NA TATU MAKAME, ZANZIBAR@@@
UNAPOZUNGUMZIA ukakamavu alionao mwanamke huwezi kusahau jinsia yake kutokana na kazi wanazofanya wanawake katika jamii kutokana na mchango wao kwa taifa.
Hata hivyo wanawake wamekuwa na mchango mkubwa wa kuelimisha jamii katika mambo mbalimbali bila kusahahu kuwa wao ni viongozi katika majukumu wanayoyasimamia.
Mtazamo wa jamii ni kuwa mwanamke ni kiumbe dhaifu na hawezi kufanya jambo la maendeleo katika jamii inayomzunguuka.
Hata hivyo kwa kuwa serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa viongozi wanawake kuona asilimia 50 kwa 50 inafikiwa jamii imekuwa na mtazamo tofauti kuhusu mwanamke hasa katika kuanzisha mambo mbalimbali katika jamii.
Aidha unapozungumzia nafasi za uongozi katika ngazi za jamii huwezi kumsahau Zainab Abdi Salum ambae ni dereva aliyeamua kuanzisha chuo cha udereva kuwaokoa madereva vijana na ajali za barabarani.
Zainab alizaliwa mwaka 1984 katika mtaa wa Kisauni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na kuanza skuli ya msingi Kiembe Samaki mnamo mwaka 1995 hadi 2001 na baadae kuendelea na kidato cha kwanza skuli ya sekondari ya Kiembe Samaki 2003 hadi 2004 hata hivyo aliendelea na kidato cha tatu na nne skuli ya sekondari Mbarali mkoa wa Mjini Magharibi Unguja mnamo mwaka 2004-2005.
Mnamo mwaka 2006 alijifunza kazi za mikono kama kushona cherehani na kufanya kazi za biashara ndogondogo hadi 20015 alipojifunza kazi ya udereva wa gari hadi 2002 alipoanzisha Chuo cha udereva Zeyna Driving school.
Zainab alisema ameamua kujifunza kazi ya udereva kutokana na kujitokeza kwa madereva wengi wazembe mbao huendesha gari bila ya uangalizi ili kuwafundisha alama za barabarani.
Alisema aliamua kuingia katika fani ya udereva ili awe mfano kwa jamii jinsi ya kuwafunzisha madereva kutumia alama za barabarani ambazo ni muhimu kwa madereva wanaoendesha vyombo vya moto.
“Baada ya kuona ajali za barabarani zimekuwa nyingi hasa kwa vijana niliamua kuanzisha chuo cha udereva ili niwe mfano kwa wanawake na jamii kuwa dereva mwanamke lakini nimewasaidia madereva wengi kujua sheria za usalama barabarani.
Alisema kuwa alichogundua vijana wengi huendesha gari bila kupata mafunzo ya udereva hali inayozidisha ongezeko la ajali za barabarani.
Alisema moja ya jambo ambalo hatosahau katika maisha yake kutoa elimu ya usalama barabarani wakati anapokuwa na wanafunzi wake darasani hasa kuwasiamamia jinsi ya kusoma kwa undani alama za barabarani.
Alisema tangu kuanza kazi ya kuwafundisha vijana kuendesha gari wengi wao wamekuwa na mwamko wa kufuata sheria za usalama barabarani ili kujikinga na ajali.
Alisema licha ya kudharauliwa na jamii kwa kuanzisha chuo kwa kuwa mwanamke bado anandoto za kuwafundisha madereva wengi zaidi hasa wanawake ambao bado mtazamo wao kuwa mwanamke hawezi kufikia maendeleo.
Alisema baada ya kuona vyuo vingi vya udereva vya wanaume na yeye aliamua kuanzisha chuo chake ili kutoa elimu jinsi ya kuendesha gari pamoja na kuzingatia alama za barabarani.
Aliwataka wanawake wengine kujitokeza kufungua vyuo vya udereva kwani kuna nafasi mbalimbali za kujifunza na pia kujiajiri kupitia sekta hiyo ya udereva.
WATU ALIOWAFUNDISHA KUENDESHA GARI.
Zena alisema zaidi ya watu 1500 tayari amewapatia mafunzo ya udereva kupitia cho cha Zeyna Driving school kilichopo Mpendae Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
MAFANIKIO
Zena alisema amekuwa mfano na kuacha utegemezi kutoka kwa familia yake kutokana na kumudu gharama za uendeshaji wa maisha na anaendesha maisha yake na familia.
Alisema mafanikio mengine kuwafundisha vinaja wengi kuendesha gari na kuwa mfano kwa jamii inayomzunguuka hasa katika kujiajiri.
CHANGAMOTO
Moja ya changamoto ya Zainab kuwa na mtaji mdogo wa kuendesha biashara ya uredeva na kueleza kuwa analazimika kutumia gari mbili za kufundishia.
“Changamoto hii inanipa wakati mgumu licha na moyo wangu wa kutaka kuwasaidia vijana lakini vifaa ninavyofundishia bado kidogo na vina nipa wakati mgumu”, alisema Zainab.
Alisema changamoto nyengine jamii kutojua thamani yake kwa kuwa ni mwanamke pekee aliyeanzisha Chuo cha udereva kwa hapa Zanzibar.
MALENGO YAKE.
Kuwafundisha vijana wengi zaidi kuendesha gari pamoja na kuongeza wataalamu watakaokuwa mfano katika taifa hasa kutoa elimu ya matumizi ya alama za barabarani.
MKUFUNZI KUTOKA SUZA
Kwa mujibu wa Mkufunzi kutoka Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Imane Duwe wakati alipotoa mafunzo ya uongozi kwa waandishi wa habari alisema kiongozi sio lazima awe mwanasiasa au mtu maarufu.
Hata hivyo kauli ya Mkufunzi huyo imeakisi pale tunapowaona wanawake wanafanya kazi kubwa na kuwa viongozi wa mifano katika kuanzisha mambo ya muhimu ambao pia wamekuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
TAMWA ZANZIBAR
Kwa uande wake Ofisa program na mawasiliano kutoka Chama cha waandishi wa habari Tanzania Twamwa ZNZ Nairat Ali Haji alisema mradi wa SWIL ambao unaimarisha uongozi wa wanawake kwa kuona waandishi wa habari wanaandika makala zinazohusiana na uongozi kwa wanawake pamoja na Takwimu.
Hata hivyo alisema mwamko umekuwa mkubwa kwa jamii kuachana na mfumo dume wa kuona mwanamke hawezi kuwa kiongozi mpaka asimamiwe.
Alisema ushirikiano wa serikali na taasisi binafsi za kutoa elimu ya umuhimu wa wanawake kuingia katika ngazi za uongozi umesaidia wanawake wengi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uongozi kwa wanawake.
MWENYEKITI BODI YA USALAMA BARABARANI
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Mkadam Khamis Mdam kwa kipindi cha miaka mitano 2021/2025, alisema takwimu za ajali zinaongezeka kila mwaka licha ya madereva kufundishwa jinsi ya kujikinga na ajali za barabarani.
Alisema jumla ya ajali 206 ziliripotiwa 2021, kati ya hizo ajali zilizosababisha vifo 151, na vifo vilikuwa 169 kati ya hao wanaume 126 na wanawake 14, majeruhi kwa mwaka huo walikuwa 196 wanaume 122 na wanawake 33, na makosa ya usalama barabarani yalikuwa 22,400.
Mwaka 2023 jumla ya ajali 193 ziliripotiwa kwa Zanzibar, ajali zilizosababisha vifo 140, vifo vilikuwa 156 na majeruhi mwaka huo walikuwa 201, wakati makosa 38895.
Mwaka 2024 jumla ya ajali 227 ziliripotiwa, ajali zilizosababisha vifo 175, vifo vilikuwa 199 na majeruhi 259 na makosa yalikuwa 49,789
Mwaka 2025 jumla ya ajali 264, ajali za vifo zilikuwa 206, vifo vilikuwa 233, majeruhi 258 na makosa yalikuwa 71,231.
MAJUKUMU YA MAMLAKA
Kwa mujibu wa Mwanasheria kutoka Mamlaka ya usafiri na usalama barabarani Zanzibar Vuai Hassan Vuai alisema moja ya jukumu la mamlaka hiyo kusimamia usajili wa vyombo vya moto na uratibu wa utoaji wa leseni,kusimamia uanzishwaji wa skuli za udereva na utoaji wa leseni kwa walimu.
Alisema jukumu jengine kusimamia utaratibu wa mafunzo kwa madereva au kutambuliwa kwa walimu wa madereva kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa chini ya sheria hii.
Pamoja na kusimamia utoaji wa leseni kwa gari za biashara, kusimamia mpango wa kusimamia viwango vya vyombo na ukaguzi,na kuweka madaftari ya usajili wa vyombo vya moto na madereva.
Hata hivyo alisema mamlaka pia inasimamia kwa karibu wasimamizi na waanzilishi wa vyuo vya udereva hapa Zanzibar ili kupunguza makosa ya usalama barabarani.
Alisema Zanzibar ina vyuo vya udereva 32 kati ya hicho kimoja kimeanzishwa na mwanamke ambae amejitokea katika mamlaka hiyo kuomba lesseni ya kuanzisha chuo kwa kuwa anauwezo wa kuanzisha chuo.
Alisema mwanamke huyo amekuwa mfano kwa jamii kwa kuanzisha chuo cha udereva ambacho kimepigiwa mfano na madereva wengi waliopata mafunzo kupitia chuo hicho.
Alikitaja chuo hicho kuwa ni Zyna Driving School ambacho kinatoa mafunzo kwa rika mbalimbali za vijana katika kuwafundisha jinsi ya kuendesha vyombo vya moto hasa udereva wa gari.
Hata hivyo anawataka wanawake kujitokeza kuanzisha vyuo vya udereva ili kuwa mfano kwa jamii hasa kutoa elimu ya usalama barabarani pamoja na kusoma sheria zinazohusu uendeshaji wa udereva kwa waendesha vyombo vya moto.
mwisho


Comments
Post a Comment