NA HAJI NASSOR, PEMBA
JESHI la Polisi mkoa wa kaskazini
Pemba, limekiri kumpa dhamana ya kipolisi daktari wa kituo cha afya Gombani
Is-haka Rashid Hadid, ambae ni anatuhumiwa kwa kumtorosha na kisha kumbaka mgonjwa
wake, ambae ni mtoto.
Kamanda wa
Polisi mkoani humo, Juma Sadi Khamis, wakati akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya
habari, alisema sababu za kumpa dhamana, ni kufuatia mtoto huyo kutaja watu
wawili tofauti.
Alisema, mtoto
huyo alimtaja daktari huyo na mtu mwengine ambae kwa sasa, wanaendelea
kumtafuta, hivyo wameona wampe dhama mtuhumiwa huyo hadi wote wawili
watakapopatikana.
Alieleza
kuwa, mtoto huyo alimtaja daktari kwa sababu alikwenda kupata huduma, ingawa
yuko mtu mwengine aliyemfanyia kitendo hicho.
‘’Kwa sasa
baada ya kuona mtoto huyo anafanya ubabaifu, daktari ambae tulikuwa
tunamshikilia tumeshampa dhamana kwa muda,’’alifafanua Kamanda huyo.
Aidha Kamanda
huyo, alieleza kuwa kwa sasa suala hilo linaendelea kupelelezwa kwa kina, na
kisha Jeshi hilo litatoa taarifa nyingine rasmi.
‘’Ni kweli
yule daktari ambae tulikuwa tunamshikilia, kwa sasa tumeshampa dhamana, maana
muathirika aliwataja watuhumiwa wawili tofauti akiwemo daktari,’’alieleza.
Wakati hayo
yakifanyika, Chama cha waandishi wa habari wanawake wanawake Tanzania -TAMWA-Zanzibar
ofisi ya Pemba, kimeshtushwa na taarifa ya Jeshi la Polisi, kumpa dhamana
mtuhumiwa huyo.
TAMWA
kimesema, kama muathirika ameshamtaja mmoja kati ya watuhumiwa wawili, haingii
akili, kumpa dhama mtuhumiwa nambari moja, kwa madai ya kumtafuta mwengine.
‘’Kama
mtuhumiwa mmoja ameshapatikana, ni vyema sasa hatua nyingine zikaendelea,
lakini unapompa dhamana ni kuivizisha kesi hiyo,’’alisema Mratibu wa TAMWA
Fat-hiya Mussa Said.
Aidha
Mratibu huyo alisema, kama kesi za udhalilishaji zimetajwa na sheria hazina
dhamana, iwe kwa watuhumiwa wote, na sio kwa baadhi yao.
Kwa upande
wake Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Kangagani wilaya ya Wete, Awena
Salim Kombo, alisema ameshangaazwa na hatua ya Jeshi la Polisi, la kumpa dhama
mtuhumiwa huyo.
Alisema,
kila siku rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi, amekuwa akisisitiza, juu ya kutotoa dhamana kwa kesi hizo, ingawa
utekelezaji haupo.
Afisa Ustawi
wa Jamii wilaya ya Wete Haroub Suleimna Hemed, alisema kwa familia anayotoka
mtuhumiwa ‘daktari’ ni kubwa, na ndio maana, kesi hiyo inakwenda ndivyo sivyo.
Alisema,
analishangaa Jeshi la Polisi mkoani humo, kumpa dhamana mtuhumiwa, huku akihoji
sheria ipi waliyoitumia kumtoa daktari huyo, wakati watuhumiwa wengine huikosa
haki hiyo.
‘’Watuhumiwa
wengine wakitajwa tu na mtoto, basi huwa sheria inafanyakazi, lakini kwa huyu
ambae ametajwa, sasa nashangaa kusikia yuko nje kwa dhamana,’’alieleza.
‘’Sasa sisi
wanaharakati na tunaotetea haki za watoto tutashindwa kutekeleza wajibu wetu,
maana tunagongana kiutendaji, wengine hawapewi dhamana na wengine
wanapewa,’’alilalamika.
Kuanzia
Mei 1, mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, lililazimika
kumshikilia daktari wa kituo cha Afya Gombani Chake Chake, Is-haka Rashid Hadid, kwa tuhuma za kumbaka
mgonjwa wake.
Kisha baina ya Mei 5 na Mei 6 mwaka
huu, mtuhumiwa alipata dhamana, kwa madai ya mtoto huyo, kutaja watu wawili
tofauti.
Ambapo Kamanda wa Polisi, alisema
walilazimika kumpa dhamana daktari huyo, hadi hapo atakapopatikana mtuhumiwa
mwengine, huku akisisitiza kwa waandishi habari hiyo, isiripotiwe.
Awali mtoto huyo aliyefanyiwa
kitendo hicho alisema kuwa, Aprili 21 mwaka huu, alikwenda kituo cha afya
Gombani, kwa ajili ya matibabu, na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo,
alimuomba nambari yake ya simu.
Alisema ilipofika usiku, walikuwa
wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms), kwa lengo la kwenda kuchukua dawa
nyingine ambazo kwa mchana huo, alizikosa hospitalini hapo.
"Nilikwenda hospitali
kutibiwa, baada ya kufanya mapele sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka
aje daktari mwengine, kwa hiyo kesho (siku ya pili yake), atakuja kunichukua,
ili ukanipe dawa nyingine", alisema mtoto.
Alieleza kuwa, kisha alimchukua
hadi kijiji cha Kangagani wilaya ya Wete, na kumfungia kwa siku tano, na kabla
ya kumbaka alimchunguza virusi vya Ukimwi.
Tukio linalofafana na hilo, liliwahi kutokea Novemba 21, mwaka 2019,
hospitali ya Chake chake, baada ya daktari wa kitengo cha Atrasaund, kudaiwa
kuomba rushwa ya ngono kwa mjamzito, kama sharti la kumpa huduma.
Aidha Disemba 18, mwaka mwaka 2019, TBC 1, iliripoti Afisa Muuguzi
msaidizi wa kituo cha Afya Mamba mkoani Katavi kushikiliwa na Jeshi la Polisi,
kwa tuhuma za kumbaka mjamzito, wakati alipokuwa akimsaidia kujifungua.
Mwisho
Comments
Post a Comment