NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ AFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar afisi ya Pemba, imewahakikishia wananchi wa shehia ya Chonga wilaya ya Chake chake, kuwa kama wako tayari kushirikiana na vyombo vya sheria, shehia yao itakuwa salama na vitendo vya kihalifu. Hayo yameelezwa leo Septemba 6, 2024 na Mwendesha Mashtaka Dhamana wa mkoa wa kusini Pemba, kutoka afisi hiyo, Seif Mohamed Khamis, wakati akijibu hoja za wananchi hao, waliooneshwa kushindwa na vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na watoto wao, kwenye mkutano wa kuwajengea uwezo wananchi hao. Alisema, kama kweli wananchi hao wameshakua tayari kuviondoa vitendo vya kihalifu kama wizi, utumiaji wa dawa za kulevya, wajitayarishe kuona mabadiliko muda mfupi ujao. Alieleza kuwa, atahakikisha ofisi yake, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na kitengo cha dawa za kulevya, wataunda timu ambayo wanawategemea wazazi na walezi, ili kuiweka Kipapo salama. Alisema, hata wao watafurahishwa mno, ikiwa wazazi sasa wako tayari...