NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na
Mifugo Zanzibar, Shamata Shaame Khamis, amesema kukamilika kwa ofisi ya kisasa
ya elimu wilaya ya Mkoani Pemba, iwe chachu ya kuongeza ufaulu na ufuatiliaji
wa masomo, wilayani humo.
Waziri Shamata aliyasema hayo Disemba 2, 2024 mara baada ya
ufunguzi wa ofisi hiyo, ikiwa ni sehemu za shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi
Zanzibar ya mwaka 1964.
Alisema, tokea kufanyika kwa mapinduzi hayo, hakujawahi
kuwa na ofisi mpya na ya kisasa ya elimu ya wilaya, ambapo wakati huo watendaji
hao walikuwa wakifanyakazi katika mazingira magumu.
Alieleza kuwa, kama sasa imeshajengwa ofisi ya kisasa na
yenye vifaa vipya, iwe chachu ya kuongeza ufaulu na suala la ufuatiliaji wa
masomo kwa wilaya ya Mkoani.
‘’Leo (jana) tumeshaifunfua ofisi mpya na ya kisasa,
hivyo ni matumaini yangu kuwa, itakuwa chachu ya kuongeza ufaulu, lakini pia
suala la kufanya ufuatiliaji kwa skuli mbali mbali wilayani humo,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Waziri huyo, alisema suala la elimu
kabla ya mapinduzi ya Zanzibar, lilikuwa likolewa kwa ubaguzi, na mtoto wa mnyonge,
hakuwa na haki ya kupata elimu.
Alieleza kuwa, jambo hilo liliwakera mno waasisi wa taifa
hili, na ndio maana hatua zilichukuliwa, na kufanya mapinduzi ya Zanzibar mwaka
1964, ili kuondoa utawala wa kidhalimu.
‘’Tukiwa nashuhudia miundombinu ya kisasa ya elimu, tukumbuke
kuwa huko nyuma, wazazi wetu hawakupata haki hii, maana ilikuwa wanaosoma ni
watoto wa watawala pekee, leo tunashukuru,’’alifafanua.
Akizungumzia suala la miaka 60 ya mapinduzi Zanzibar,
Waziri huyo alisema kila mmoja, anayohaki ya kuyalinda, kuyaenzi kwani ndio mkombozi
wa maisha ya wazanzibari.
Mapema Katibu Mkuu wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar Khamis Abdalla Said, alisema ujenzi wa ofisi hiyo, walikabidhiwa na Halmashauri
ya wilaya ya Mkoani, ili kuendeleza ujenzi wake.
Alisema kuwa, kisha wizara iliridhia kukamlisha ujenzi huo,
ili watendaji wa wizara ya elimu ngazi ya wilaya, wapate ofisi ya kisasa ya
kuendesha shughuli zao.
Alieleza kuwa, walitumia shilingi milioni 182.882, kwa
ajili ya kukamilisha ujenzi huo pamoja na kazi nyingine, kama ya utiaji umeme,
maji, madirisha, milango, marekebisho ya maktaba, ujenzi wa ukuta pamoja na
rangi.
Katibu huyo alieleza kuwa, ndani ya ofisi hiyo
wameshaweka kompyuta za kisasa, mashine ya fotokopi ya kisasa yenye uwezo wa
kufanya muunganiko wa kutoa kopi.
Aidha alieleza kuwa, kazi hiyo ya ukamilishaji ujenzi
huo, imefanya na kampuni ya United Ram Construction, na kusimamiwa na mshauri
ambae ni kampuni ya kizalendo ya AE&Q.
‘’Kazi ya kukamilisha ujenzi huu, ulianza Septamba 2023,
na kumalika mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo ndani yake, mna vyumba vitano,
maktaba na vyoo pamoja na stoo,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo wa wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdulla Said, alisema ujenzi huo ni eneo
moja wapo, la utekelezaji wa mageuzi makubwa ya elimu, yalioridhiwa na serikali
ya awamu ya nane.
‘’Serikali, imedhamiria kuwa na ofisi ya elimu za wilaya
ya kisasa, na tayari tumeshajenga katika wilaya saba na nne zilizobakia ujenzi
utafanyika kabla ya mwaka 2025,’’alifafanua.
Wakati huo huo, aliwapongeza waalimu, wanafunzi na wazazi
wa wilaya ya Mkoani, kwa kuongoza katika mitihani ya taifa ya darasa la saba,
kufuatia matokeo yaliotolewa hivi karibuni.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mkoani Khatib Juma
Mjaja, alisema ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Dk. Mwinyi, wameshajengewa
madarasa 381 pamoja na ajira za waalimu 596 kwa wilaya za Chake chake na
Mkoani.
Hata hivyo, amewataka wazazi, walezi na waalimu kuendelea
kushirikiana, ili kuona watoto wanapata elimu katika mazingira rafiki, na hasa
baada ya kukamilika kwa ujenzi wa ofisi ya elimu ya wilaya ya Mkoani.
Naibu Waziri wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali
Abdull-ghulam Hussein, alitaka kuendelea kutunzwa kwa ofisi hiyo mpya na ya kisasa,
ili iwasaidie na wingine hapo badaae.
Shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zitaendelea
tena leo kwa uwekaji wa jiwe la msingi skuli ya Utaani Wete, ufunguzi wa kituo
cha afya cha mama na mtoto Tironi Mkoani na uzinduzi wa barabara ya Kijangwani-
Birikau wilaya ya Chake chake.
Mwisho
Comments
Post a Comment