NA TATU MAKAME. ZANZIBAR@@@
UNAPOZUNGUMZIA ujasiri na ucheshi alionao mwanamke utagundua kuwa ni kiungo muhimu katika jamii hasa kwenye nafasi za uongozi.
Aidha wanawake wenye uthubutu wa kufanya harakati za jamii wamekuwa na uwezo mkubwa wa kushawishi jamii kufanya harakati za maisha ili kuendeleza maisha yao katika jamii.
Hata hivyo serikali na taasisi binafsi nazo zimekuwa mfano mkubwa kuwahamasisha wananwake kuingia kwenye nafasi za uongozi baada ya kuwapatia mafunzo ya kuwania nafasi za uongozi ili kuachana na mfumo dume wa kuwa mwanamke uwezo wake mdogo kuwa kiongozi.
Hata hivyo Mradi wa SWIL unaoimarisha uongozi wa wanawake unaoendeshwa na Chama cha waandishi wa habari Tanzania Tamwa ZNZ nao umekuwa mfano bora wa kuwahamasisha wanawake kuingia kwenye nafasi za uongozi na kuwa kioo kwa jamii.
Kwa mujibu wa Mkufunzi kutoka Chuo kikuu cha taifa cha Zanzibar (SUZA) Imane Duwe alisema kiongozi sio lazima awe mwanasiasa au mtu maarufu kama wengine.
Hata hivyo alisema wanawake wanaoingia katika nafasi za uongozi wanakuwa na mchango mkubwa kwa jamii inayowazunguuka.
Kwa upande wake Ofisa Program na mawasiliano kutoka Chama cha Waandishi wa habari Tanzania Tamwa ZNZ Nairat Ali Haji alisema wataendelea kuhamasisha wanawake kuingia katika nafasi za uongozi ili kutambua mchango wao katika jamii.
Hata hivyo alisema mradi huo pia unaangazia takwimu za wanawake ambao wanajiunga katika nafasi uongozi kuona wanawake wanakuwa katika ngazi za maamuzi.
Mwandishi wa makala haya alifanya mazungumzo na Njuma Ali Juma ambae amekuwa na utayari na uthubutu wa kuwa kiongozi mwanamke anaepigania na kupambania nafasi ya uongozi hasa jamii inayomzunguuka na watoto pamoja na watu wenye ulemavu.
Njuma alisema hawezi kuwa nyuma kama walivyo wanawake wengine hasa katika kushirikiana na serikali katika kufanya mazoezi ya viungo kwa watoto wenye ulemavu wa viungo.
Alisema alifanya kazi hiyo kwa kuwa imo kwenye damu yake ili kusaidia watu wenye ulemavu mchanganyiko ili wapate huduma kama watu wengine.
Alisema anachukizwa na watu wenye tabia ya kuwatelekeza watu wenye ulemavu na ndio akaamua kuwa nao karibu ili kuwasaidia kupata huduma.
Alifafanua kuwa moja ya kazi aliyoifanya kuwahamasisha wanawake kuhakikisha kila mtoto mwenye ulemavu anapatiwa huduma za matibabu ya viungo.
“Nililazimika kutumia usafiri wa Pikipiki kwenda vijijini kufuatilia na kuwapatia huduma za matibabu watoto wenye ulemavu wa viungo”, alisema.
Alisema pia serikali ilimpatia mafunzo maalum kuendelea na kazi yake ili kufanya kazi kwa weledi.
SAFARI YA KUANZISHA SACCOS
Njuma mbali ya kazi hiyo ambao aliajiriwa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar pia alianzisha SACCOS mnamo mwaka 2005 baada ya kupata mafunzo ya jinsi ya kuanzisha Saccos kupitia mafunzo maalum ambayo alisomea kwa muda mfupi
“Mimi nilikuwa na wezangu wasiopungua 20 ambao tulipatiwa mafunzo ya kuanzisha vikundi vya saccos na mimi kama kawaida yangu nikianzisha jambo sipendi livie nitafuatilia hadi nijue mwisho wake”, alisema.
Alisema alianzisha Meli nne Saccos akiwa na wanachama 150 wanawake 127 na wanaume 23.
Hata hivyo Njuma alisema Saccos hiyo inaendelea hadi sasa na inawanachama 3000.
“Ingawa nilidharauliwa na watu lakini sikuvunjika moyo niliendela nayo hadi sasa nashkuru kati ya watu 20 niliyenzisha Saccos na kuendelea ni mimi na pia natolewa mfano hadi sasa”, alisema.
WATU WA KARIBU WALIOMPA MOYO NJUMA
Watu walionipa moyo nipamoja na Marehemu Abdalla Mwinyi,Ayoub Mohamed Mahmoud,Shamsi Vuai Nahodha na wengine.
Hata hivyo alisema pia amekuwa na mashirikiano ya karibu na serikali kwa kuanzisha jambo hilo na pia serikali ilimuunga mkono ili kuendesha vyema saccos hiyo.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaniamini maana ilinipatia eneo kwa muda wa miaka mitatu kama mkataka lakini niliendesha vizuri saccos na pia kuongwezwa eneo jengine la kuendesha saccos”, alisema.
Alisema kwa sasa saccos hiyo imekuwa ya mfano na saccos ina kumbi nne za kufanyia mikutano na shuhuli za kijamii kama harusi.
Alisema nia ya kuendesha saccos ni kuwakomboa wanachama na hali ya umaskini ili kujiunga na saccos na kuacha kuingia kwenye mikopo ya riba.
SAFARI YA UJASRIAMALI.
Njuma alisema licha ya kuwa alikuwa mfanya kazi wa serikali lakini pia ni mjasria mali ambae anatengeneza vyungu na,mikungu na vyetezo na kueleza kuwa safari yake hiyo tayari amewafundisha zaidi ya wanawake 200 ambao walipata ujuzi kupitia ufinyazi wa vyungu.
“Mimi nilizaliwa mtaa wa Kiembe Samaki mji mpya na ufinyazi wa udogo unafanyika hapo kwa iyo nilipofika meli nne nilianzisha kikundi cha ujasriamawa cha ufinyanzi “, alisema.
Alisema kazi hiyo ya ufinyazi aliianza tangu mnamo mwaka 1981 hadi sasa anaendeleza ujasriamali huo.
Alisema kuwa baada ya kuona watu wenye ulemavu na wao wanahitaji kazi za mikono alianzisha kikundi cha ufinyazi eneo la Muembe Makumbi ili kuwasaidia watu wenye ulemavu kuendesha kazi za mikono.
“Mnamo mwaka 2018 nilianzisha kikundi chengine cha ufinyazi kwa ajili ya watu wenye ulemavu tu ambao pia ninaendelea nao kwa kuwapatia kazi za ufinyanzi”, alisema.
Sambamba na hayo alisema kwa upande wa watu wenye ulemavu tayari watu 15 amewapatia ujuzi wa kazi ya ufinyazi ili kujiajiri na kujikwamua na hali ya umaskini.
“Lengo langu ni kuongeza idadi ya watu wenye ulemavu lakini nashindwa kuwaendeleza kutokana na kukosa eneo sahihi na pia eneo tunalofanyia kazi zetu tuliazima na tayari kuna mtu aliyejitokeza kutaka eneo lake ingawa bado tunaendelea na kazi hiyo ya ufinyazi na kundi hilo la walemavu”, alisema.
KAZI YA UPISHI WA VYAKULA.
Njuma alibainisha kuwa kazi nyengine ya mikono anayoendesha maisha yake na familia ni kupika mikate ya aina mbalimbali kwa ajili ya shuhuli na mikusanyiko ikiwa ndio ajira aliyokulia akiwa tangu mdogo.
“Kazi ya upishi nilianza nayo nikiwa mdogo na hadi sasa naendelea na upishi wa vyakula vya oda kwa akinamama wanaohitaji vyakula vya harusi maholini”, alisema.
Alisema kazi hiyo imempatia umaarufu mkubwa kutokana na kupika mikate ya mikate ya aina mbalimbali kama keki,mikate ya mayai,mchele na mengine ikiwa ni kazi yake nyengine ya mkono.
“Mimi tangu nipate akili zangu sijawahi kukaa bila kazi nikiacha kupika nafinyanya vyungu na mikungu,nikiacha huko naingia jikoni kupika vyakula vya oda na hata zawadi za maholini na mikate nimekuwa nikichukua kila muda”, alisema.
Njuma alisema kwa kazi ya upishi wa mikate yatari amewahi kuwafundisha zaidi ya watu 100 na tayari wengi wao wamejiajiri kupitia kazi za mikono.
KAZI NYENGINE ZA MICHEZO
Bi Njuma alieleza kuwa hakuwahi kutegemea usafiri wa mtu katika maisha yake ila mwenyewe ni dereva wa kwanza wa Pikipiki aliyewahi kuingia kwenye mashindano ya mbio za pikipiki kupitia mikutano ya siasa na hatakati nyengine za serikali.
“Nimewahi kuongoza mashindano ya mbio za Pikipiki kwenye mikutano ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka kadhaa pamoja na sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kupitia uwanja wa Amani”, alisema.
Alisema mbio hizo alikuwa anakimbia umbali wa zaidi ya kilomita 50 kutoka Mji wa Zanzibar hadi Makunduchi ambapo aliwahi kushindana na makundi mengine ya vijana wakati huo wa 1988 na kuendelea.
“Washindani wangu wakubwa walikuwa Maboro,Kisuamku, Malboro na baharia ambao ndio waliokuwa wakiongoza misafara pamoja”, alisema.
MAFANIKIO YA NJUMA
Alisema moja ya mafanikio aliyopata ni pamoja na ujenzi wa nyumba zake na pia kuunganisha wanawake katika kazi za ujasriamali.
Alisema mafanikio mengine kuwafundisha kazi za mikono watu wenye ulemavu na kuwaunganisha wanawake na wanaume katika kujiunga na saccos.
Hata hivyo alisema amekuwa mchango mkubwa kwa jamii pamoja na kupata umaarufu na jamii hasa kwenye kuwapatia huduma za chua watoto wenye walemavu wa viungo.
CHANGAMOTO ZA NJUMA
Alisema changamoto alizokumbana nazo ni za kawaida kwenye maisha yake yote kutokana na kujiamini.
“Mimi kwa upande wa changamoto ni za kawaida kwani ninao uwezo wa kuonana na yoyote ninapotaka kufanikisha kazi zangu za ujasiriamali aqu kazi nyengine” alisema.
MALENGO YA NJUMA
Kuwasaidia wanawake wengi zaidi licha ya kumaliza umri wake wa kufanya kazi serikalini ili kila mwanamke au mtu mwenye ulemavu afaidike na matunda yake.
“MASHIRIKA ALIYOFANYA NAYO KAZI
Njuma alisema alifanya kazi na Shirika lisilo la kiserikali (NGO) la kimataifa linaloshuhulika na kulinda haki na kuboresha maisha ya (save the Children) alifanya nao kazi kwa muda wa miaka mitano kama ni mtoa huduma kwa watoto mwenye ulemavu wa viungo.
“Wakati nafuatilia kesi za watoto wenye ulemavu nililazimika kutumia Pikipiki kurahisisha kazi kwenda vijiji tofauti na kufuatilia watoto mwenye ulemavu na mimi ndie mwanamke wa kwanza kuendesha pikipiki nikiwa muhudumu wa afya na shirika hili liliniunga mkono”, alisema.
Alisema hadi sasa anaendelea na kazi hiyo ya kufuatilia watoto wenye ulemavu wa viungo vijijini na kueleza kuwa anajivunia kazi hiyo kwani tayari amesaidia jamii.
TAKWIMU ZA SACCOS
Kwa mujibu wa bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuna vyama vya ushirika 7,621 vilivyosajiliwa ikiwemo vyama vyote vya ushirika kama Saccos.
HISTORIA YA NJUMA
Njuma alizaliwa mwaka 1965 mtaa wa Kiembe Samaki mji mpya na kuanza skuli ya msingi Jang’ombe Unguja, mnamo mwaka 1972 na kuendelea skuli ya Miti ulaya kisiwani Pemba 1981 hadi alipomaliza kidatu cha tatu skuli hiyo.
Njuma alifunga ndoa mnamo mwaka 1981 na mnamo mwaka 1982 alipata mtoto wa kwanza.
Hata hivyo maisha ya Njuma yalianza kuonekana mnamo mwaka 1984 alipojiunga na chuo cha afya Sebleni kwa Wazee Unguja kwa kusomea kama bibi afya hadi 1986 alipomalizia masomo yake kwa ngazi ya cheti.
Njuma alianza kazi 1986 baada ya kuajiriwa na Wizara ya afya Zanzibar na kupangiwa kituo cha kazi Uwanja wa ndege wa Zanzibar kama bibi afya na alifanya kazi kwa kipindi cha miezi nane na kuhamishiwa kituo cha kazi cha Mbweni Matrekta Unguja mnamo mwaka 1987.
Hata hivyo alijiunga na Jeshi la kujenga uchumi JKU kwa kuwa kipindi hicho ilikuwa ni lazima kwa kila mfanyakazi apitie kwenye mafunzo hayo ya kijeshi ingawa hakutaja mwaka alioingia kwenye mafunzo.
“Nilipopata miezi mitatu kambini nilipata nafasi ya kwenda kuonana na familia yangu na kumkuta mtoto wangu ambae alikuwa nanyonyesha amedhoofika mno kiafya niliamua kuomba barua ili nikatishe mafunzo kwa kumnusuru mtoto wangu na serikali ilinikubalia nashukuru “, alisema.
Hata hivyo mnamo mwaka 1988 alirejeshwa kituo cha kazi cha Mnazi mmoja akiwa na nafasi ya bibi afya hata hivyo mwaka huo huo aliteuliwa kwenda kufuatilia watoto wenye ulemavu mchanganyiko vijijini na baadae kuhamishiwa umoja wa watu wenye ulemavu Kikwajuni.
Alisema mnamo mwishoni mwa mwaka 1988 aliendelea na masomo ya miezi sita ya marekebisho ya watoto wenye ulemavu nchini Uganda na baadae kuhamishiwa Ofisi ya watu wenye ulemavu wilaya y magharibi ‘B’ Dimani kitengo cha marekebisho cha watu wenye ulemavu na baadae kuhamishiwa kituo cha kazi Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja baada ya akima mama wengi kushindwa kufuatilia huduma za afya kituo cha Mnazi mmoja hadi sasa anafanya kazi hiyo.
“Nilipoanza kazi huko Kaskazini nilikutana na changamoto mbalimbali za watu wenye ulemavu na kuanza kufanya kazi kwa karibu mno na watu wenye watoto wenye ulemavu hadi kufika kupewa mtoto mmoja katika kijiji cha Matwemwe na nimemlea kama mtoto wangu na sasa tayari anakibarua chake na bado naishi nae kama mtoto wangu”, alisema.
Njuma anawatoto watoto sita akiwemo mmoja aliyepewa baada ya kufanya kazi ya mazoezi ya viungo kwa watoto wenye ulemavu.
Comments
Post a Comment