SERIKALI imesema bandari ya Fumba itakuwa na uwezo wa kushusha na kupakia kontena 40 kwa wakati mmoja ifikapo Januari mwakani hali itakayorahisisha ushushaji wa mizigo katika bandari hiyo na kuondosha usumbufu kwa wafanyabiashara.
Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar Akif Ali Khamis alisema hayo Fumba wakati akitoa maelezo ya ujenzi wa gati ya bandari hiyo kufuatia ziara iliyofanywa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yussuph Juma Mwenda aliyefika bandarini kukagua ujenzi wa bandari hiyo.
Alisema ujenzi wa bandari utakapokamilika utarahisisha usafirishaji wa mizigo kwa wafanyabiashara na kuongeza mapato kupitia mamlaka ya mapato TRA hasa usafirishaji wa mizigo.
Alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kushusha vyombo 750 kwa wakati mmoja kutokana na ukubwa wa bandari na kueleza kuwa bandari itarahisisha ushushaji wa mizigo kutofautisha na bandari ya Malindi ambayo inashusha kontena 10 hadi 12 kwa wakati mmoja hali inayoleta usumbufu kwa wafanyabiashara na kusababisha ucheleweshaji wa mizigo bandarini.
Alisema bandari hiyo ni ya kwanza kujengwa kati ya serikai na sekta binafsi na kueleza kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi imekamilika na sasa inaendelea awamu ya pili.
Alisema bandari hiyo itakapomilika itaongeza uwezo mara mbili ya kushusha na kupakia mizigo kuliko bandari ya Malindi ambapo bandari zote zitakuwa na uwezo wa kushusha kontena 80.
Alisema bandari hiyo ni chanzo kikubwa cha mapato kwa mamlaka ya Mapato Tanzania na TRA hasa biashara ya forodha ambayo wafanyabiashara watakuwa na fursa ya kusafirisha mizigo yao moja kwa moja kupitia bandarai hiyo.
“Pia bandari itawekwa skana ambayo itawezesha kushusha mizigo na kuondosha usumbufu pamoja na kuunganisha mifumo kumuwezesha mfanyabiashara kufanya malipo sehemu yoyote alipo”, alisema.
Alisema Shirika la Bandari litaongeza zaidi mashirikiano na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ili kukuza uchumi wa nchi.
“Kwa sasa mizigo inayoingia nchini inaingia kupitia bandari ya Mombasa na lamu Kenya hali inayochelewesha uingizaji wa mizigo na kuwa changamoto kubwa kwa wafanyabiashara”, alisema.
Alisema mizigo inayoshushwa bandari hizo inaongeza gharama za usafirishaji na kuleta usumbufu kwa wafanyabiashara.
“Utakapokamilika ujenzi wa bandari ya Fumba usafirshaji wa mizigo utapungua gharama kwa asilimia 30 na kuwawezesha wafanyabiashara kuleta bidhaa nyingi zaidi na kuongeza mapato na wafanyabiashara wanapoleta mizigo kwa wingi hata ukusanyaji wa mapato utaongezeka na kuongeza tija kwa bidhaa wanazoingiza nchini”, alisema.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzani (TRA) Yusuph Juma Mwenda alisema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa bandari hiyo ya fumba na kueleza kuwa kukamilika kwa bandari hiyo TRA intaongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato hasa usafirishaji wa mizigo kupitia bandari hiyo.
Sambamba na hayo aliiwapongeza wakandarasi wa ujenzi wa bandari hiyo na kueleza kuwa kazi wanayoifanya inakwenda sambamba na matakwa ya serikali ya kujenga bandari kwa wakati ili kuondosha usumbufu kwa wafanyabiashara.
MWISHO
Comments
Post a Comment