Skip to main content

CHAMA CHA MADEREVA KUSINI PEMBA CHANG'AKA NAULI MPYA YA DALADALA

 



NA HANIFA SALIM, PEMBA

CHAMA cha Wamiliki wa gari za abiria na mizigo Mkoa wa Kusini Pemba ‘PESTA’ kimesema hakitambui uwepo wa nauli mpya wa gari za abiria, katika Mkoa huo kama wanavyofanya baadhi ya madereva na makondakta.

Kimesema, kwa sasa madereva wanapaswa kuendelea kuwatoza abiria wao nauli kongwe, na sio mpya kama ambavyo wanafanya baadhi yao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, Katibu wa chama hicho Pemba, Hafidh Mbarka Salim amesema, hana taarifa ya kuwepo kwa nauli mpya, kwa gari za abiria.

Alieleza kuwa, anachofahamu ni kuwa tayari ‘PESTA’ imeshapeleka maombi ya mchanganuo wa nauli mpya, kufuatia wamiliki wa gari hizo kukumbwa na changamoto kadhaa, ikiwemo kupanda bei ya mafuta.

‘’Kwa sasa hakuna mmiliki wa gari wala dereva, aliyeruhusiwa kupandisha nauli mpya, na badala yake zitumike nauli kongwe hadi pale tangazo litakapotolewa,’’ alisema.

Hafidh alifafanua kuwa, katika muongozo huo wa maombi walioutuma serikalini, pamoja na upandaji wa bei ya mafuta lakini, kuna ongezeko la kodi pampoja na gharama za bima.

Hivyo amewataka madereva na wamiliki wa gari za abiria kuendelea kuvuta subira, na waendelee kutumia nauli kongwe wanapokua kazini.

Mapema Afisa Mdhamini wizara ya ujenzi, mawasiliano na uchukuzi Pemba, Ibrahim Saleh Juma, amekiri kupokea maombi ya ongezeko la nauli mpya kutoka ‘PESTA’.

Alieleza kuwa, tayari vikao vimeanza kukaliwa kwa ajili ya kujadili uwezekano wa kupandisha nauli mpya, kufuatia nishati ya mafuta, kodi na bima kupanda.

‘’Madereva na wamiliki wa gari za abiria, waendelee kuwa watulivu wakati wowote Serikali itatoa tamko, kuhusiana na nauli mpya,’’ alisema.

Katika siku za hivi karibuni, kufuatia kupanda kwa bei za mafuta wapo baadhi ya abiria wamekua wakilalamikia ongezeko la nauli, kabla ya serikali kutangaza bei mpya.

Mmoja kati ya abiria hao Khadija Omar Muhene wa Chake chake alisema, alitozwa shilingi 2,000 badala ya shilingi 1700 ya kutoka Chake chake hadi Mkoani.

Nae Suleiman Abdi alisema kuwa, alitozwa nauli ya shilingi 500 badala ya shilingi 400, kutoka Chake chake mjini hadi Machomane.

‘’Nauli ninayofahamu mimi kutoka mjini Chake chake hadi Wawi ni shilingi 400, lakini juzi tu nilipopanda gari ya Vitongoji nilipishwa shilingi 500 kwa madai ya nauli mpya,’’alisema.

Abiria Omar Abdull-kadir Ali alisema hata eneo la Limbani Wete sasa imepanda kwa shilingi 100 na kuwa shilingi 500 badala ya shilingi 400 ya asili.

Nao baadhi ya madereva wamesema kuwa wamelazimika kupandisha nauli kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta kwa zaidi ya miezi miwili.

Dereva Haji Abdalla Omar anaefanyakazi barabara ya Chake chake Mkoani, alisema ni zaidi ya miezi mitatu sasa mafuta na gharama nyingine za gari zimepanda pasi na nauli kupandishwa.

Nae Hassan Suod alisema, kama mafuta yamepanda bei kwa haraka, hakuna sababu kwa nauli kuchelewa kupandishwa.

Kwa mara ya mwisho serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipandisha nauli mpya za gari za abiria wakati wa awamu ya saba baina ya mwaka 2017 na mwaka 2018.

                                         MWISHO.

 

Comments