NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
NAIBU Waziri Mkuu, ambae pia ni Waziri wa
Nishati wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Doto Mashaka Biteko, amesema
kitendo cha kufanyika kwa mapinduzi ya Zanzibar, kilikuwa chema, kwani
kililenga kuwapa uhuru wa wananchi, kusafiri nje ya mipaka kadiri wapendavyo.
Naibu Waziri huyo Mkuu, aliyasema hayo Disemba 6, mwaka 2024 uwanjwa wa Umoja
ni nguvu Mkoani Pemba, mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi, wa ofisi na
makaazi ya maafisa wa Uhamiaji, wilayani humo, ikiwa ni shamra shamra za miaka
60 ya mapinduzi.
Alisema, mapinduzi hayo, yalikuwa yanafaa mno kuona
wazanzibari na wananchi wote, wanatumia haki yao kwenda watakako kwa mujibu wa
sheria, uhuru ambao hawakuwa nayo, kabla ya mapinduzi.
Alieleza kuwa, mapinduzi hayo kupitia viongozi na wakuu
wa nchi tokea mwaka 1964 hadi leo, wanaendelea kusimamia haki hiyo, ili kuhakikisha
wananchi, wanasafiri zaidi nje ya mipaka ya Tanzania.
‘’Kila mmoja ni shahidi, baada ya kufanyika kwa mapinduzi
haya na kisha kuundwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, viongozi
waliendelea kusimamia masuala ya safari, chini ya idara ya safari na pasipoti,
ili kila mmoja kupata haki hiyo,’’alieleza.
Aidha Dk. Biteko alieleza kuwa, mapinduzi hayo si tu
kwamba yamempa uhuru mzanzibari, lakini yamemuonesha njia ya kufika mbali, kwa
ajili ya kiuchumi, ili kutatua changamoto zake.
Alieleza kuwa, matunda ya mapinduzi hayakuishia hapo,
kwani April 26, mwaka 1964 viongozi na waasisi wa mapinduzi hayo, akiwemo Rais
wa kwanza wa Zanzibar Abeid Amani Karume na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, waliziunganisha nchi, na kuzaliwa
Tanzania.
‘’Lengo la Muungano, pamoja na mambo mingine, lakini pia
ni kuimarisha huduma mbali mbali kwa wananchi, ikiwemo upatikanaji wa vibali
vya kusafiria nje ya nchi,’’alifafanua.
Aidha alieleza kuwa, huduma za uhamiaji kisha zilisambaa nchi
nzima, ambapo kwa wilaya ya Mkoani, zilianza mwaka 1979, ambapo ofisi yake,
haikukidhi vigezo kwa wakati uliopo.
‘’Leo tukiwa ndani ya miaka 60 ya mapinduzi, tumeanzisha
safari mpya kwa kuwa na ofisi ya kisasa na makaazi ya maafisa wa Uhamiaji hapa
wilaya ya Mkoani,’’alieleza.
Hivyo amewataka wananchi wa Zanzibar, kuendelea kuyaenzi,
kuyalinda na kuyaheshimu mapinduzi ya Zanzibar, ambayo matunda yake sasa,
yanaonekana kila sekta,
Wakati huo huo Naibu Waziri huyo Mkuu na Waziri wa Nishati
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Doto Mashaka Biteko, ameushauri uongozi
wa Idara ya Uhamiaji, kuiga aina ya ujenzi wa ofisi hiyo, ili kujenga nyingne
nchi nzima.
Mapema akisoma taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais, (sera, uratibu na Baraza la Wawakilishi), Zanzibar Seif
Islam Salum, alisema ujenzi huo, utakapokamilika utakuwa na makaazi ya maafisa
sita, pamoja na ofisi zenye huduma zote.
Alieleza kuwa, ujenzi huo ulianza mwezi August 2022,
ambapo ulitarajiwa kumalizika mwaka mmoja baadae, ingawa kwa sababu mbali mbali,
ulimalizika mwezi Disemba mwaka jana.
‘’Ujenzi wa jengo hili, kwa hakika unaakisi na fedha
ambazo zilitengwa kwa kazi hiyo, maana jengo limetimiza viwango vinavyotakiwa,’’aliafafanua.
Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Jumanne Sagini, alisema mapinduzi ya Zanzibar, ndani ya Idara ya Uhamiaji,
imeweka historia mpya, kwa ujenzi wa jengo hilo la ofisi na makaazi ya maafisa wa
Uhamiaji.
Hata hivyo, alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Samia Suluh Hassan, amekubali kutoa fedha za kuimarisha utendaji kazi
wa Idara ya uhamiaji, ikiwemo ujenzi wa ofisi za wilaya na mkoa nchi nzima.
‘’Na kwasasa, serikali imeridhia ajira 1,741 za Idara ya
Uhamiaji, pamoja na upandisha vyeo maafisa mbali mbali wa Uhamiaji 2,824 kwa nchi nzima,’’alifafanua.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania
Anna Peter Makakala, alisema Idara hiyo inaendelea kutekeleza maagizo ya
kiongozi wa nchi, ili kuona wanatoa huduma za kileo.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud,
alisema ujenzi wa ofisi hiyo na maakazi ya maafisa wa Uhamiaji, ni moja ya
matunda ya muungano, yalioasisiwa na mapinduzi.
Jengo hilo la ghorofa limegharimu shilingi bilioni 1.53, ambalo
lilikuwa na mkandarasi kampuni ya Bench Mark Engerneering na kusimamiwa na wakala
wa majengo Zanzibar ‘ZBA’
Mwisho
Comments
Post a Comment