NA HAJI NASSOR, PEMBA: “KESI ya mtoto wangu mwenye ulemavu wa matamshi, ilifutwa mwaka 2021 mahakamani, kwa sababu ya siuntafahamu ya eneo alilobakwa ni tofauti na walilolitaja mashahidi,’’anasema mama wa mtoto huyo. Mama huyo mkaazi wa Pujini Dodo wilaya ya Mkoani, anasema tokea asili mtoto wake anaulemavu wa akili na matamshi, sasa kasoro ya kumbu kumbu yake ndio chanzo cha kukosa haki zake. Anasema bado watu wenye ulemavu, mara baada ya kubakwa imekuwa ni shida mpya kuvifikia vyombo vya sheria, kutokana na ulemavu wao wakati mwengine sheria kuwa na kasoro kwao. Baada ya mtoto wake kubakwa na mtuhumiwa Abdalla Khatib Abdalla miaka 25, mwanzoni mwa mwaka 2018, kesi hiyo ilichukua tena miezi minane, hadi kufika mahakamani. “Nilipofika kituo cha Polisi Chake chake, kwanza sikupata ushirikiano, na walionipokea wakaniambia kesi yangu inaweza kuwa ngumu mahakani, kwa sababu hakuna mkalimani,’’anasimulia. Anasema ingawa a...