Na Salma Lusangi, ZANZIBAR
Wizara ya Maji, Nishati na Madini (WMNM) Zanzibar, imekusanya jumla
ya shilingi bilioni 2.97 katika kipindi
cha miezi mitatu iliyopita ikiwa ni mauzo ya mchanga na vibali kutokana na
utaratibu mzuri wa usimamizi pamoja
kuimarika kwa mfumo wa kielektroniki wa maombi ya vibali vya Maliasili Zisizorejesheka (Madini Management System).
Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Waziri, WMNM Shabaan Ali Othman katika kikao cha utekelezaji
wa programu za Wizara kwa kipindi cha Julai –Septemba, 2022 katika kikao cha
pamoja na kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar
kilichofanyika jana katika ukumbi wa ZURA Maisara, Unguja.
Alisema usimamizi mzuri pamoja na kuimarika kwa mfumo wa
kieletroniki wa maombi ya vibali vya Maliasili Zisizorejesheka umesaidia udhibiti wa mchanga
ambapo Sekta ya Madini imekusanya shilingi 2.97 bilioni sawa na asilimia 120 ya
makadirio ya kukusanyo 2.46 bilioni.
Pia alisema Idara ya Nishati na Madini imeimarisha kikosi cha doria
kwa dhamira ya kudhibiti uchimbaji holela wa mchanga hivyo Idara hiyo imenunua
gari tatu ambazo zitatumika katika doria kwa maeneo mbali mbali ya Unguja.
Alisema kikosi cha doria pia
kilipatiwa mafunzo ya ukaguzi wa vibali na leseni pamoja na kuwapatiwa vifaa vya mawasiliano
ili kurahisisha mawasiliano baina yao kwa ajili ya kuleta ufanisi katika
kudhibiti maliasili hizo.
Aidha alisema Idara ya Nishati na Madini ilitumia shilingi milioni
100 kuwalipa fidia wananchi 23 ambao mazao yao yalithirika kutokana na shughuli ya uchimbaji Maliasili Zisizorejesheka
katika maeneo yao.
“Mheshimiwa Mwenyekiti Wizara ilipangiwa kukusanya shilingi 2.46 bilioni kutoka katika vyanzo
vya mapato yatokanayo na mauzo ya mchanga na vibali hadi kufikia 30 Septemba,
2022 Wizara imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 2.97 bilioni sawa na asilimia
120 ya makadirio,” Alisema Othman.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Yahya Rashid Abdulla aliiagiza
Wizara kukutana na Mkuu wa Wilaya na
vijana wanaouza mchanga eneo la TAVETA, ili kutafuta namna ya kudhibiti
biashara hiyo katika eneo hilo.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Nishati na
Madini Mhandisi Said Haji Mdungi alisema
watalifanyia kazi agizo hilo
lilitolewa na kamati hiyo, kwaajili ya
kupata maoni mbali mbali ingawa Idara ya Nishati na Madini inatumia Sheria Na 3
ya mwaka 2015, Sheria ya Mazingira ya
Zanzibar ambayo inamruhusu mtu kusafirisha Maliasili Zisizorejesheka na sio
kuuza.
Mwisho
Comments
Post a Comment