NA NUSURA SHAABAN, ZANZIBAR@@@@
KATIKA dunia ya leo, umuhimu wa kuwaandaa watotowa kike kuwa viongozi wa kesho hauwezi kupuuzwa, Skulini ndiko safari ya uongozi huanzia, na hapa Zanzibar, skuli kama Memon Academy na Skuli ya Sekondari Benmbella zinachukua hatua kubwa kuhakikisha watoto wa kike wanapewa fursa ya kujifunza na kuongoza.
Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar 2050, unasimama kama nguzo muhimu ya kuendeleza vijana, hasa wasichana, kwa kuwaandaa kushika nafasi za uongozi wa siku zijazo.
Mpango huu umejikita katika kukuza elimu na ustawi wa vijana,ambapo mbali na mpango huo, kuna na Sheria ya mtoto ya Zanzibar ya mwaka 2011, inayolenga kulinda haki za watoto, ikiwa ni pamoja na haki ya kupata elimu na fursa sawa za maendeleo ya uongozi.
Kwa kupitia sheria hiyo tunashuhudia namna watoto wa kike wanavyopata fursa mbalimbali za kielimu, ikiwemo majukumu ya uongozi kwa nafasi za mawaziri wa darasa, viongozi wa michezo, na wakuu waklabu. Hiyo ni sehemu ya mchakato wakuwajengea uwezo wakiakili na kiroho wakuwa viongozi wa kesho.
Kwa mujibu wa takwimu za UNICEF (2018), asilimia 60 ya wasichana walioko kwenye program za uongozi skulini wameonyesha kuboresha ujuzi wa mawasiliano, ushirikiano, na uwezo wakufanya maamuzi.
Aidha, ripoti ya UN Women (2020) inabainisha kuwa 50% ya watoto walioshiriki katika program za uongozi wamepiga hatua kubwa katika kujenga ujasiri na kushiriki katika majadiliano ya kijamii.
Hayo ni mafanikio yanayothibitisha umuhimu wa kuwaandaa watoto wa kike kuwa viongozi wakiwa bado skulini.
Uongozi wa Wanafunzi wa Kike: Mfano wa Skuli ya Benmbella na Memon
Maryam Hassan Kassim, Rais wa Serikali ya Wanafunzi katika Skuli ya Sekondari ya Benmbella, anaongoza wanafunzi 870 Skulini hapo, anakiri changamoto za uongozi lakini anamtazamo chanya.
"Uongozi wa wanafunzi si mdogo. Ni daraja kuelekea kuwa kiongozi wataifa. Mimi nataka kuwa Rais wa pili wa kike wa Tanzania," alisema Maryam.
Katika nafasi ya Waziri wa Mazingira, Nasra Hatibu Abdalla, ni mwanafunzi wa kidato cha sita Skuli ya Sekondari ya Benmbella, anaeleza kuwa kiongozi mwanamke kama Rais Samia Suluhu Hassan ni chachu ya kutokata tamaa licha ya changamoto anazo kutana nazo.
Hali hiyo inaungwa mkono na Twalaa Kassim Suleiman, Makamu wa Rais wa Skuli hiyo kwasababu anasema "Huwezi ukawa kiongozi na watu wote wakakukubali, lakini changamoto hizi ndizo zinazotufanya kuwa na nguvu."
Kwa upande wake mwanafunzi Sabra Salum Omar, yeye ni Rais wa Skuli ya Memon Academy iliyopo Hurumzi Mjimkongwe Mjini Zanzibar, anaongoza Wanafunzi 499, miongoni mwao Wanawake ni 262 na Wanaume ni 237, anasema, “Wanawake tunapaswa kujiamini. Tukiamua tunaweza kufikia malengo yetu ya kuongoza nchi yetu."
Walimu waskuli hiyo wanatumia mbinu kama kuunda klabu za uongozi na serikali za wanafunzi kuhamasisha wasichana kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi.
Mchango wa Walimu Katika Kuandaa Viongozi wa Baadaye
Mwalimu Nihifadhi Juma Hamad wa Skuli ya Memon anasema, "Tunawaandaa wanafunzi kupitia serikali ya wanafunzi, klabu za uongozi, na kuwashirikisha watoto wa kike katika majukumu mbalimbali."
Aidha, Mwalimu Masika Omar Salim anaongeza kuwa klabu za uongozi ni msingi wakuwajenga wasichana kujiamini na kuwa viongozi wa baadaye.
Kwa Skuli ya Benmbella, Mwalimu Bakari Mohammed anaeleza kuwa uchaguzi wa serikali za wanafunzi unawahamasisha watoto kujiamini. Rais wa wanafunzi huchagua baraza lake la mawaziri na kushiriki kikamilifu katika utawala wa shule.
Mtazamo wa Wazazi Katika Kukuza Viongozi wa Baadaye
Wazazi wana nafasi muhimu katika kuandaa watoto wa kike kuwa viongozi. Leyla Salum Juma, mzazi wa mwanafunzi wa Skuli ya Memon, anasema, "Watoto wasasa wanajitambua zaidi. Kama wazazi, ni jukumu letu kuwaunga mkono na kuhakikisha tunawapa matumaini katika ndoto zao."
Mwanakheri Mohamed Ali, mzazi mwingine, anahimiza wazazi kuwahoji watoto wao kuhusu ndoto zao za baadaye na kuwapa nafasi za kujifunza. "Watoto wote wanahitaji wasikilizwe. Tuwatie moyo katika malengo yao," alisema.
Jitihada za Serikali na Wizara ya Elimu
Afisa Elimu wa Wilaya ya Mjini, Hassan Abbass Hassan, anaeleza kuwa jitihada mbalimbali zinafanyika kupitia miongozo ya walimu na serikali za wanafunzi. "Hatujawahi kuwa na mwongozo rasmi wakukuza uongozi kwa watoto wa kike, lakini serikali za wanafunzi zimekuwa zikiwasaidia watoto kujifunza uongozi."
Suhuba Daud Issa, Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Wanafunzi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, anasema, "Tuna miradi kama Boys and Girls Science and Leadership Programme inayowawezesha watoto wa kike kuwa viongozi wa baadaye."
Hitimisho
Maandalizi ya watoto wa kike kuwa viongozi wa kesho yameonyesha mafanikio makubwa kupitia program mbalimbali shuleni, msaada wa walimu, na uungwaji mkono wa wazazi. Takwimu kutoka Global Partnership for Education zinaonyesha kuwa nchi zinazowekeza katika elimu ya watoto wa kike zina 70% ya uwezekano wakuwa na viongozi bora kwenye nafasi za kisiasa na kijamii katika siku zijazo.
Zanzibar ipo katika mwelekeo sahihi wakufanikisha mpango wake wa Maendeleo wa mwaka 2050, na jitihada hizi ni hatua muhimu kuelekea kujenga kizazi cha viongozi wa kike wenye maono na uwezo wakubadili jamii.
Comments
Post a Comment