NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WIZARA ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Pemba, imewatoa hofu wananchi wanaodhani kuwa, barabara zaidi ya kilomita 134, za vijijini zinazojengwa, kwamba hazitowekwa lami, na kusema kuwa jambo hilo sio sahihi.
Wizara hiyo imesema, kwa azma ya serikali inayoongozwa na Dk. Mwinyi kupitia wizara hiyo, ni kuusuka kwa lami mtandao wa barabara zote zilizoingia vijijini, ili wananchi wazitumie kwa kipindi chote cha mwaka.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Novemba 28, 2024, Afisa Mdhamini wa wizara hiyo Pemba, Ibrahim Saleh Juma, alisema barabara zote, zinazoendelea na zitakazojengwa, zitawekewa lami, kama ilivyoa ahadi ya Rais wa Zanzibar.
Alieleza kuwa, ujenzi huo ni maalum, kwa ajili ya kuwapa miundombinu ya uhakika wa barabara wananchi na hasa wakulima wanaoishi vijijini.
Alifahamisha kuwa, kwa muda mrefu wananchi walikuwa wakipata usumbufu, kuanzia usafiri wao hadi mazao wanayoyasafirisha, kwenda sokoni.
‘’Ujenzi wa barabara zinazoendelea hapa kisiwani Pemba kuanzia zile za vijijini, lengo hasa ni kuziwekea lami, ili ziwe za kudumu kwa muda mrefu,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine Afisa Mdhamini huyo, alisema serikali ya awamu ya nane, imepania kuona ndani ya kisiwa cha Pemba, hakuna tena kijiji chanye shinda ya barabara.
‘’Unajua kasi ya Dk. Mwinyi ni ya mfano wa pekee, maana kati ya zile kilomita 275 za kwa Zanzibar, nasi Pemba kwa awamu ya kwanza, tunakilomita 134, ambazo kazi inaendelea kwa kasi,’’alieleza.
Hata hivyo, aliwapongeza wananchi walioridhia kutokupokea fidia kwa vipando vyao, wakati huu ujenzi wa barabara hizo za ndani, ukiendelea.
‘’Kuhusu fidia za nyumba, kila mwananchi aliyeguswa ama kuhaharibiwa mpango wa kulipwa fidia upo, ingawa kwenye vipando, wananchi walisharidhia kupitia mikutano yetu ya awali,’’alifafanua.
Wakati huo huo, aliwataka wananchi wanaoishi karibu na ujenzi wa barabara hizo, kuendelea kushirikiana na wajenzi, ili kuhakikisha kazi inakwenda kama ilivyopangwa.
Baadhi ya wananchi, walisema kazi ya ujenzi wa barabara hizo utakapomalizika, utakuwa msaada mkubwa kwao, ikiwemo kurahisisha usafiri na usafirishaji.
Mayasa Himid Mcha wa Likoni Kengeja, alisema walikaa kwa zaidi ya miaka 60, bila ya kijiji chao kuwa na barabara ya kisasa.
Nae Asha Haidar Mohamed wa Kiuyu, alisema barabara wanayoitumia kwenda kwa shughuli zao maisha, ilikuwa inachangamoto hasa za mvua.
Kwa upande wao wafanyabiashara Mkubwa Hasnuu Omar na Mcha Othman Juma wa Matale walisema, sasa watasafirisha biadhaa zao kwa salama.
‘’Kwa hakika mpango wa Dk. Mwinyi wa kuzijenga barabara hizi kwa kiwango cha lami, umetusaidia maana ilikuwa ni vigumu hadi kuifikia barabara kuu,’’walisema.
Zanzibar inamtandao wa barabara usiozidi kilomita 1, 344, na wakati anagia madarakani Dk. Mwinyi, kulikuwa na wastani wa asilimi 40 ya barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami, na asilimia 60, zilikuwa na kifusi na udongo.
Barabara ambazo zimeshakamilika kwa hatua za awali na kusubiri zoezi la uwekaji lami ni pamoja na ya Finya- Kicha kilomita 8.6, Micheweni-Kiuyu Mbuyuni kilomita 7.5.
Nyingine ni Micheweni- Shumba mjini -bandarini kilomita 3.5, Mapofu- bandarini Tumbe kilomita 12.7, Chanjamjawiri-Matale- Pujini kilomita 4.6, Ukutini- Mtangani bandarini kilomita 4, Mgagadu- Kwa utawa kilomita 5.6, Polisi Kengeja, kupitia Likoni hadi Kiimbini kilomita 4.4.
Mwisho
Comments
Post a Comment