Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto bi Abeida Rashid Aballah amesema mtoto Farhia Omar Mohamed (10) ambaye aliyekuwa anapigwa na mamaake wa kambo huko Bububu, Unguja hali yake inaendelea vizuri. Ameyasema hayo jana wakati alipomtembea mtoto huyo katika nyumba ya kulea watoto Mazizini, Unguja.
Bi Abeida amesema mtoto Farhia atapatiwa haki zake zote za msingi kama sheria ya mtoto inavyoeleza . Amefahamisha kwamba sheria ya mtoto sheria Na 2 ya mwaka 2011 imeainisha haki za mtoto ikiwemo haki ya kupata elimu, matibabu, kuishi, nk.
Ameeleza ni wajibu wa Wizara ya Maelendeleo ya Jamii , Jinsia , Wazee na Watoto kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo kwa maslah ya taifa.
Aidha katibu Mkuu Abeida ametoa wito kwa wazazi na walezi kutumia busara zaidi wakati wa kumuadhibu mtoto endapo amefanya kosa, kwani ikumbukwe kwamba mtoto ni wa Serikali hivyo, Serikali haitovumilia kuona mtoto anafanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa aina yeyote ikiwemo kupigwa, kunyanyaswa, kutelekezwa, n.k.
Mtoto Farhia Omar alichukuliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na kuhifadhiwa katika malezi bora, siku ya Jumapili, tarehe 11/02/2024
Comments
Post a Comment