Na Maulid Yussuf, Zanzibar
Mkurugenzi Idara ya
Mipango, Sera na Utafiti, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Bi Daima Mohamed Mkalimoto amesema hatua ya uanzishwaji wa Jukwaa la haki za watoto kwa wadau
wanayoshughulikia maendeleo ya watoto itasaidia kuweka pamoja na kuunganisha
shughuli za watoa huduma za watoto.
Amesema hayo jana katika
ukumbi wa UN Women wakati akifungua mkutano wa wadau wanaoshughulikia masuala
ya Watoto kutoka taasisi za umma, binafsi na Washirika wa Maendeleo, ambapo
mkutano huo ulilenga uanzishwaji wa Jukwaa la haki za Watoto Zanzibar.
Bi Daima amesema hatua
hiyo itasaidia kuwaweka pamoja wadau hao katika uratibu wa utekelezaji wa
shughuli zinazogusa Maendeleo ya watoto nchini. Hivyo amewaomba wadau hao kutoa
maoni yao ili yafanyiwe kazi na kuingizwa katika mapendekezo ya kuanzishwa kwa
jukwaa hilo.
“Kuna umuhimu wa uratibu na
usimamizi wa pamoja wa uanzishwaji wa jukwaa la haki ya watoto ili kuweza kutoa
huduma bora za watoto katika mazingira na hali tofauti” Alisema bi Daima.
Akiwasilisha mapendekezo
ya kuanzishwa kwa Jukwaa la haki ya watoto kwa wadau wanaoshughulikia Maendeleo
ya watoto Zanzibar, Mshauri elekezi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Watoto (UNICEF) na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania
Dkt. Ladislaus Batinoluho ameipongeza Serikali ya Zanzibar kupitia Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa hatua nzuri iliyofikia kutokana
na kazi kubwa wanayoifanya katika masuala mazima ya maendeleo ya watoto nchini.
Amesema pamoja na
mafanikio hayo, bado watoto wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo
utumikishwaji kwa watoto, kudhalilishwa, na kubakwa, hivyo wazo la UNICEF la
kuanzishwa Jukwaa hilo litasaidia kuleta nguvu za pamoja katika kumkomboa
mtoto.
Nao washiriki wa mkutano
huo, wameshauri kuanza taratibu za kuanzishwa Jukwaa hilo ni vyema kuwashirikisha
wadau na taasisi zote zinazoshughulikia watoto akiwemo Wizara ya Elimu, Wizara
ya Afya, n.k ili kufikia malengo ya
kuanzishwa kwa Jukwaa hilo la haki za watoto Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment