NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@
KATIKATI
ya giza nene lililogubika haki ya mwanamke kuwa kiongozi kwa wakati huo, kuna mwanamke
alielishinda?.
Alisimama kidedea, yeye na waliomzunguka
walihakikisha anafanikiwa na kweli alishika nafasi mbalimbali za uongozi, mpaka
kuwa mmoja wa viongozi wanawake walioweka alama isiyofutika katika jamii.
Ni Hanuna Ibrahim Massoud, alieanza kuliona jua mwaka
1959, Kisiwani kwa Binti Abedi wilaya ya Wete kaskazini Pemba.
Alianza kusaka elimu yake ya msingi, mwaka 1965,
ambapo aliipata katika skuli tofauti kama Ziwani, Shamiani na Utaani.
Mnamo mwaka 1974, alikamilisha elimu yake ya
sekondari kidato cha nne, katika skuli ya Fidel Castro.
“Safari yangu ya masomo haikuwa na kituo kimoja,
nilisoma maeneo mengi, lakini huku kulinifanya kuyajuwa na kuyatawala vizuri mazingira,’’anahadithia.
Kumbe wakati huo kuelimika kwa mtoto wa kike hadi
kidato cha nne, ilikuwa fursa adimu na nimsingi mkubwa wa ukombozi.
Safari yake ya kutafuta elimu, ikaendelea hadi miaka ya 1970, alipopata nafasi ya
kujiendeleza kimasomoni Mkoani Moshi kwa miezi tisa, ambako alijifunza mafunzo
ya uongozi.
Anakiri mafunzo hayo, yalimpa msingi wa uongozi na
utawala, usimamizi wa rasilimali watu, na mbinu za kushughulikia kero za
wananchi.
Maana mwaka 1987, uwezo wake wa kufanya kazi,
uaminifu na uzalendo ukasababisha kuchaguliwa, kuchukuwa kozi ya sayansi ya
jamii nchini Urusi.
HANUNA
KATIKA UWANJA WA SIASA
Hanuna Ibrahim Massoud, aliwahi kuwa mwanasiasa
mwenye ushawishi mkubwa.
Mbio zake za kisiasa, zilianzia mapema skulini akiwa
ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), aliejiunga na ‘Young Paunia’ (Chipukizi
kwa sasa), ambako alishika nafasi mbalimbali, kama Mwenyekiti.
Kisha baada ya kumaliza kidato cha nne, alianza
kujihusisha na shughuli za Umoja wa vijana (UVCCM), katika chama chake cha
Mapinduzi.
Wakati akiwa huko, alishika nafasi mbalimbali za
uongozi katika jumuiya za chama, kama Mjumbe wa Jumuiya ya Wazazi wa tawi lake la
Kichungwani na Mjumbe wa UWT tawi hilo.
Nafasi nyengine ni Katibu wa Wazazi katika Tawi la
Kichungwani, pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Vijana na wanawake
tawini humo.
“Kwamara ya kwanza kwenye siasa, nilikuwa mwenyekiti
wa ‘Young Paunia’ wa skulini, nilipomaliza na kujiunga katika jumuiya ya vijana,’’anakumbukia.
Anasema hapo ndipo akawa anashika nafasi kama ujumbe
UWT, Mjumbe wa kamati tekelezaji ya vijana na wanawake tawini.
Losha Hanuna, alichaguliwa kuwa Katibu wa Vijana
Wilaya ya Wete, nafasi alioipata baada ya ushindani mkubwa, uliokuwepo baina
yake na wanachama wingine ambao wengi walikua wanaume.
Anasema miaka yote hayo, ilikuwa ni kama maandalizi
yake, katika kumjengea ujasiri na ukakamavu wa kuwa kiongozi, katika duru za
kisiasa.
Safari yake, iliiva rasmi 1990, wakati siasa za
Zanzibar zikiwa katika mfumo wa Chama kimoja, ambapo aligombea nafasi ya Uwakilishi
Jimbo la Chake Chake.
Maana kwa wakati huo, CCM Chake Chake ilisimamisha
wagombea wawili, ambao ni yeye na mwenzake Abdallah Said Haji, aliekuwa na
ushawishi na umaarufu mkubwa.
Mwenzake huyo ambae kwa sasa ni marehemu, wakati
anasimama jukwaani kuomba ridhaa za wananchi, alikuwa ni Waziri wa Kilimo
Zanzibar.
Tena jambo lililomfanya kushindwa kujiamini katika
kinyang’anyiro, hicho hasa kwa umaarufu wa mwenzake wake kwenye siasa.
“Mwaka 1990 nilikuwa Ofisini kwangu, akaja dadaangu
Ashura Abeid (marehemu), akaniambia nikachukuwe fomu ya kugombea wa Uwakilishi,
na Abdallah utamshinda, sikuwa tayari kwa hilo,’’anafafanua.
Anahadithia mchuano huo, ulikuwa wa kihistoria,
kwani alimshinda mgombea mwenza aliekuwa Waziri wa Kilimo, kwa wakati huo kwa
kura zaidi ya 100 kutoka kwa wananchi.
Anasema jambo hilo, liliwashangaza wengi, kuanzia
familia yake, jamii, chama chake na hata yeye mwenyewe, kwani ilikuwa kama
“Ngamia kupita katika tundu ya sindano”,
Kampeni zake, ziligubikwa na maneno kama “maajabu
mwanamke kugombania”, “wanawake wakae wapike tu” huku wengine wakienda mbali zaidi
kwa kusema “na apoteze muda bure, mwanamke hawi kiongozi”.
Hanuna anaeleza, aliitumikia nafasi ya Uwakilishi wa
jimbo la chake chake kwa mitano hadi, ulipokuja mfumo wa vyama vingi.
Mwenyewe anaeleza “uchaguzi wa mwanzo wa vyama vingi
wananchi waliniambia nigombee na tuko pamoja na wewe, isipokuwa mara hii chama chako
kiwe CUF, sikuweza kuiacha CCM.
MCHANGO
WAKE KATIKA JAMII
Mkaazi wa Chake Chake Mohamed Ali Mohamed anaeleza,
baada ya kuingia katika baraza la Wawakilishi Hanuna, alielekeza nguvu zake,
katika kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
“……hee!! Hanuna alituziba midomo, zile zana za
mwanamke hawezi ziliishia pale, alikuwa Mwakilishi mzuri wa wananchi, alipita kusikiliza
kero zetu na alizifanyia kazi”, anahadithia.
Anasema Hanuna, akiwa Mwakilishi ndie aliepigania ujenzi
na ukarabati wa madarasa katika skuli ya Pondeani na Michakaini msingi kwa
wakati huo.
Salma Ali wa Shungi, anasema Hanuna alipokuwa Mwakilishi
wao, alipambania ujenzi wa kituo cha Afya Shungi, kwa kuomba ufadhili wa vifaa
kama bati na saruji.
“Tulikuwa na changamoto ya kituo cha afya, Hanuna
alipopata Uwakilishi, alitafuta wafadhili, mpaka ujenzi ukakamilika na hadi
sasa kinatumika” anaeleza.
Said Kheir Said mkaazi wa Pondeani anasema, akiwa
Mwakilishi mwanamke huyo, aliwatatulia changamoto ya ubovu wa daraja la
Pondeani na lile la Bandataka, ili kurahisisha usafiri.
BAADA
YA HAPO
Kutokana na uzoefu wake katika utawala
usiyotikisika, mwaka 1996, Hanuna aliteuliwa kuwa Afisa Tawala wilaya ya Chake
Chake nafasi aliodumu nayo hadi 2002.
Ambapo Rais Amani Abeid Karume, alimteua kuwa Afisa
Tawala na baadae kuwa Mkuu wa wilaya ya Chake Chake.
Hadi 2017, akateuliwa kuwa Msaidizi wa Rais kisiwani
Pemba, akijikita katika kuhudumia jamii na kusikiliza kero za wanachi.
Katika mwaka huo huo, aliteuliwa kuwa Afisa Mdhamini
wa Tume ya Maadili Pemba, nafasi aliyoihudumu nayo, mpaka alipostaafu mwaka
2019, akiwa afisa mdhamini wa mwanzo wa tume hiyo.
Hanuna baada ya kustaafu, mwaka 2020 alihudumu kama
Mkuu wa Utawala wa Chuo cha Mwalimu Nyerere Tawi la Pemba, na baadae sheria
ilipobadilika, alihudumu kama Afisa Utumishi wa Chuo hicho.
KABLA
YA SIASA
Ajira yake ya mwanzo, ni katika Wizara ya Biashara
alikuwa anafanyakazi kama Karani wa Fedha, pia aliwahi kufanya kazi Ikulu ya Wete
Pemba kama msimamizi.
Mtumwa Ali Khalifa ni miongoni mwa watu
waliofanyakazi kwa karibu na Hanuna anasema, utendaji wake ni kizalendo,
ujasiri na kupenda wenzake.
Aidha aliwahi kuhudumu kama Mpiga Chapa wa katibu wa
Baraza la Mapinduzi Zanzibar, pia Katibu Muhtasi wa wilaya ya Chake Chake na Katibu
Muhtasi wa Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba.
Hanuna Masoud “Bihanuna” kama wanavyopenda kuitawatu
wengi, ni mama wa familia wa watoto sita.
Anakiri mwanamke kuwa kiongozi, haibadilishi lolote
juu ya wajibu wa kuitumikia familia yake, anawasihi wanawake viongozi kujituma,
kuwajibika na kujiheshimu.
Anawasihi wanaume kuiga mfano wa mumewake, katika
kuwaunga mkono wanawake, kushiriki katika uongozi.
Mumewe wake Hanuna, Abuu-bakar Mohamed Ali anasema
anamuona mkewe ni kielelezo cha mwanamke shujaa, aliyetumia ujana na utu uzima
wake wote, kutumikia wananchi.
Bali haya hayakuja hivihivi, isipokuwa kwa juhudi za
serikali na wadau wengine wa kupambania haki za wanawake.
Mfano serikali ikaridhia Mkataba wa umoja wa Mataifa
wa kutokomeza aina zote za udhalilishaji (CEDAW) wa 1979, wenye ibara ya 7 inayoeleza
inagusia hilo,
“Nchi wanachama zihakikishe zinawapa wanawake fursa
za kushiriki katika uongozi,’’ infafanua ibara hiyo.
Lengo Namba 5.5 la maendeleo endelevu (SDGs,2015/2030),
lililozitaka nchi zote kuhakikisha, ushiriki kamili na waufanisi wa wanawake na
fursa sawa za uongozi, katika ngazi zote, iwe kisiasa na kiuchumi.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ibara yake ya 21
(1) inayoeleza kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki, katika shughuli za
utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia Wawakilishi waliochaguliwa
kwa hiari.
Hadi sasa TAMWA –Zanzibar wakiwa ni wadau wa
kuhamasisha na kutetea haki za wanawake, katika kupata fursa za uongozi,
wamekua wakiwapa mafunzo yakujitambua na kupambania haki zao.
Aidha TAMWA-Zanzibar wamekua wakitoa mafunzo kwa
waandishi wa habari, ili waweze kuandika habari zitakazoshajihisha wanawake
kuingia katika uongozi.
MWISHO




Comments
Post a Comment