NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
UONGOZI
wa shehia ya Shungi wilaya ya Chake chake Pemba, umewataka wananchi, ambao bado
hawajachimba mashimbo ya kuhifadhi maji taka, kufanya hivyo haraka, ili kuzuia uwezekano
wa kukumbwa na magonjwa ya mripuko.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi shehiani hapo, Sheha wa shehia hiyo Hamad Ramadhan
Soud, alisema shehia haitomvumilia mwananchi yeyote, anetiririshaji maja taka,
kwani athari yake inaweza kuenea kwa shehia nzima.
Alisema, kila
mwananchi ahakikishe amechimba shimo maalum na kisha kulifunika vyema, ili
kuhifadhi maji anayotumia kutoka nyumbani mwake, badala ya kuyaacha yasambae.
Alieleza kuwa,
maji yanayotumiwa hata kwa kukoshea vyombo au kukogea chooni, ndio chanzo cha
magonjwa kama matumbo ya kuharisha damu, kipindu pindu na minyoo.
‘’Niwatake
wananchi wangu, haraka sana wale ambao hawajachimba mashimo ya kuhifadhi maji
taka, kama vile yanayotiririka kutoka chooni, kufulia au hata ya kukoshea vyombo,
wachimbe ili kuzuia maradhi,’’alifafanua.
Katika hatua
nyingine, Sheha huyo amewataka wananchi, kuendelea kumpa taarifa pindi
wakibaini kuwepo kwa mwenzao, anayetiririshaji taka, ili hatua za kinidhamu
zichukuliwe.
Wakati huo
huo, amewaahidi wananachi kuendelea kuwasiliana na wataalamu wa afya, ili
kufika shehiani humo na kuwapa elimu juu ya namna bora ya kuyahifadhi maji
taka.
Mwananchi Asma Said Abdalla wa Chanjamjawiri,
alisema lazima elimu iongezwe kwa wale wachache wanaoendelea kudharua, juu ya
suala la uchimbaji mashimo ya kuhifadhi maji taka.
Kwa upande
wake, Mbarouk Idrissa Omar wa Misooni shehiani humo, alisema hata suala la faini
liweze kufanyakazi ikiwa, kuna mwananchi anashindwa kutekeleza agizo hilo.
Nao Asha
Suleiman Hamad na Amina Suleiman Juma wa kijiji hicho, walisema wengi wao wameitikia
wito wa uchimbaji mashimo, ingawa ni yale yanayojaa haraka.
‘’Kama kuna
mfadhili, ni vyema akajitokeza, ili tumshawishi kutuchimba shimo moja kubwa,
kwa kila baada ya nyumba tano hadi saba, ili kudhibiti maji hayo,’’walifafanua.
Mtaalamu wa
magonjwa ya binaadamu kutoka Manispaa ya Chake chake Abubakar Khatib Bakar, alisema
Manispaa hufanya mara kwa mara msako wa nyumba hadi nyumba, ili kuwabaini wananchi
wanotiririsha maji taka.
Alisema, kwa
sasa wamo kwenye mpango kabambe wa kuhakikisha ndani ya miaka 10 ijayo, hakuna
magonjwa ya mripuko, na sasa wameshatimiza miaka mitano, bila ya ugonjwa huo.
‘’Manispaa
ya Chake chake imejipanga, ili kuona ndani miaka 10 hakuna mgonjwa ya mripuko,
na ndio maana tukimgundua kwa mara ya kwanza, anapigwa faini ya shilingi 20,000
lakini mara ya pili anafikishwa mahkamani, na faini isiyopungua shilingi
250,000,’’alifafanua.
Hata hivyo,
amewakumbusha wananchi wanaonzisha ujenzi wa nyumba, kuhakikisha wanafanya kila
namna, ili kudhibiti maji taka, ambayo athari yake pia ni kusababisha ugonjwa
wa ngozi.
Shehia ya Shungi
iliyopo wilaya ya Chake chake Jimbo la Chonga, inao wananchi 3,884 ambapo
inaundwa na vijiji vya Missoni, Shungi, Kiziwani, Chanjamjawiri, inayomiundombinu
ya elimu, afya na barabara.
Mwisho
Comments
Post a Comment