NA HAJI NASSOR, PEMBA
JAMII imeshauriwa kubuni kila mbinu na mikakati endelevu, ili
kuhakikisha kundi la watu wenye ulemavu linapata haki zao zote za msingi,
ikiwemo matunzo.
Akizungumza na mwanadishi wa habari hizi, Wete Mkoa wa kaskazini
Pemba, Mshauri kutoka Shirika la watu wenye ulemavu la Norway (NAD) Christine
Cornick alisema, bado jamii haijawapa umuhimu watu wa kundi hilo.
Alisema, watu wenye ulemavu wamekuwa wakidharauliwa, kugawanya,
kutengwa na kudhalilishwa, kutokana na mazingira yao, jambo haliingii akili.
Alisema kuwa, ushirikiano wa pamoja ndio utakaoleta nguvu ya
kufanya kazi na kuleta mabadiliko ya haraka katika ukondoishaji wa masuala ya
watu wenye ulemavu katika nchi mbali mbali.
"Katika mtandao huu tumeshirikisha watu mbali mbali,
wanakuwa na sehemu ama mahala ambapo wanakutana na kubadilishana uzoefu katika
ngazi mbali mbali na kutoa maamuzi ya kujenga jamii iliyobora", alisema.
Alifahamisha kuwa, watu wenye ulemavu wamekuwa wakikosa huduma
zao za msingi, jambo ambalo linasababisha kudharaulika na kudhalilika, hivyo ni
wajibu wa jamii kulifikiria hilo.
Mapema Mkurugenzi wa Baraza la watu wenye ulemavu Zanzibar Ussi
Khamis Debe alisema kuwa, Serikali ipo pamoja na watu wenye ulemavu kutumia
mtandao mbali mbali, katika kuhakikisha wanafikisha changamoto zinazowakabili
sehemu husika, ili ziweze kupatiwa ufumbuzi unaofaa.
"Tunaamini kwamba lengo la taasisi ya malezi na makuzi Bora
ya watoto (MECP-Z) ina lengo la kutusaidia na kupata haki zetu sawa na watu
wengine, hivyo tushirikiane kwa pamoja ili kufanikisha", alisema
Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo wa uharakishaji haki za
watu wenye ulemavu, Saida Amour alieleza kuwa, watu wenye ulemavu wanakosa
usaidizi katika sehemu za kutoa huduma, wanalipishwa nauli mara tatu wakati
wanapokwenda safari na pia kuna ushirikishwaji mdogo katika masuala ya michezo.
"Hizi ni changamoto kubwa zinazowakabili watu wenye ulemavu
ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi na kuondoshwa kabisa ili wajisikie huru ndani
ya jamii", alieleza Mratibu huyo.
Nae muwakilishi kutoka Shirikishao la Jumuiya za watu wenye
ulemavu Zanzibar ‘SHIJUWAZA’ Ali Khamis Machano alisema kuwa, watu wenye
ulemavu wamekosa elimu ya watu wazima pamoja na ya utunzaji wa fedha, jambo
ambalo linasababisha kutoendeleza biashara zao.
"Watu wenye ulemavu unawakuta mara nyingi miradi yao inakwama
na hawaendelei mbele, jambo hili linawakwaza, hivyo kuna haja ya kupewa elimu
ya utunzaji wa fedha", alifafanua.
Mjasiriamali wa mboga mboga katika eneo la Wawi wilaya ya Chake
chake, mwenye ulemavu wa akili, Himid Juma Khamis, alisema hata bidhaa zao wapo
wanaocha kuzinunua kwa tafsiri zao potofu.
Mfanyabiashara wa viungo vya mchuzi katika soko la Wete mwenye
ulemavu wa viungo, Maua Ali Mkonde, alisema hata mamlaka za serikali, wakati
mwengine huwasababisha maumivu ya kazi zao.
Sheria ya haki na fursa kwa watu wenye ulemavu nambari 9 ya
mwaka 2006 ya Zanzibar, kifungu cha 43, kimekataza kwa mtu yeyote kumfanyia
dharau au kejeli mtu mwenye ulemavu.
MWISHO.
Comments
Post a Comment