NA HAJI NASSOR, PEMBA WANANCHI kisiwani Pemba, wametakiwa kuendelea kuchukua hatua za kuchunguuza afya zao mara kwa mara, ili wajielewa ikiwa wanaishi na vimelea ambavyo vinaweza kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu ‘TB’. Ushauri huo umetolewa na m taalamu kutoka kitengo shirikishi cha maradhi ya ukoma, kifua kikuu na Ukimwi Zanzibar, Said Khamis Ahmada, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi. Alisema, moja ya njia ya kujikinga ama kuwahi matibabu ya ugonjwa huo, ni kuwa na tabia ya kuchunguuza afya mara kwa mara, ii upatikane ufumbuzi kwa wataalamu wa afya. Alieleza kuwa ugonjwa wa kifua kikuu kitaalamu unaoitwa (‘ Tuberculosis’ TB) ni miongoni mwa magonjwa 10 yanayosababisha vifo kwa wingi duniani kote. Alifahamisha kuwa tafiti zilizofanywa na Shirika la Afya Ulimwenguni ‘WHO’ zinaonesha kuwa, inakisiwa watu milioni 10 wameugua ugonjwa huo, duniani kote, na hadi mwaka 2020, na kati ya hao watu milioni 1.5 wamefariki dunia. ...