NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
AFISA Miradi Mwandamizi kutoka shirika la ‘LSF’ ofisi ya Zanzibar Bakar Hamad, alisema wastani wa shilingi bilioni 5.1 zinaendelea kutumika kuanzia mwaka 2023, kwa ajili ya kusaidia msaada wa kisheria, kwa Tanzania bara na Zanzibar.
Alisema, kati ya fedha hizo, asilimia 30 zimeekezwa Unguja na Pemba, kupitia wasaidizi wa sheria na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar.
Hayo aliyasema hivi karibuni, wakati akitoa salamu za shirika hilo, kwenye siku ya kwanza ya jukwaa la nne la msaada wa kisheria Zanzibar, lililofanyika mjini Unguja.
Alisema, fedha hizo ambazo hutolewa kama ruzuku, zinalengo la kuimarisha msaada wa kisheria, ili haki iweze kupatikana kwa wnanachi, hasa wanyonge na wale wa makundi ya pembezoni.
Alieleza kuwa, kiasi hicho cha fedha kimeekezwa zaidi katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, elimu ya kisheria kwa jamii pamoja na kuwawezesha wanawake kwenye eneo la kiuchumi.
‘’Kupitia uwekezaji wa fedha hizo, LSF imesaidia kundi kubwa la wanawake kupata haki zao za ndoa, mirathi pamoja na migogoro mingine maarufu ndani ya jamii ya Zanzibar,’’alifafanua.
Alifahamisha kuwa, kwa kushirikiana na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria na wasaidizi wa sheria wa jumuia zao kwenye wilaya ya 11, wamefanikiwa kutatu migogoro 50,575 ya aina mbali mbali.
‘’Hii imefikiwa kutokana na ushiriki wetu wa ‘LSF’ wa moja kwa moja, katika kusaidia Idara husika pamoja na wasaidizi wa sheria kufika hadi vijijini ambapo, huwa ni changamoto kufika kirahisi,’’alifafanua.
Aidha Afisa huyo Miradi Mwandamizi wa LSF ofisi ya Zanzibar Bakar Hamad, alifahamisha kuwa, wapo wazanzibari 372,487 wamefikiwa na elimu ya kisheria, kupitia njia mbali mbali, ikiwemo elimu ya mikutano.
‘’Lakini hata kwenye kesi za udhalilishaji, nako tumepambania watu kupata haki zao, na kushughulikia matukio 10,553 yakiibuliwa na wasaidizi wa sheria wa Unguja na Pemba,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, alisema kuelekea mwaka 2025, na hasa wiki ya msaada wa kisheria, LSF haitoondosha ufadhili wake kwa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, pamoja na wasaidizi wa sheria, kutokana na uchapakazi wao.
‘’Jingine kubwa zaidi LSF, itakaa na Idara ili kuona, sasa wanasajili mwemvuli wa jumuiya za wasaidizi wa sheria Zanzibar (ZAPONET), na ndani yake kutakuwa na watendaji wakaoajiriwa ili, kuusimamia umoja huo,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, alisema kutokana na uchapakazi mkubwa wa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, umekuwa ukiwapa nguvu, LSF kuona ipo haja ya kuendelea kushirikiana.
Alieleza kuwa, Idara hiyo imekuwa ikitekeleza wajibu huo kwa kasi, na hawayaachi maagizo kweye makaratasi, kama ilivyo baadhi ya tasisi.
‘’Ufuatiliaji kwa karibu unaofanya na wenzetu hawa, umekuwa ikileta tija kwa wananchi wenyewe, ambao ndio walengwa wa kupatikana kwa haki,’’alieleza.
Awali jukwaa hilo lilifunguliwa na Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Haroun Ali Suleiman, ambae alisema anafurahisha, kuona serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinashirikiana katika kufanikisha utoaji wa msaada wa kisheria.
Mapema akiwasilisha maazimio ya jukwaa la tatu la msaada wa kisheria, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hajjat, Hanifa Ramadhan Said, alisema mingi yao yameshaanza kutekelezwa.
Moja wapo ni kwa skuli ya sheria Zanzibar kufanya marekebisho ya mitaala yao, jambo ambalo limeshanza kutekelezwa.
‘‘Lakini pia kulikuwa na wazo la kufutwa kwa ada kwa wasaidizi wa sheria, hili nalo limeshatekelezwa na tayari kwa mwaka huu wasadizi wa sheria hawakulipa,’’alifafanua.
Jukwaa la nne la msaada wa kisheria kwa mwaka huu 2024, kauli mbiu yake ni ‘ushawishi wa upatikanaji wa rasilimali za kuendeleza huduma za msaada wa kisheria Zanzibar’.
Mwisho
Comments
Post a Comment