NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
JAMII imetakiwa kutoa ushirikiano kwa watu wenye ulemavu kwa kuwasaidia mambo wanayoyahitaji, ili kuweza kushiriki shughuli mbali mbali bila ya usumbufu.
Akizungumza na wananchi baada ya kumkabidhi kigari cha kutembelea Hijra Khalfan Hamad mwenye ulemavu wa viungo, Mkaguzi wa shehia ya Pandani Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi alisema, kila mmoja kwa nafasi yake ana wajibu wa kuwasaidia watu wenye ulemavu.
Alisema kuwa, watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo husababisha kukosa fursa ya kushiriki kwenye mambo yanayowahusu, jambo ambalo linawanyima furaha katika maisha yao.
"Katika kampeni yetu ya nyumba kwa nyumba ya Familia yangu haina uhalifu, tulimkuta mama huyu akatuelezea changamoto yake ya kukosa kigari cha kutembelea, niliona ni muhimu kwake na ndio maana nimekuja leo kumpeleka," alisema Mkaguzi huyo.
Alisema kuwa, Jeshi la Polisi limeamua kuweka wakaguzi kwenye shehia ili kusudi kuisaidia jamii kuishi katika hali ya amani na usalama, hivyo aliwashauri wakaguzi wenzake kwenye shehia zao kupiga mfano wake wa kuibua changamoto zinazowakabili wananchi na kutafuta njia bora ya kuzitatua.
"Katika jamii zetu kuna changamoto mbali mbali, za mtu mmoja mmoja na za jamii kwa ujumla, hivyo ikiwa tutachimba basi tunaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa," alisema Inspekta huyo.
Kwa upande wake mama huyo aliepewa kigari cha kutembelea mkaazi wa kijiji cha kwa Mwenyewe aliushukuru msaada huyo na kusema kuwa sasa ataweza kushiriki shughuli mbali mbali za kijamii ambazo zitafanyika kwenye shehia yake.
"Nimefurahi sana kwa sababu ilikuwa siwezi kutoka hata nje, sipati kuhudhuria mikutano wala shughuli nyengine ambazo zingeniwezesha kutoa malalamiko yangu ama ushauri, lakini sasa naamini na changamoto nyengine zitatatuka," alieleza.
Sheha wa shehia hiyo Khamis Rashid Ali alilishukuru Jeshi la Polisi kupitia Mkaguzi huyo ambae amekuwa akishirikiana na wananchi katika kusikiliza kero zao na kuzitafutia njia ya kuzitatua pamoja na kutokomeza uhalifu katika shehia.
"Kwa kiasi kikubwa shehia yetu imepunguza uhalifu na hii ni kutokana na ushirikiano kati yetu na Mkaguzi huyu kwa sababu muda wote anakuja kuwanasihi vijana na wananchi, hii ni faraja kwetu," alieleza sheha huyo.
Akizungumza kwa niaba ya familia yake, mwanafamilia Omar Abdalla Omar alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kusaidia kutatua changamoto ya mdogo wao, hali ambayo imewapa amani katika moyo wao.
MWISHO.
ReplyForward |
Comments
Post a Comment