NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@ NAIBU Katibu Mkuu wa Utumishi na Utawala bora Zanzibar Omar Haji Gora, amesema kupandishwa kwa mshahara kwa watumishi wa Umma katika serikali ya awamu ya nane ni miongoni mwa juhudi za serikali za kuwaandalia mustakbali mzuri wa maisha watumishi baada ya kustaafu. Alisema hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya maandalizi ya kustaafu kwa wastaafu watarajiwa watakaolipwa mafao yao ya kustaafu kazi na mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar ZSSF, yaliofanyika katika ukumbi wa Kiwanja cha kufurahishia watoto Tibirinzi Chake chake Pemba. Alisema katika kuhakikisha watumishi wa umma wanakua na mustakbali nzuri wa maisha yao baada ya kustaafu serikali imechukua juhudi kadhaa ikiwa ni pamoja na kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wa serikali, kupandisha pensheni, pamoja na kutoa mafunzo ya maandalizi kwa wastaafu ili kuweza kupata uelewa wa namna bora ya kujiandalia mazingira ya kuyakabili maisha baada ya kustaafu. ...