Skip to main content

SAADA MKUYA AZINDUA SIKU 16 ZA KUPINGA UDHALILISHAJI, ATOA NENO

 


HOTUBA YA MHE. DR. SAADA MKUYA SALUM WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS FEDHA NA MIPANGO KATIKA UZINDUZI WA SIKU 16 ZA HARAKATI ZA KUPINGA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA, KATIKA UKUMBI WA CHUO CHA POLISI ZANZIBAR WILAYA YA MJINI MKOA WA MJINI MAGHARIBI -UNGUJA.  TAREHE 25/11/2024.

 

MHE. RIZIKI PEMBE JUMA,WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO.

MHE. ANNA ATHANUS PAUL, NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO,

MHESHIMIWA IDRISA KITWANA MUSTAFA, MKUU WA MKOA M/MAGHARIBI,

NDUGU KHATIB MWADINI, KAIMU KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAEDNELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO,

MUWAKILISHI WA SHIRIKA LA UN WOMEN,

MWAKILISHI WA SHIRIKA LA UMOJA WA MATAIFA LA IDADI YA WATU DUNIANI (UNFPA) ZANZIBAR,

WAHESHIMIWA WAKUU WA WILAYA MLIOPO,

NDUGU HAFIDH ALI, AFISA MDHAMINI WMJJWW,

WAKURUGENZI MBALI MBALI MLIOPO,

MAOFISA KUTOKA WIZARA NA MASHIRIKA MBALI MBALI,

WARATIBU WA WANAWAKE NA WATOTO,

WANAHARAKATI MBALIMBALI MLIOPO,

NDUGU WAANDISHI WA HABARI ,

NDUGU WAALIKWA, MABIBI NA MABWANA,

ITIFAKI IMEZINGATIWA.

 

 Asalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatu.

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mtukufu Mungu Mwingi wa Rehema na mwenye kurehemu, kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa tukiwa wazima wa afya.

Pili  nipende kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi  na kumpongeza kwa kutimiza miaka minne ya Uongozi wake ambao tumeshuhudia Mapinduzi ya maendeleo ya Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa yakiendelea ndani na nje ya nchi yetu. Tumuombee kwa Mwenyezi Mungu amzidishie Afya njema na nguvu ili aweze kuendelea na majukumu yake ya kuiongoza nchi kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

 

NDUGU WANAHARAKATI,

Pia, nitakuwa mchoyo wa shukurani ikiwa sitowashukuru waandaaji wa shughuli hii, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakiongozwa na Waziri Jembe, Mhe Riziki Pembe Juma, chini ya usimamizi wake na utoaji wa maelekezo yaliyowezesha kutekelezwa na leo hii tunashuhudia mageuzi yaliyopo katika maadhimisho haya. Sambamba na Kumshukuru Naibu waziri wake Mhe.Anna Athanas Paul, Kaimu Katibu Mkuu pamoja na kuwashukuru wakurugezi wote Kwa  ushirikiano wao bila ya kuwasahau Wakuu wa Divisheni zilizopo ndani ya Wizara na nje ya Wizara ambazo zimewezesha kukamilisha shughuli hii, niseme Hongereni sana na ninakushukuruni kwa kuniheshimisha mimi leo hii kuwa mgeni rasmi katika siku hii maalumu ya uzinduzi wa siku 16 za harakati za kupinga ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, sina zaidi ya kusema Ahsanteni sana.



Aidha, napenda kulishukuru Shirika la UN WOMEN na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Dunia (UNFPA) kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano ya kuondoa na kutomeza tatizo la Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia. Bila ya kusahau wadau wengine wote ambao sikuwataja ila ninatambua na kuthamini mchango wenu katika harakati za mapambano haya.

NDUGU WANAHARAKATI  

Chimbuko la siku 16 za wanaharakati za kupinga vitendo vya Ukatili na udhalilishaji wa Kijinsia ni kampeni ya ulimwenguni kote  ambayo chimbuko lake linatokanana na mkutano wa wanaharakati dhidi ya udhalilishaji wa kijinsia uliofanyika mjini Bogota Colombia America ya kati tarehe 18 – 21 November 1991  kwa kubadilishana mawazo juu ya kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia duniani.  Mkutano huo uliazimia  na kuchagua siku 16 kuanzia tarehe 25/ Novemba ambayo ni siku ya Kimataifa dhidi ya vitendo vya ukatili na  udhalilishaji na  hadi tarehe 10 Disemba  ambayo ni siku ya kimataifa ya haki za binaadamu kwa lengo la kuhusisha  masuala ya ukatili na masuala ya haki za binaadamu.  

NDUGU WANAHARAKATI  



Mwaka 1999 Umoja wa Mataifa uliridhia na kutangaza kuwa siku 16 za wanaharakati za kupinga ukatili na udhalilishaji wa kijinsia. Kwa  hapa kwetu Zanzibar harakati hizi zilianzia mwaka 2011 na kuendelea hadi leo kwa kufanya shughuli mbali mbali.

Lengo la maadhimisho  haya ni kutathmini juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na wadau katika kupambana na  vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, kuhamasisha wadau na jamii kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivi  na kupanga mikakati mipya ya kupambana  na kadhia hii.

Ni furaha kubwa kwa Zanzibar kuona kwamba siku ya leo tunaungana na nchi nyengine  duniani katika kuiadhimisha siku hii ikiwa na kauli mbinu isemayo “Kuelekea 2030 : Tuungane kutafakari na kuchukua hatua kumaliza udhalilishaji dhidi ya Wanawake na Watoto Zanzibar”.    

Ujumbe  wetu huu  unasisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano na kutafakari kwa pamoja kwa kuangalia visababishi, vichocheo na hatua za kuchukua kwa kuzingatia matokeo yenye tija na maendeleo kwa maslahi ya jamii yetu na kizazi chetu. Lengo ni kuendelea kuishi bila ya kuathiriwa na vitendo vya udhalilishaji katika ngazi zote za Kijamii, Kiutawala na Kisiasa.

 Dhamira ya siku hii kwa leo ni kuwaleta pamoja wanaharakati, wataalamu wa masuala ya Kijamii, wachumi, wanasiasa, viongozi wa dini wa Zanzibar na wanazuoni wengine katika  kuweka mikakakti na kuimarisha kazi zao katika kukuza mwitiko wa kushughulikia vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia. Na tumelenga kuwaleta watoa huduma na wataka huduma pamoja ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa na huduma za msingi za kujikinga na kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo la vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia.   

Aidha, inaweza kuchochea uwepo wa usawa wa Kijinsia na kuimarisha uwajibikaji kwa wote katika kutokomeza vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia na kuondoa dhana potofu dhidi ya watoto.

 


NDUGU WANAHARAKATI,  

Katika kuhakikisha kuwa changamoto ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia vinapatiwa ufumbuzi Serikali imekuwa ikiendelea na jukumu la kuratibu zoezi hili pamoja na kutoa elimu katika jamii na taasisi mbalimbali ikiwemo Skuli na Madrsa. Lengo ni kuiwezesha jamii kutambua njia na mbinu za kukabiliana na janga hili. Nimeelezwa hapa kwamba, WMJJWW Kwa kipindi cha mwaka mmoja 2023/2024 imeweza kuzifikia jumla ya skuli zipatazo 654 na madrasa 274 katika kupatiwa elimu Wanafunzi na Walimu wa taasisi hizo. Pia baadhi ya shehia zimeweza kufikiwa katika wilaya zote 11 za Zanzibar. Aidha, jambo kubwa la kuzingatia ni uwajibikaji, uthubutu, utekelezaji na kuondoa muhali katika kusimamia masuala ya upatikanaji wa haki.

 

NDUGU WANAHARAKATI,

Sote tunafahamu kwamba Nchi yetu iliandaa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kupambana na vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto kwa mwaka 2017/2022, ambapo tokea tumetekeleza mpango huo sasa ni miaka mitano imekamilika. Wizara WMJJWW imefanya tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi huo na kubaini kwamba yapo mafanikio kadhaa ambayo yamepatikana ikiwemo kukuza uelewa kwa jamii juu ya namna ya kujikinga, utumiaji wa rasilimali watu na fedha katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia, uratibu na usimamizi wa mpango kazi na kamati za kitaalamu, Wilaya hadi Shehia. Hata hivyo bado tathmini hiyo imebaini mapungufu kadhaa ambayo ni uwajibikaji mdogo kwa kamati za kupambana na udhalilishaji za ngazi ya Shehia, uelewa mdogo kwa wasimamizi wa Kamati za Shehia na utegemezi katika uendeshaji wa shughuli za mapambano ya kupinga vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia hapa nchini.

Ni jukumu letu sote kutafakari njia na mbinu stahiki za kupambana na matukio ya Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto kwa kuangalia sababu na maeneo hatarishi ambayo ndio vyanzo vikuu vinavyopelekea kutokea kwa matukio ya udhalilishaji na kuweka kwa mikakati imara ya kuondoa vikwazo hivyo kwani kwa pamoja tunaweza katika kutimiza wajibu wetu.

 

NDUGU WANAHARAKATI,  

Jukumu la mapambano ni letu sote na halihitaji kuelezwa mwenyewe ni nani bali kila mmoja kwa nafasi yake anaweza kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia miongozo, taratibu na kanuni elekezi katika kuliendea hilo. Miongoni mwa majukumu makubwa na ya msingi ni kutoa elimu, kuhamisha mila zilizo bora na zenye tija kwa kuzingatia utamaduni na silka zetu kama Jamii ya Kizanzibar na Tanzania kwa ujumla.

 

NDUGU WANAHARAKATI,

Takwimu zinaonesha kwamba kwa mwaka 2023 jumla ya matukio 1,954 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa ambapo waathirika walikuwa 1,959. Waathirika wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 83.7, wanawake asilimia 12.0 na wanaume asilimia 4.3. Miongoni mwa watoto waathirika; wasichana walikuwa 1,263 sawa na (asilimia 77.1) na wavulana walikuwa 376 sawa na (asilimia 22.9).

Jumla ya watu 13 wenye ulemavu wamefanyiwa ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kwa mwaka 2023. Ambapo wanawake walikuwa sita (6), wanaume wawili (2),wasichana wanne (4) na mvulana mmoja (1).

Kwa mwaka 2024, kwa kuanzia Julai Jumla ya matukio 165 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa, ambapo waathirika walikuwa 165, ikiwa Waathirika wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 86.1, wanawake asilimia 10.9 na wanaume asilimia 3.0.Miongoni mwa watoto ambao wameathirika 142 wasichana walikuwa 115 sawa na asilimia 11.0 na wavulana walikuwa 27 sawa na asilimia 19.0.

Matukio ya udhalilishaji kwa mwezi Agosti yalikuwa ni 157 ambapo waathirika walikuwa 157 waathirika wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 87.2 wanawake asilimia 11.5 na wanaume asilimia 1.3. Miongoni mwa waathirika watoto ni 137 wasichana walikuwa 112 sawa na asilimia 81.8 na wavulana walikuwa 25 sawa na asilimia18.2

Katika mwezi Septemba 2024  jumla ya matukio 148 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa Waathirika wengi walikuwa watoto kuanzia kuzaliwa hadi miaka 17 sawa na asilimia 87.9, Wanawake miaka 18 na zaidi sawa na asilimia 7.4 na Wanaume kuanzia miaka 18 na kuendelea sawa na asilimia 4.7, miongoni mwa watoto waathirika 130 Wasichana walikuwa 107 sawa na asilimia 82.3 na wavulana walikuwa 23 sawa na asilimia 17.7.

Takwimu hizi zinaonesha kuwa bado matukio ya Udhalilishaji yanawaathiri watoto wetu kike kwa kiume na wanawake kwa mujibu wa toleo la Takwimu za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar, hali hii inatupasa tuongeze kasi ya kupambana na vitendo hivyo kwa nguvu zetu zote  ili tuweze kuyatokomeza kabisa matendo hayo thakili ndani ya jamii zetu.

NDUGU WANAHARAKATI,  

Natambua kazi inayofanywa na Wanaharakati na wanazuoni wakiwemo Viongozi wa dini ambao ni muhimili mmoja wa wanajamii katika kusimamia uamrishaji mema na kukataza maovu ndani ya jamii, ninawashukuru sana kwa kutekeleza jukumu hilo na kuisaidia Serikali katika kukamilisha na kuyafikia malengo yake. Napenda kuwasisitiza kuwa fursa mliyoipata ya kushajiisha jamii yetu iondokane na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa Kijinsia itumieni vyema kwani mafanikio yatakayopatikana  ni yetu sote na kizazi chetu cha sasa na baadae.

NDUGU WANAHARAKATI,  

Pamoja na juhudi nyingi zinazochukuliwa na Serikali na Taasisi zisizo za Kiserikali, bado vitendo vya udhalilishaji vinaendelea. Jamii bado haijashajiika na kufahamu athari ya vitendo hivi na badala yake inaendeleza rushwa na  muhali.   

Hivyo, ni jukumu letu sote kuendeleza kutoa taaluma ya athari za vitendo hivi ili jamii ipate uelewa  wa kina kuhusiana na ubaya wa vitendo hivyo.  

NDUGU WANAHARAKATI,  

Kwa leo itoshe niliyoyasema ni jukumu letu sote  kuyatafakari na kuyafanyia kazi, tukiwa na wajibu mkubwa wa kuitumikia Jamii yetu kwa vitendo.

NDUGU WANAHARAKATI,  

Naomba nimalizie hotuba yangu kwa kuwashukuru wadau wetu wote ambao wamekuwa wakiiunga mkono Serikali yetu kwenye mapambano haya ya kupinga vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Pia, nikushuruni nyote kwa ushiriki wenu na kukubali kuwa mabalozi kwa niaba ya wananchi wengine na viongozi wengine kwa kuamua kuja kuitikia wito wetu. Bila kuwasahau waratibu wetu wa wanawake na watoto wa shehia kwa kujitolea kwenu katika mapambano haya. Serikali ya Dr Mwinyi iko pamoja nanyi kuhakikisha yale maslahi yenu kama yalivyoahidiwa na mhe Waziri wenu wakati wa usomaji wa bajeti yanazingatiwa vizuri. Na Ukizingatia mimi nilie hapa mbele yenu ndie waziri mwenye dhamana ya kusimamia fedha zetu, nitahakikisha hilo linafanikiwa vizuri.

Mwisho lakini si kwa umuhimu niiombe wizara kuharakisha mchakato wa mapitio ya sheria ya Mtoto, mpango wa udhalilishaji, majukwaa ya wanawake na yote yanayopaswa kuja katika ngazi za maamuzi yaharakishwe ili tuweze kuyapitisha na nyenzo hizi zifanye kazi yake. Naomba mtambue pia mm ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wawakilishi Wanawake wa Baraza la Wawakilishi ambapo sharia na kanuni zote tunazipitisha ndani ya Baraza, tupo mkao wa kula kuzisubiri hizo sharia ili tuweze kuzipitisha. Na niendelee kuwaomba wadau wote kuendelea kuziunga mkono juhudi za Dr Hussein Mwinyi katika kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunapambana kutokomeza  vitendo vyote vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia

 

Sasa naomba niseme kwamba Uzinduzi wa Siku 16 za Harakati za Kupinga Vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kwa mwaka 2024 nimezizindua rasmi. Na  sasa nipo tayari kwenda kufungua Maonesho ya Watoa Huduma.

                AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.

Comments

BLOG'S VISITORS

DAKTARI MWENGINE CHAKE CHAKE KULA SIKUKUU POLISI, NI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MGONJWA WAKE

NA WAANDISHI WETU, PEMBA::: DAKTARI anaetoa huduma kwa wagonjwa kituo cha afya cha serikali cha  Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, Is-haka Rashid Hadid, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16, mkaazi wa Gombani. Daktari huyo miaka 35 ni mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani. Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa, April 21 mwaka huu alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu. Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms) kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo alizikosa hospitalini hapo. "Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele katika sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje da...

'MKAPA' NA WENZAKE PEMBA WALAZWA RUMANDE

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ MAHKAMA kuu Zanzibar kisiwani Pemba, chini ya Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, imewapeleka rumande watumuhimwa wanne wanaokabiliwa na tuhuma za kuua kwa makusudi, akiwemo Ali Mussa Omar ‘ Mkapa’ mkaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake Pemba. Watuhumiwa wengine walioanza maisha mapya ya rumande ni mtuhumiwa Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari Mussa Omar miaka 30 pamoja na mtuhumiwa Yassir Mussa Omar ‘ Makababu ’ miaka 29, wote wakaazi wa shehia ya Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba. Awali watuhumiwa hao waliwasili mahakamani hapo, kwa mara ya kwanza, kwa ajili ya kusomewa tuhma zinazowakabili za kumuua kwa maksudi Said Seif Kombo. Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Seif Mohamed Khamis akiambatana na mwenzake Mussa Khamis Ali kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaia kufanya mauwaji hayo kwa maksudi. Ilidai kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo Oktoba 16, mwaka huu, baina ya saa 7:00 m...

HII KALI MBUNGE ASIYA AMKOGESHA MWANANCHI HADHARANI KISA HICHI HAPA......

  NA HAJI NASSOR, PEMBA MBUNGE wa viti maalum nafasi za wanawake mkoa wa kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka wananchi wa kijiji cha taifu, shehia ya Kinyasini jimbo la Gando wilaya ya Wete Pemba, kuyalinda miundombinu ya maji safi na salama, ili yawe endelevu kwao. Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kuwasili kijijini humo, na kumkogesha mwananchi mmoja kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama, ulioasisiwa na mbunge wa Jimbo la Gando. Alisema, hawana mbadala kwa sasa bali ni kuilinda miundombinu ya huduma hiyo, hasa baada ya mbunge wa wao Salim Mussa Omar, kuwarejeshea huduma hiyo. Alieleza kuwa, inafahamika kuwa kwa miaka 14 waliikosa huduma hiyo hasa kwa vile viongozi waliokuwepo hawakujali kuwatatulia tatizo hilo, hadi juzi ilipofanywa na mbunge wao. “Baada ya huduma hii sasa kurejeshwa na mbunge wa jimbo la Gando, kazi iliyobakia kwenu wananchi ni kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii,’...

TUHMA ZA DAKTARI PEMBA KUCHIWA HURU: POLISI KASKAZINI KUTOA TAARIFA RASMI LEO

  NA HAJI NASSOR, PEMBA KAMANDA wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, amesema leo Mei 9, mwaka huu atatoa taarifa rasmi, juu ya kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana ya Polisi, daktari wa Kituo cha Afya Gombani Is-haka Rashid Hadid, anayetuhumiwa kwa ubakaji. Alisema, kwa vile alikuwa katika mapumziko mafupi, haelewi jambo lolote linaloendelea kwa mtuhumiwa huyo, juu ya kuendelea kushikiliwa kwake kituoni hapo. Alieleza kuwa, leo Mei 6 (jana), hajapata taarifa za ndani za mtuhumiwa, huyo na kuwataka wananchi na wanaharakati, wasubirie hadi Jumatatu ijayo. Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Kamanda huyo, alisema hana taarifa zozote za kupewa dhamana mtuhumiwa ndani ya kituo chake cha Polisi au kuendelea kuwepo. ‘’Ilikuwa mimi sipo kazini kwa muda, kuanzia anakamatwa hadi anafikishwa Polisi, kwa sasa siwezi kueleza jambo lolote kwa mtuhumiwa huyo, hadi Jumatatu,’’alieleza. Aidha Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa sasa hawezi kutoa uf...

…….SUZA WATOA USHAURI WA ADHABU YA KUNYONGWA

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ WANAFUNZI wanaosomea uwalimu Chuo cha taifa cha Zanzibar ‘SUZA’ kampasi ya Benjamin Wiliam Mkapa Wete Pemba, wamependekeza adhabu ya kunyongwa hadi kufa, kwa mtu atakaetiwa hatiani, kwa kosa la dawa za kulevya. Walisema, haiingii akili kuona, mahkama imeshamtia hatiani mtu kwa kukutwa na dawa za kulevya, ambazo huathiri nguvu kazi ya taifa na kisha, kupewa hukumu ya kifungo pekee. Wakizungumza leo Juni 26, 2024 kwenye kongamano la vyuo vikuu, juu ya masuala ya msaada wa kisheria, kuelekea wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar, lililofanyika Chuoni hapo, walisema wakati umefika sasa kutolewa kwa hukumu hiyo. Walipendekeza kuwa, ni vyema kwa mtu anayetiwa hatiani asibakie chuo cha Mafunzo pekee kuitia tena hasara serikali kwa chakula na wakati mwingine matibabu, wakati tayari ameshasababisha madhara, kwa vijana. Mshiriki Juma Nafasi Juma, alifafanua kuwa kama mtu ameamua kuliumiza taifa kwa kuingiza, kusafirisha, kusambaaza dawa za kulevya, hivyo n...