NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ ‘’BILA ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi’’. ‘’Tena pia mtu huyo ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati, na raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio ya nchini na duniani kote, ambayo ni muhimi kwa maisha yake’’. Ndivyo Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inavyoelekeza kifungu cha 18, juu ya upatikanaji na utoaji wa habari kwa raia, tena bila ya kujali mipaka ya nchi. Mwanasheria wa kujitegemea Khalfan Amour Mohamed, anasema suala la kupata habari, au kutoa ni haki ya kikatiba, ambayo inatofautiana na haki nyingine. ‘’Ukitaka kuzigawa haki hizi, basi zipo haki za kikatiba na haki nyingine zilizotengenezewa sheria yake mbali mbali, mfano haki ya elimu,’’anafafanua. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwajali wananchi wake, haikuishia tu ndani ya Kati...