NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
JUMLA ya watahiniwa 95,955 kutoka shule za sekondari 841 na vituo vya kujitegemea 250 wanatarajia kuanza mitihani yao ya kumaliza kidato ya sita leo Tanzania bara na Zanzibar.
Hayo yameelezwa leo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde wakati akizungumza na waandishi wa Habari na kueleza kuwa pia watahiniwa 9,670 kutoka vyuo 70 wamesajiliwa kufanya mitihani ya mwisho ya mafunzo ya ualimu katika ngazi ya stashahada na cheti.
Dk. Msonde alisema kati ya watahiniwa wa kidato cha sita, 85,531 ni waliopo skuli na 10,424 ni wa kujitegemea.
“Kati ya hao wanaume ni 47,859 ni sawa na asilimia 55.96 na wasichana ni 37,672 sawa na asilimia 44.04. Pia wapo watahiniwa wenye mahitaji maalumu 151, kati yao 136 ni wenye uoni hafifu na 15 ni wasioona kabisa,” alisema Dk. Msonde.
Alifafanua kwamba kati ya watahiniwa wa kujitegemea 10,424 waliojisajili, wanaume ni 6,546 sawa na asilimia 62.80 na wanawake ni 3,878 sawa ana silimia 37.20 na asiyeona ni mmoja.
Katibu huyo alieleza kuwa kati ya walimu watakaoketi kufanya mtihani ya ualimu, 4,560 ni wa ngazi ta stashahada na 5,110 ni ngazi cheti.
Aidha Dk. Msonde amesema baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litajiridhisha kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa mitihani ya taifa na kuwasihi watahiniwa wote kuzingatia kanuni na sheria za mitihani.
'CHANZO ZANZIBAR LEO'
Comments
Post a Comment