NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
AFISA Mdhamini wizara ya Fedha na Mipango Pemba Abdul-wahab Said Abubakar, amezitaka asasi za kiraia Pemba, kuitumia ofisi yake, wakati wanapotaka kuandika miradi, ili kupata takwimu sahihi.
Alisema, ili waweze kupata andiko lenye mashiko la mradi, hawanabudi kuwa karibu mno na ofisi hiyo, ili kupata takwimu sahihi, zinazotambuliwa na mamlaka husika.
Afisa Mdhamini huyo aliyasema hayo, leo Novemba 24, 2024 ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake, alipokuwa akifungua mjadala kwa asasi za kiraia, juu ya changamoto za sekta zilizopo kisiwani Pemba zilizolalamikiwa kurudisha nyuma harakati za maendeleo kwa asasi na wananchi .
Alisema, asasi za kiraia zimekuwa ndio mdomo wa changamoto zilizopo ndani ya jamii, hivyo wakiitumia ofisi yake, wanaweza kupata takwimu zinazoweza, kupata mashiko ya hoja zao.
Alifahamisha kuwa, haiwezekani kwa asasi za kiraia, kukaa mbali na wizara ya Fedha, kwani imekuwa ndio eneo pekee lenye kukusanya kodi na takwimu nyingine za serikali.
‘’Nizitake asasi za kiraia Pemba, kuhakikisha wanafanyakazi kwa karibu na wizara ya Fedha, ili kupata takwimu sahihi zitakazo kuwa na mashiko, wakati wanapotetea au kuomba miradi,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Afisa Mdhaminu huyo wa Fedha na Mipango Pemba, alisema serikali inajali na kutambua kwa kiasi kikubwa, mchango wa asasi za kiraia katika maendeleo.
Mapema kwa upande wake Afisa Mdhamini wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, alizitaka asasi za kiraia, kuendelea kuwa mabalozi wa kulinda amani na utulivu hususan ni katika kundi la vijana kuelekea uchaguzi .
‘’Mwakani tunatarajia kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa vyama vingi, lazima asasi za kiraia, zitambue wajibu wa kulinda nchi na wananchi wake, na zisiwe sehemu ya machafuko hususan ni vijana ambao wao ndio hutumika vibaya mara nyingi,’’alieleza.
Akielezea mradi wa uraia wetu, Mratibu wa miradi kutoka Mwemvuli wa asasi za kiraia Pemba ‘PACSO’ Mohamed Najim Omar, alisema uraia wetu ni mradi wa kukuza mazingira wezeshi, kwa asasi za kiraia zenye uwezo wa kushiriki, katika utawala wa kidemokrasia nchini.
Mradi huo unaofadhiliwa na ‘the foundation for Civil society’ na kutekelezwa na ‘PACSO’ kwa Pemba na kituo cha majadiliano kwa vijana ‘CYD’.
Alieleza kuwa, mradi huo umegawika maeneo matatu makuu, ikiwemo ngazi ya kitaifa, taifa na utekelezaji kwenye makundi maalum, wakiwemo wanawake na vijana.
Kwa ngazi ya kitaifa, mradi unatekelezwa na asasi kadhaa ikiwemo Jukwaa la Katiba Tanzania ‘JUKATA’, Tanganyika law society kwa upande wa Tanzania bara na JUWAUZA kwa Zanzibar.
‘’Kupitia mradi huu, tayari tumeshakutana na makundi ya watu wenye ulemavu, wanawake, vijana, waandishi wa habari na maafisa wa serikali, nao waliibua changamoto zao za kisheria na kisera,’’alifafanua.
Akizungumzia lengo la mradi, Mratibu huyo alisema ni kuchangia kuwepo kwa mfumo wa sera na kisheria, ambao umeimarishwa na kuwezesha mazingira mazuri ya ushirikishwaji wa asasi za kiraia, kama watendaji wakuu wa utawala bora na demokrasia.
Katibu Mkuu wa ‘PACSO’ Sifuni Ali Haji, alisema lengo la mjadala huo, ni kuibua changamoto hizo na kuzifanyia kazi.
Alisema, ‘PACSO’ kwa sasa inaendelea na utekelezaji wa mradi wa urai wetu, ambapo moja ya eneo la utekelezaji wake, ni kuibua changamoto za kisheria na sera, zinazokwaza makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Akiwasilisha changamoto za kisera na sheria zilizowasilisha Novemba 3, mwaka huu mwanaharakati Juma Bakar Alawi, alisema moja ya changamoto hizo ni makampuni kutowapa mikataba watendaji wao.
Alisema jingine ni kuwepo kwa vifaa vya sayansi katika skuli za sekondari ambavyo vimeshapitiwa na muda wa matumizi, na kukosa kuteketezwa.
Mjadala huo, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ‘uraia wetu’ unaotekelezwa na ‘PACSO’ kwa muda wa miaka minne, kwa ufadhili wa ‘the foundation for civil society’ kupitia Umoja wa nchi za Ulaya ‘EU.’
Mwisho
Comments
Post a Comment