NA ZUHRA JUMA, PEMBA@@@@
UONGOZI wa Kamati ya kutetea haki za watu wenye ulemavu shehia ya Shungi wilaya ya Chake chake Pemba, imesema wakati umefika sasa, kwa wanawake wenye ulemavu, nao kupewa nafasi za uongozi, kwani ni haki yao kikatiba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Katibu wa kamati hiyo, Asha Mohamed Yussuf, alisema bado wanawake wenye ulemavu, hawaonekani kuwa wanaweza kuongoza, jambo ambalo sio sahihi.
Alisema, kelele zinazopigwa juu ya wanawake na uongozi, hazijawangalia wanawake wenye ulemavu, jambo ambalo wao kama wanaharakati linawarejesha nyuma.
Alifafanua kuwa, wanawake wenye ulemavu wanauwezo mkubwa wa kuongoza iwe nafasi za usheha, kwenye vikundi vya kijamii, ukuu wa wilaya na hata ngazi ya urais, ingawa changamoto ni kukosa watetezi.
''Wanawake na wanaume wana haki sawa za kuongoza, lakini maandiko na maazimio kadhaa iwe ya kikanda na kimataifa, hajamuangalia mwanamke mwenye ulemavu,''alieleza.
Katika hatua nyingine, alisema kazi inayofanywa na TAMWA-Zanzibar ni nzuri, maana imekuwa ikiwashirikisha wanawake wenye ulemavu na wale wingine.
''Kwa mfano TAMWA imekuwa ikiwajengea uwezo waandishi wa habari, kuandaa makala na vipindi, ambavyo vinatugusa sisi watu wenye ulemavu, na kwa kiasi kikubwa sasa tunajua haki zetu,''alifafanua.
Aidha Katibu huyo, alisema changamoto kubwa kwa sasa inayowakabili ni baadhi ya wazazi, kutotoa ushirikiano wa karibu na kamati hiyo, wakati inapotekeleza wajibu wake kwa jamii.
Mapema Mwenyekiti wa kamati hiyo Khadija Mohamed Suleiman, alisema pamoja na changamoto hiyo, lakini wamefanikiwa kiasi, kuwaelezea wanawake wenye ulemavu, haki yao ya kuwa viongozi.
''Tumekuwa tukiwashajihisha wanawake wenye ulemavu, kwamba waombe nafasi za uongozi kuanzia kwenye vikundi, udiwani, uwakilishi na ubunge, kwani ni haki yao kikatiba,''alifafanua.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisema changamoto anayoiyona ni kuwa, bado jamii haijawaamini vya kutosha wanawake na hasa wenye ulemavu kushika nafasi za uongozi.
Amina Suleiman Juma wa kijiji cha Misooni shehiani humo, alisema wamekosa elimu ya kujengewa ujasiri, jambo ambalo wengi wao wanakosa umakini, katika kuomba nafasi za uongozi.
''Bado tupo baadhi yetu sisi wanawake, hutuna elimu ya ujasiri, kwanza kuomba na kisha kusimama mbele ya watu kusema jambo lolote,''alieleza.
Nae Mkali Juma Ali, wa kijiji cha Chanjamjawiri, alisema jamii itambue umuhimu wa uongozi kwa wanawake wenye ulemavu, kwani kila mmoja ana haki na wajibu huo kikatiba.
Nao Asma Said Abdalla, Sharifa Mohamed Khamis na Bimkubwa Othman Khamis, walisema wanajisikia faraja, kuwepo kwa kamati hiyo, kwani imekuwa msaada wa kuwaelimishana, juu ya haki zao.
Sheha wa shehia ya Shungi Hamad Ramadhan Soud, alisema kamati hiyo ilipata baraka zote za wananchi, hivyo hakuna budi kuiunga mkono, ili kufanikisha malengo yao.
‘’Kamati ipo
kwa ajali ya kushughulikia, kuibua na kufuatilia haki mbali mbali za watu wenye ulemamavu, sasa lazima sisi wananchi tuisaidie, ili ifikie malengo
yake,’’alieleza.
Mratibu wa TAMWA-Ofisi ya Pemba, Fat-hya Mussa Said, alisema ni vyema kwa waandishi wa habari, kuongeza kasi ya kutoa makala na vipindi, vyenye kuwasaidia wanawake wenye ulemvu kujua haki zao.
Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema wanawake wenye ulemavu wana haki sawa na wingine, iwe katika uongozi ama nafasi nyingine.
Mwisho
Comments
Post a Comment