NA MARYAM NASSOR, PEMBA@@@@
KESI ya kupatikana na dawa zinazoaminika kuwa
ni za kulevya, iliyopo mahakama kuu Zanzibar, kanda ya Pemba, imeshindwa
kuendelea, baada ya shahidi nambari moja, ambae ni Mkemia kushindwa kufika mahakamani hapo, kwa udhuru wa ugonjwa wa ‘RED EYES’.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo
kuwa, mtuhumiwa katika shauri hilo, Omar Khatibu Juma, alikutwa na misokoto 700
yanayosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya
aina ya bangi, yenye uzito wa gramu 2836.75, eneo la Machomane wilaya ya
Chake chake.
Mara baada ya kufika mahakamani hapo, mtuhumiwa akiwakilishwa na wakili
wake Zahran Mohamed Yussuf aliambiwa na
upande wa mashtaka ulioongozwa na Mwendesha mashtaka kutoka Afisi ya Mkurugenzi
wa mashtaka, Mohamed Ali Juma, kuwa walikuwa
wanategemea kupokea mashahid watatu.
Alidai kuwa,
kesi hiyo ipo kwa ajili ya kusikilizwa, na wamepokea mashahidi wawili, kati ya watatu
waliyoitwa, ingawa shahidi nambari moja ambae ni Mkemia, hajafika mahakamani
hapo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa macho mekundu.
Aliendelea kudai
kuwa, kutokana na aina ya kesi hiyo wanahitaji mtiririko mzuri wa mashahidi,
hivyo hawawezi kusikiliza shahidi wengine kabla ya kuanza na Mkemia.
‘’Mheshimiwa
leo (jana) kesi ipo kwa ajili ya kusikilizwa, ingawa shahidi nambari moja
hajafika mahakamani, hivyo tunaomba utupangie tarehe nyingine, kwa ajili ya
kusikiliza mashahidi,’’alidai.
Mara baada
ya kuusikiliza upande wa mashtaka, Jaji wa mahakama kuu Pemba, Ibrahim Mzee
Ibrahim, aliuliza upande wa utetezi kuwa wanasemaje kuhusu ombi la upande wa
mashtaka.
Nao, upande
wa utetezi ulikuwa ukiongozwa na mawakili Zahran Mohamed Yussuf na Massoud Juma
walidai kuwa, hawakubaliani na ombi hilo kutokana na kuwa, mteja wao ameshakaa
ndani muda mrefu na kuomna kusikilizwa kwa mashahidi waliofika mahakamani.
“Mheshimiwa
Jaji, kama ikikupendeza, basi tunaomba usikilize hao mashahidi wawili waliofika,
kutokana na kuwa mteja wangu yuko ndani mudaa mrefu,”alidai.
Alidai kuwa,
shauri hilo tokea lifunguliwe mahakamani hapo, linafika miezi sita na mtuhumiwa
yuko ndani, kama ikiwezekana basi wasikilizwe hao mashahidi waliyofika na isiwe
vyenginevyo.
Nae Jaji wa
mahakama hiyo, alimuliza wakili wa upande wa utetezi kuwa mteja wake, ana
shutumiwa na makosa mangapi, kwa sababu kama kosa ni kukutwa na bangi basi shahidi
nambari moja ni Mkemia.
Aidha
alisema, Mkemia ndie atakae thibitisha kuwa kile alichokiona ni bangi au laa na
hapo, ushahidi utakaofuata utakuwa unasaidia.
“Hatuwezi
kusikiliza shahidi wengine kabla ya Mkemia, kwa sababu ndie atakae thibitisha
hizi tuhuma ni za kweli au laa,”alisema.
Nao upande
wa utetezi kisha, ulikubaliana na hoja za Jaji huyo, na kisha kesi hiyo kughairishwa
hadi Machi 7 mwaka huu, ili kuendelea na ushahidi.
Ilidaiwa mahakamani
hapo kuwa, Julai 28, jana majira ya saa 4:00 za usiku eneo la Mkoroshoni,
katika wilaya ya Chake chake, bila ya halali
alipatikana na misokoto 700, ya dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya
aina ya bhangi, yenye uzito wa gramu 2836.75.
Hilo ni kosa
kinyume na kifungu cha 21 (1) (d) cha sheria za Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya Zanzibar, sheria namba 8
ya mwaka 2021 sheria za Zanzibar.
MWISHO
Comments
Post a Comment