DK. MWINYI AWEKA JIWE LA MSINGI NYUMBA ZA MADAKTARI MKOANI, AAHIDI UJENZI WA HOSPITAL YA RUFAA KILA MKOA
NA
HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema ujenzi wa nyumba za madaktari karibu na
hospitali, kutaondoa adha kwao na wagonjwa, kwa kumudu kutoa huduma saa 24.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo Disemba 3, mwaka 2024, uwanja wa mikutano
bandarini Mkoani, mara baada ya kuziwekea jiwe la msingi, nyumba za madaktari
zilizopo hospital ya Abdalla Mzee Mkoani Pemba, ikiwa ni shamra shamra za
kuelekea miaka 60 ya mapinduzi Zanzibar.
Alisema, nyumba hizo zitakapokamilika, zinatarajiwa
kuondoa usumbufu kwa madaktari hao na wagonjwa wanaokwenda hospitali, kwa kule kuwa
karibu na sehemu zao za kazi.
Alieleza kuwa, serikali pia itapunguza gharama za
kuwafuata madaktari kwenye maakazi yao ya uraiani, pale inapotokezea wagonjwa
wa dharura, hasa nyakati za usiku.
‘’Leo (jana) tumeshaziwekea jiwe la msingi nyumba za
madaktari wetu, ni matumaini yetu sasa huduma zote za kitabibu, zitapatikana
saa 24, kwa vile madaktari watakuwa wanaishi karibu na hospitali,’’alisema.
Aidha Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema ujenzi wa nyumba hizo ambao unafanywa
na serikali ya watu wa China, ni kuendeleza historia yao na Zanzibar.
Alieleza kuwa, ushirkiano huo ulianzia pale China, kwa kuwa
nchi ya kwanza kuyatambua mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, na kuanzia hapo,
walianza kuiunga mkono Zanzibar, hasa katika huduma za afya.
Alifafanua kuwa, kuanzia mwezi Aprili mwaka 1969,
serikali ya watu wa China, walijenga hospitali ya Abdalla Mzee iliyopo Mkoani,
na kuanza kutoa misaada na madaktari mbali mbali wa fani tofauti.
Alisema kuwa, katika kuendeleza dhamira yao hiyo, kisha
mwaka 2016, serikali hiyo ya Jamhuri ya watu wa China, iliifanyia ukarabati
mkubwa hospitali hiyo.
‘’Kutokana na vifaa na uwezo iliyonayo hospitali hiyo, na
msaada mkubwa wa wataalamu kutoka China, kwa sasa inatumika kama hospitali ya
rufaa, hapa kisiwani Pemba,’’alifafanua.
Aidha Dk. Mwinyi alieleza kuwa, msaada wa kuimarisha
huduma za matibabu hospitalini hapo, ulikuja tena mwezi Novemba mwaka 2021,
ambapo China, iliiahidi serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuifanyia ukarabati
wa baadhi ya maeneo na ujenzi wa nyumba za madaktari.
‘’Leo nimefurahishwa kujionea mwenyewe, mwenzetu hawa
wametekeleza kwa vitendo, kile waliochokiahidi na kuendeleza ushirikiano wa dhati,
uliopo miaka 54 iliyopita, kwa ujenzi wa nyumba hizi,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, Rais huyo wa Zanzibar, alisema
serikali kwa upande wake, itajenga nyumba nyingine za madaktari, katika
hospitali za wilaya za Kinyasini, Micheweni, Vitongoji kwa Pemba na Kitogani,
Pongwe, Panga tupu na Kivunge kwa Unguja.
Alifafanua kuwa, matayarisho ya ujenzi wa nyumba hizo
yameshaanza, na matarajio yake ni kuona, miradi hiyo inakamilika kwa wakati,
kama ilivyopangwa hapo awali.
Hata hivyo alisema, baada ya kukamilika kwa miradi hiyo,
itakuwa kumeendelezwa kwa vitendo, mafanikio ya sekta ya afya nchini, kwa kuondoa
kukosekana kwa madaktari, kutoa huduma za dharura.
Wakati huo huo, Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, akijibu maombi ya Mkuu wa mkoa wa
kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud, juu ya uwepo wa hospitali ya rufaa Pemba,
alisema matayarisho yake yameanza.
Alisema, serikali inampango wa kujenga hospitali ya moja
kila mkoa, ambayo itakuwa na hadhi, vifaa na wataalamu, ambapo kwa mkoa kwa kusini
Pemba, itajengwa Chake chake.
‘’Pamoja na kuwa na hospitali za rufaa za kila mkoa,
lakini serikali inatarajia kujenga hospitali nyingine ya rufaa ya ujumla kwa
Zanzibar, eneo la Binguni Unguja,’’alieleza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamisb
Hafidh, alisema wananchi 129,141 walitibiwa katika hospitali ya Abdalla Mzee,
ambayo kwa sasa, inatumika kama hospitali ya rufaa kisiwani Pemba.
Alieleza kuwa, ndio maana kwa mwaka jana pekee, kulikuwa
na wagonjwa 50,479 wa nje walitibiwa na waliolazwa kwa mwaka huo ni 633,464.
‘’Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, inapokea wagonjwa
kutoka Pemba na Unguja, kwani sasa ndio hospitali ya rufaa kwa kisiwani Pemba,
kutokana na matibabu yake,’’alifafanua.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa nyumba za madaktari, Meneja
mradi wa ujenzi huo Zhang Ligen, alisema kuwa, kuna majengo manne ya ghorofa nyenye
nyumba zaidi ya 65 kwa ajili ya madaktari.
Alieleza kuwa, mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi
Julai mwaka huu, na kuishukuru serikali na watendaji wa wizara ya Afya, kwa ushirikiano
wao, wakati huu wakiendelea na ujenzi.
Mkurugenzi mkuu wizara ya Afya Zanzibar Dk. Amour Suleiman
Mohamed, alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilisaini makubaliano na
serikali ya Jamhuri ya watu wa China, August 13, 2021 kwa ajili ya ujenzi wa
nyumba hizo.
Alisema nyumba hizo zinajengwa kwa msaada wa serikali ya watu
wa China, chini ya mkandarasi kutoka kampuni ya Zhengtai group na shilingi
bilioni 16.481 zitatumika hadi kukamilika kwake.
‘’Mradi huu utakapokamilika, utandoa kilio cha muda mrefu
cha madaktari, cha kutokuwa na makaazi karibu na sehemu zao kazi, jambo
lililokuwa likizorotesha utendaji,’’alifafanua.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud, awali
alimuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyeiki wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi, kuangalia uwezekano wa kujenga hospitali ya rufaa kisiwani Pemba.
Aidha aliwataka wananchi, kuendelea kuyalinda na kuyaenzi
mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kwani ndio funguo ya maendeleo na uwepo wa
miradi mikubwa.
Mwisho
Comments
Post a Comment