WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar Ali Suleiman Ameir amewataka wananchi na wadau mbali mbali kutumia fursa ya kutoa maoni kwenye rasimu ya sera mpya ya mambo ya nje, ili kujenga sera madhubuti ambayo ni dira ya maendeleo itakayowanufaisha kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Akizungumza katika kongamano la kukusanya maoni kuhusu marekebisho ya sera hiyo ya mwaka 2001 alisema, Serikali imeelelekeza kushirikishwa wadau ili kuwezesha kupata sera madhubuti itakayoboresha.
Alisema kuwa, ni muhimu kwa wadau kuunda sera madhubuti ambayo italiwezesha Taifa hili kunufaika ipasavyo na kukuza ushirikiano baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mataifa mengine duniani.
"Tayari tumeshafanya makongamano haya katika mikoa mengine na sasa tunaendelea, haya yanalenga kupata sera yenye tija ambayo itakidhi matarajio ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alisema.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alisema kuwa, kupitia kongamano hilo, wataelewa masuala muhimu katika sera ya mambo ya nje, ikiwemo dhana ya uchumi wa buluu ambayo ni miongoni mwa mbinu za kukuza uchumi katika nchi.
Aidha alieleza kuwa, sera hiyo itatoka fursa kwa wakulima wa mwani na karafu kupanua wigo katika masoko duniani, kwa lengo la kupata tija zaidi ya bidhaa zao.
Nae Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa alisema, sera hiyo iliundwa mwaka 2001 na kuanzia kutumika mwaka 2004 ikiwa na lengo na kuimarisha ujirani mwema, ushirikiano wa kiuchumi, ushirikiano na nchi zinazoendelea, pamoja na umoja wa nchi za afrika.
Alisema kuwa, matarajio yao katika sera hiyo ni kuimarisha uchumi wa buluu, uratibu wa mikataba na kulinda mila zetu za kiafrika, hivyo kuna haja ya kutoa maoni kwenye rasimu ya sera hiyo ili kuimarisha zaidi.
Akiwasilisha mada Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora Jastin Kisoka alifahamisha kuwa, msingi wa sera hiyo ni kulinda uhuru, kukuza ushirikiano wa kiuchumi na washirika wa maendeleo, kuanzisha, kuendeleza na kulinda maslahi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa pamoja na kujenga uchumi endelevu.
Akielezea baadhi ya mafanikio alisema kuwa, ni kuimarisha ujirani mwema na ushirikiano wa uwili, ushirikiano wa kikanda na usuluhishi wa migogoro.
"Pia kuna baadhi ya changamoto ambazo zimetufanya tuje hapa kukusanya maoni yenu na kuziboresha, ikiwa ni pamoja na kutotumia ipasavyo lugha yetu, ukosefu wa miongozo ya kisera na kutokuwepo kwa ulinzi na usalama," alieleza.
Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvivi Zanzibar Dk. Abdul Suleiman Jumbe akiwasilisha dhana ya uchumi wa buluu alisema, rasimu hiyo imezingatia maeneo muhimu ya rasilimali za uchumi wa buluu ambazo wanaamini wataimarisha zaidi na kukuza uchumi wa wananchi na nchi kwa ujumla.
Waziri Mstaafu wa SMZ Mohamed Aboud Mohamed alisema, ni wajibu wa washiriki hao kutoa maoni ya kujenga ambayo yatakuwa na maslahi kwa Taifa lao, kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Matar Zahor Massoud alisema, aliwasisitiza wananchi kutoa maoni mbali mbali kuhusu sera hivyo kwa maslahi yao na Taifa.
Kwa upande wao washiriki wa mkutano huo waliomba, ulinzi na usalama uimarishwe mbali mbali ikiwemo mipakani kwani kuna madawa ya kulevya yanaingizwa siku hadi siku, ambayo yanawaathiri vijana wengi ambao ndio Taifa la leo.
Mshiriki kutoka Baraza la vijana Micheweni alisema kuwa, ni vyema sera hiyo ikazungumzia namna bora ya kutatua changamoto za kimaadili, kwani imekuwa ni kikwazo kikubwa katika nchi ya Tanzania.
Kongamano hilo la siku moja limefanyika katika viwanja vya kufurahishia watoto Tibirinzi Chake Chake Pemba.
MWISHO.
Comments
Post a Comment