NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ WANANCHI wa Halmashauri ya wilaya ya Micheweni Pemba, wametakiwa kurejea utamaduni wao wa kuweka mazingira yao safi na salama, ili kujikinga na magonjwa ya kuharisha, ambayo chanzo chake kikuu ni uchafu. Ushauri huo umetolewa jana na Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Rukia Khamis Haji, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii, kufuatia uwepo wa tishio la matumbo ya kuharisha, katika baadhi ya maeneo kisiwani Pemba. Alisema, suala la usafi haipendezi kuona wananchi wanalifanya kwa shindikizo la Halmshauri, bali wenyewe waamue kujielekeza kwenye usafi, ili kujihakikisha usalama wao. Alieleza kuwa, utamaduni wa kuweka mazingira safi na salama, ni vyema kwa wananchi wa Halmashauri hiyo, ikawa ndio utamaduni wao endelevu, kwani kinyume chake ni kujiangamiza. ‘’Hichi ni kipindi cha mvua na kinakuwa na changamoto zake, ikiwemo kusambaa kwa uchafu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hivyo suala la usafi lazima liwe kipaumbele chetu,’’alieleza. ...