ili kuwapa mbinu za kukuza mitaji yao.
‘’Kwa sasa, uwepo barabara hizi za ‘MCC’ kwa kiwango cha lami,
zimewapa urahisi wanawake, kutoka vijijini kwenda mjini, iwe ni kwa ajili ya
kutafuta soko au kufuatilia rasilimali,’’anasema.
Anaona, ingekuwa sio rahisi kwa wanawake, kutoka kisiwa cha
Kojani au Kangagani na Mtambwe, kuwaona kwenye maonyesho ya kitaifa, maana hapo
awali, walikuwa wakikabiliwa na changamoto za uchakavu wa barabara.
‘’Leo sisi tunajivunia, kuona hata hali za wajasiriamali
tunaowasimamia na hasa kwenye zile barabara tano, wanafursa ya kutoka na
kuingia kwa wateja wakati wowote, tofauti kabla barabara hizi kujengwa,’’anasema.
Kwa sasa anaona kuna mpishano mkubwa wa biashara, kati ya
wanawake wa kijiji kimoja na chengine, maana usafiri umeimarika, baada ya
kuwepo kwa barabara za hakika.
‘’Bidhaa kama Vanila, iliyolimwa na wajasiriamali wanawake
Mtambwe sasa imekuwa maarufu, katika masoko ya miji ya Wete na Chake chake na
nje ya Pemba, na hata usafirishaji baada ya kuwepo kwa pikipiki ni
rahisi,’’anasema.
Kwa kuimarika huko miundombinu ya barabara, sasa TAMWA
inavyovikundi 12 vya wajasiriamali wanawake, vinavyojumuisha wanachama 210
kutoka vijiji vilivyopitiwa na barabara za ‘MCC’ mkoa wa kaskazini Pemba.
WAJASIRIAMALI
Hamid Juma Mohamed, wa Uwondwe shehia ya Mtambwe mkoa wa kaskazini
Pemba, anaendesha maisha yake kupitia uwekaji na ukopaji wa fedha ‘saccos’
anasema, wamehamasika kuanzisha vikundi vya kilimo cha mboga baada ya kuwa na
usafiri wa uhakika.
‘’Sasa tunavuna mboga saa 12:00 asubuhi na saa 12:45 tumeshafika
soko la mjini Wete kwa kuuza, ingawa kabla ya ujenzi wa barabara yetu kwa
kiwango cha lami, hatukufikiria kuwa na kilimo cha aina hii,’’anasema.
Meiye Hamad Juma, anasema uwepo wa barabara ya uhakika ni eneo
kubwa la kukuza pato lao, na kinyume chake ni kudhoofisha juhudi zao.
‘’Mimi kwa sasa naweza kumtuma mwenye piki piki wakati, siku
na muda wowote kunipelekea bidhaa au kunichukulia mali ghafi, maana barabara ni
ya uhakika na sio kama zamani,’’anasema.
Salma Hassan Shaame, anaefanyabiashara za nguo kijijini hapo,
anasema uwepo wa barabara hiyo, kwa sasa imekuwa chachu ya kukuza pato lake,
kutokana na ongezeko la wateja.
‘’Wakati barabara haijajengwa, ilikuwa mauzo yangu kwa siku
hayazidi shilingi 60,000 ingawa kwa sasa huuza kati ya shilingi 100,000 hadi
shilingi 120,000,’’anasema.
Hata mkulima wa tungule na njugu kijiji cha Kangagani
wilaya ya Wete, Aisha Msabaha Himid, anaona sasa wateja wake wanamfuata
shambani, hata kipindi cha mvua, kutokana na uwepo wa barabara ya uhakika.
‘’Kabla ya kujengwa kwa barabara hizi na MCC ilikuwa, baada ya
kuvuna unaweza kuweka mazao ndani hata mwezi mmoja, ili asubiri mvua zipite na kuyasafirisha
mazao kwenda sokoni, lakini kwa sasa wakati wowote unasafirisha,’’anasema.
Kama alivyo Mwajuma Issa Haji wa Pandani, anasema kwa muda
mrefu anafuga kuku wa kienyeji, lakini alikuwa akiuza kwa bei ndogo, maana
wateja walikuwa wakimfuata.
‘’Sasa hukusanya kuku wangu kati ya 30 hadi 50 na huwaingiza
garini hadi soko la Wete, na huuza mmoja kati ya shilingi 15,000 hadi shilingi
20,000 ingawa hutegemeana na ukubwa,’’anafafanua.
Hapa anasema bei hizo hakuwahi kuzipata kwa vile uchakavu wa
barabara yao kwa Pandani kwa wakati huo, ulichangia wateja wanaomfuata kumlalia
kibei.
Kumbe hata Ashura Makame Mjaka wa Kojani, anasema bidhaa yake
ya mafuta ya nazi, unga wa karafuu na mapambo ya akinamama, amepata umaarufu na
kuongeza wateja.
‘’Ilikuwa ikfika saa 10:00 jioni popote nilipo nianze safari
ya kurudi Kojani, maana uchakavu wa barabara ulikatisha tamaa ya usafiri,
ingawa kwa sasa wakati wowote sina wasi wasi,’’anasema.
Anauza kati ya shilingi 75,000 hadi shilingi 85,000 kwa siku
katika mitaa ya Mchanga mdogo, Madenjani, Kangagani na Shengejuu jambo
linalokuza pato lake.
Mwanzilishi wa usafiri wa chombo aina ya bajaji barabara ya
Kipangani- Kangani Omar Abdalla, anasema nae amekuza pato lake, kwa
kuwasafirisha abiria kutoka Kangagni hadi njia kuu, ya kwendea miji ya Wete,
Chake chake, Micheweni na Mkoani.
‘’Kwa siku hujipatia kati ya shilingi 60,000 hadi 70,000 ingawa
hutegemeana na mwamko wa wasafiri
wenyewe, lakini kwa hakika uwepo wa barabara hii iliyojengwa na watu wa
Marekani, kwangu ni mkombozi,’’anasema.
Mfanyabiashara wa duka la chakula eneo la Mzambarau takao,
Mohamed Omar Habibu, anasema kabla ya ujenzi, wananchi wa Pandani walikuwa
wakilaza vyombo vyao vya usafiri, uwanjani kwake.
‘’Wakati mimi nasoma, lazima ilikuwa hadi wanafunzi
tujukusanye sita au saba, ili tufuatane kutokana na pori lililokuwepo, ingawa
baada ya ujenzi wa kiwango cha lami, sasa nafuu ipo,’’anasema.
Anapotaka kusafirishia bidhaa zake kutoka miji ya Konde,
Mapofu na Micheweni kuleta dukani kwake, anaitumia barabara hiyo ya Pandani
kutokana na kujengwa kwa kiwango cha lami.
SERIKALI
Afisa Mdhamini wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Pemba
Ibrahim Saleh Juma, anasema tokea kufunguliwa kwa barabara hizo miaka tisa (9)
iliyopita hawajawahi kuzifanyia matengenezo, kutokana na uimara wake.
‘’Matengenezo tuliyoyafanya ni barabara ya Bahanasa- Mtambwe
kwenye daraja, baada ya kuharibika kutokana na mvua kubwa, iliyonyesha mwaka
2017 na kwa sasa barabara zote tano, ziko madhubuti,’’anasema.
Mhandisi mkaazi mstaafu wa waujenzi wa barabara Pemba wakati
wa ujenzi wa barabara za MCC, Khamis Massoud Khamis, anasema uimara wa barabara
hizo, ulitokana na aina ya ujenzi.
Anasema ujenzi wa barabara hizo umetofautiana na nyingine,
maana tabaka mbili za juu ‘sub base and base’ zilichanganywa
kokoto nyembamba na saruji, kwa ujazo wa mita moja na kwa mfuko mmoja wa
saruji.
Aina ya ujenzi wa barabara hizo za MCC hazikutumia lami moto ‘asphalt
congreate’ bali zilitumia mfumo wa lami ya kuchemsha ‘surface
dressing’ na kisha kumwagwa, baada ya muda humiminiwa kokoto zenye
ujazo wa milimita 15 hadi 20 na kuzama kwenye lami hiyo.
‘’Baada ya kushindiliwa hadi kuzama kwa kokoto, humwagwa tena
lami zikiwa na kokoto ndogo ndogo, zenye ujazo kati ya milimita 8 hadi 10,
lengo ni kuziba nafasi ilizoachwa wazi, na kokoto kubwa za awali,’’anafafanua.
Jengine linalotofautiana kwenye ujenzi wa barabara hizo za MCC,
ni kutumia shilingi bilioni 1.1 kwa urefu wa kilomita 1, wakati ujenzi wa
barabara za kawaida kwa urefu huo, ni hugharimu shilingi bilioni 1.
‘’Ujenzi wa aina hii ya barabara za MCC hutakiwa kufanyiwa
matengenezo kila baada ya miaka 10, ingawa kwa kwetu zinaweza kuzidi kutokana
na kutokuwepo kwa gari nyingi zenye uzito wa zaidi tani 15, kama uhimili wa
barabara zinavyotakiwa,’’anasema.
Hata hivyo Afisa Mdhamini wa sasa wa barabara Ibrahim Saleh
Juma anasema, wamekuwa wakiziangalia kila muda barabara hizo, na hawatosita
kuzifanyia matengenezo yatakapohitajika.
Mwisho
Comments
Post a Comment