Skip to main content

JUMUIYA ZA WATU WENYE ULEMAVU PEMBA ZATOA NENO UAMUZI WA RAIS

 

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA::

JUMUIYA za watu wenye ulamavu kisiwani Pemba, wamepongeza hatua ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuvikodisha, visiwa vinane vidogo vidogo, kwa dola za Marekani milioni 271.5 wastani wa shilingi bilioni 600.357.

 

Wakizungumza na mwandishi wa habari kwa nyakati tofauti juu ya hatua ya serikali kuvikodisha visiwa hivyo, walisema bila shaka nia ya serikali ni kuongeza mapato ya nchi.

 

Mjumbe wa kamati tendaji wa Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar JUWAUZA Hidaya Mjaka Ali, alisema wazo hilo ni zuri, kwani linaelekea kwenye maslahi bora ya taifa.

 

Alisema, bila shaka katika hatua hiyo, kila mmoja kwa nafasi yake na alipo yatamfikia matunda ya ukodishwaji huo, ambapo ni hatua moja yapo ya kufikia maendeleo ya kweli.

 

‘’Mimi kwa niaba ya JUWAUZA, lazima hili lililoamuliwa na kiongozi wa nchi nilipo ngeze, maana bila shaka linamanufaa kwetu wananchi na taifa kwa ujumla,’’alisema.

 

Hata hivyo, ameziomba mamlaka husika wasiwaache kila hatua wetu wenye ulemavu, kwani wana haki sawa kama yalivyomakundi mengine.

 

Mwakilishi wa vijana wenye ulemavu katika baraza la taifa la Vijana Zanzibar Katija Hamad, alisema hatua hiyo inaonesha, nia ya dhati ya serikali, ya kutaka kuwainua wananchi kiuchumi, jambo ambalo ni vyema nao, wakaangaliwa kunufaika na uwekezaji huo.

 

Alieleza kuwa, hatua hiyo ya serikali inayoongozwa na Dk. Mwinyi, wameifurahia mno, na sasa kilichobakia kwa watendaji sekta ya utalii, kuweka mazingira rafik kwa ajili yao.

 


Mwenyekiti wa Jumuiya ya wasioona Pemba ZANAB Suleiman Mansour, alisema uwekezaji huo ikiwa watashirikishwa kikamilifu, unaweza kuwa na maana pana kwao, ikiwa ni pamoja na ajira za kudumu.

 

“Sisi watu wenye ulemavu, mara zote tumekuwa tukisahauliwa kushirikishwa katika utekelezaji wa sera mbali mbali, na kisha hukumbana na changamoto kama za miundombinu rafiki,’’alieleza.

 

Nae Msaidizi Katibu wa Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar ‘JUWAUZA’ Bimkubwa Mohamed Ali, alisema watu wenye ulemavu na hasa wanawake, wamekuwa wakiandamwa na changamoto, ambazo zinaweza kuzuilika kabla.

 

“Hatua ya Dk. Mwinyi mpaka kuwashawishi wawekezaji na kuonesha nia ya uwekezaji ni nzuri, lakini lazima sera ziwalazimishe wawekezaji, kutushirikisha na sisi watu wenye ulemavu,’’alishauri.

 

Mkurugenzi wa Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar mwalimu Ussi Khamis, alisema bado sheria nambari 9 ya mwaka 2006 ya watu wenye ulemavu Zanzibar, haitekelezwi hasa kipengele cha uajira kwa kundi la watu wenye ulemavu.

 ‘’Kuanzia vifungu vya 6 hadi cha 8 vya sheria hii, inafafanua suala la ajira kwa watu wenye ulemavu, sasa kama haki au fursa katika ajira za kitaifa watu wenye ulemavu, wasiaachwe nyuma,’’aliependekeza.

 

Mdhamini Kamisheni ya Utalii Pemba Hamad Amin, amesema watu wenye ulemavu, wana haki sawa na wengine, na niwakati nao kujipanga, ili kunufaika na uwekezaji huo.

 


Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud, alisema lazima katika ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni, zifikiria mazingira kwa watu wenye ulemavu.

 

Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar ‘ZIPA’ Sharif Ali Sharif, alivitaja visiwa hivyo vinane kuwa ni Changuu, kinachoekezwa kwa dola zisizopungua milioni 20 kupitia kampuni ‘Changuu Lodge Ltd’.

 

Kisiwa cha Bawa kitaekezwa na kampuni ‘Bawe Retreat Ltd’ kwa mtaji wa dola milioni 30, ambapo kisiwa cha Chapwani kitaekezwa na kampuni ya ‘Zan Texas Ltd’ kwa dola milioni 20 na kisiwa cha Snake dola milioni 10, kupitia kampuni hiyo.

 

Aidha Mkurugenzi huyo, alikitaja kisiwa cha Kwale kikiwa na uwekezaji kupitia kampuni ‘Group Eight Holding Ltd’ sawa na mtaji wa dola milioni 68.

 

Kisiwa cha Misali Pemba, kitaekezwa na kampuni ‘East African Investment Ltd’ kwa mtaji wa dola za Marekani milioni 83, wakati visiwa Pamunda ‘A’ na ‘B’ vimechukuliwa na kampuni ya ‘Tulia Zanzibar Beach Resort’ kila kimoja kwa dola milioni 15.

“Kisiwa chengine ni Pungume Unguja kilichopewa mwekezaji kupitia kampuni iitwayo ‘Emperial East African Ltd’ kikiwekezwa kwa dola milioni 10.5,’’alieleza Mkurugenzi huyo.

 

Rais wa Zanzbar Dk. Hussein Ali Mwinyi, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, kuwa katika kipindi cha mwezi Novemba mwaka 2020 hadi Disemba 2021, ZIPA imesajili miradi 120 ya uwekezaji, yenye mtaji wa dola za Marekani milioni 877.

 

Miradi hiyo inatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 7000, na tayari wawekezaji wameshajitokeza katika visiwa vidogo vidogo 10, vilivyotangaazwa kukodishwa.

  

                  MWISHO

 

Comments