IMEANDIKWA NA ZUHURA
JUMA, PEMBA
"SIKATI
tamaa ipo siku nitafanikiwa lengo langu nililolikusudia kwa sababu kila kitu
kimepangwa kwa muda maalumu, hivyo naamini bado wangu haujafika"
Sio maneno ya mtu mwengine bali ni Awena Salim Kombo mwenye umri
wa miaka 50 mkaazi wa shehia ya Kangagani Wadi ya Kiuyu, Jimbo la Kojani Wilaya
ya Wete Pemba.
Awena ni mwanamke shupavu mwenye ndoto ya kuwa kiongozi tangu
akiwa kijana mdogo, na ndipo mwaka 1990 alipoamua kujiunga kwenye chama cha
Mapinduzi CCM, ili kusudi apate nafasi ya kuwa kiongozi.
Lengo lake la kusaka uongozi ni kutaka kusaidia jamii kwenye
mambo mbalimbali ikiwemo kutatua changamoto zinazowakabili.
"Hivi sasa baadhi ya wanajamii wenye matatizo hunifuata
kutaka msaada, hivyo wakati mwengine nashindwa kutokana na hali yangu
kutomudu" anaeleza.
Mwaka 2017 Awena alianza kupata nafasi za uongozi katika chama chake,
ambapo alijiona tayari anaenda kutimiza ndoto zake alizokuwa akiziwaza mara kwa
mara kwenye maisha yake.
Alianza kushika nafasi ya Mjumbe wa Wadi UWT, na baadae akagombea
nafasi ya Katibu wa Jimbo wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ingawa hakufanikiwa
kwenye nafasi hiyo.
Kwa sasa Awena anashikilia nafasi ya Katibu wa Wazazi Wadi ya
Kiuyu, ambapo nafasi zote hizo aligombea na kushinda.
"Kwa vile lengo langu ni kuwa kiongozi na kuwaletea
wananchi maendeleo, sikufikia hapo bali niliendelea kugombea na kushikilia
nafasi mbalimbali ndani ya chama changu," anaeleza Awena.
Anasema, bado hajachoka ataendelea kugombea nafasi za uongozi,
ili aweze kutimiza ndoto zake za kuwasaidia wananchi wa Jimbo lake.
Mama huyo anashikilia nafasi mbalimbali ndani ya chama, ndipo
alipoona sasa kuna haja ya kuingia kwenye vyombo vya maamuzi ili lengo lake la
kuwatumikia wananchi aweze kulifikia.
"Nilijiona kuna nafasi nyingi nimeshikilia ndani ya chama
changu, lakini nilisema kuwa bado lengo langu sijalifikia, hivyo lazima
nipambane, ingawa nimeshawahi kugombea udiwani viti maalumu lakini kura
hazikutosha kwa upande wangu," anasema.
Awena anasema ni mwiko kukata tamaa, na ilipofika mwaka 2020
hakuwa nyuma alikwenda kuchukua fomu ya kugombea uwakilishi Jimboni, ingawa hakupita
kwenye kinyang'anyiro hicho tangu ngazi ya nchini.
Alipokwenda kuchukua fomu baadhi ya wananchi walimkebehi na
kumuhisi kwamba hawezi, ingawa hakusikiliza maneno hayo na kuamua kusonga
mbele.
Anahadithia kuwa, ilikuwa ni ngumu kuingia jimboni kugombea
kutokana na wanaume kumkwaza kwa kile wanachodai kuwa, nafasi za wanawake ni
viti maalumu pekee na za majimboni ni za wanaume tu.
"Kwa kweli maneno yao yanaweza kukuvunja moyo ikiwa
hukusisimama kidete kwenye jambo hili, na niliwaambia kuwa nimeshaweka nia ya
kugombea na nimeamua," anahadithia
Baadhi ya wanajamii pia walikuwa na mtazamo hasi tofauti na
sasa, hivyo waliona kama nahangaika na kuharibu pesa bila kujua kwamba
anatarajia kitu gani kwa kile anachokipambania.
Aliwaeleza kuwa, hawezi kupindisha kauli ya lengo lake hasa kwa
vile chama chao kinazingatia jinsia, jambo ambalo linampatia nguvu zaidi.
"Pia mume wangu na familia yangu inaniunga mkono kwa hiyo
sikutetereka katika hili, nilikwenda kuchukua fomu, na nashukuru hata kama
nimekosa nafasi lakini kila siku zinaposogea nazidi kuwa jasiri na imara,"
anasema Awena.
Katibu huyo wa Wazazi Wadi ya Kiuyu, anasema licha ya kukosa
awamu zote kwa nafasi mbili za udiwani na moja ya uwakilishi, lakini hajakata
tamaa na itakapofika mwaka 2030 atagombea tena kwenye jimbo lake.
Anaeleza kuwa, kipindi kifupi kijacho pia kutakuwa na chaguzi za
ndani ya chama, hivyo nazo hatokuwa nyuma katika hilo na atagombea.
Mama huyo anaeleza, pindi atakaopata nafasi na kuingia kwenye
chombo cha maamuzi, anaamini atapata nafasi ya kuwasilisha changamoto
zinazowakabili wananchi na kuweza kutatuliwa kwa haraka.
Vile vile atapata fedha za kuwasaidia wananchi wake pale
wanapotokezewa na tatizo ama la jamii kwa pamoja au la mtu mmoja mmoja kama
anavyofanya sasa.
"Jamii inanipenda hasa pale wanaponiona nasaidia wenzangu
kwa hali na mali, hivyo naamini nikipitishwa tu kwenye chama changu kugombea,
basi naamini Jimbo nitalichukua," anaeleza.
Mama huyo hakushawishiwa na mtu yeyote kugombea uongozi, bali
yeye mwenyewe anaupenda kutoka moyoni ili apate nafasi ya kuwasaidia wanajamii
na Taifa kwa ujumla.
Kupitia nafasi aliyonayo kwa sasa Awena amepata faida nyingi
ikiwemo kujuana na watu mbalimbali na kushirikiana nao, sambamba na kupatiwa
usafiri wa pikipiki ambayo inamsaidia kutekeleza vizuri majukumu yake ya chama
na Serikali.
"Hata jamii inanikubali sana na kuniamini, kwani panapokuwa
na jambo huniweka mstari wa mbele, hivyo najivunia sana," anaeleza.
Mbali na uongozi wa chama anaosimamia, pia ni Mratibu wa
Wanawake na Watoto wa shehia ya Kangagani na pia ni mjasiriamali wa kilimo cha
chakula, mboga na matunda.
"Sijazoea kukaa tu bila kujishughulisha, kwa sababu hicho
ninachokipata pia nasaidia wengine wanapotokezewa na shida, ingawa soko la
bidhaa hizo wakati mwengine ni shida," alieleza.
Awena ameolewa na ana watoto kumi, ambapo amesoma skuli ya
msingi Ole na kumalizia kidato cha nne katika skuli ya Sekondari Utaani Wete.
Mume wa Awena, Hasnuu Fakih Hassan anasema kuwa, mke wake ni
mchapa kazi katika kila sekta, hivyo anaamini akipewa nafasi ya kuwatumikia
wananchi basi atafanya kazi kwa juhudi zote.
Anaeleza kuwa, anamuunga mkono kwenye harakati zake zote za
uongozi na kugombea nafasi mbalimbali, kwani ameshamuona kwamba ni mwanamke
jasiri na anaweza kusimama popote kutetea haki za wananchi.
"Hata hapa nyumbani anasaidia sana wananchi wanapokuja na
matatizo yao, hivyo atakapopata nafasi ya kuingia kwenye chombo cha maamuzi
atatetea wananchi na changamoto zote zitaondoka," anasema.
Badria Juma Issa ni dada anaemfahamu Awena na kusema kwamba, ni
mwanamke anaefaa kuwa kiongozi kwa imani yake ya kusaidia wengine hata kama
alichonacho hakitoshi, hivyo wanawake kama hao ni muhimu katika maendeleo ya
jamii husika.
Anasema, Awena anajiamini sana na ndio maana hawezi kukata tamaa
kirahisi kwa sababu kama ni mtu mwengine angekuwa hagombei tena kutokana na
vipindi kadhaa kukosa nafasi.
Ingawa kwake yeye amechukulia changamoto hiyo ni kama fursa ya
kujiandaa upya katika chaguzi zijazo.
Katibu wa CCM Jimbo la Kojani Tamimu Ali Omar mkaazi wa Mchangamdogo
anamuelezea Awena kuwa ni, mtendaji na mfuatiliaji mzuri wa masuali mbalimbali
ya chama na jamii, kiasi ambacho kinampa siha ya kuwa kiongozi bora.
‘’Tayari ameshaanza kuonesha uwezo wake kwa kujitolea katika
kusaidia wengine wenye changamoto, pia kwa vile ni mama lazima atakuwa na
huruma juu ya kuwasaidia wanawake wenzake na jamii kwa ujumla,’’ anasema Katibu
huyo.
Mratibu wa Programu ya SWILL kutoka TAMWA Zanzibar Sabrina Ali
Mwatanga anafafanua, wanaendelea kuelimisha na kuhamasisha uongozi kwa wanawake
ili waingie kwa wingi katika vyombo vya maamuzi kwa ajili ya kutetea mambo
yanayowahusu pamoja kuleta maendeleo kwenye majimbo yao.
Hiyo ina lengo la kuongeza ushiriki wao katika uongozi na siasa,
kuimarisha mipango ya maendeleo jumuishi na kuweka msingi imara wa maandalizi
ya uchaguzi wa mwaka 2030.
‘’Itakapofika mwaka 2030 tunataka tuwaone wanawake wengi
wanaingia kwenye mchakato wa uchaguzi na kufanikiwa, hii itasaidia kutetea
mambo yao yanayowahusu na masuala mengine ya kijamii, kwani tunawaona
waliofanikiwa namna wanavyoleta maendeleo katika maeneo yao,’’ anasema.
Anawanasihi wanawake wote ambao wana nia ya kugombea wasivunjike
moyo bali waendelee kupambana, ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na usawa kwenye
vyombo vya maamuzi.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka TAMWA Zanzibar mwaka 2020-2025
wawakilishi wanawake walikuwa nane (8) sawa na asilimia 16, huku wanaume wakiwa
42 sawa na asilimia 84, ambapo idadi ya wote walikuwa 50.
Mwaka wa uchaguzi uliofuata wa 2025-2030 wawakilishi wote ni 50,
ambapo wanawake ni wane (4) sawa na asilimia nane na wanaume ni 46 sawa na
asilimia 92.
Serikali kwa kutambua umuhimu
wa mwanamke, sera na sheria mbalimbali za Zanzibar zimeeleza kuhusu haki ya
wanawake kushiriki katika demokrasia na uongozi.
Kifungu cha 21 (2) cha Katiba
ya Zanzibar ya mwaka 1984 kimeeleza kwamba, kila mzanzibari anayo haki na uhuru
wa kushiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu
mwanamke na taifa lake.
Azimio la kimataifa juu ya haki
za binadamu la mwaka 1948 ambalo ndio msingi wa haki zote za binadamu, ikiwemo
haki za kiraia na kisiasa linatoa haki kwa kila mtu katika uongozi wa nchi.
MWISHO.



Comments
Post a Comment