NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali ya awamu ya nane, itaendeleza kwa
vitendo, malengo ya mapinduzi ya Zanzibar, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya
kisasa, kama vile barabara.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo Disemba 4, mwaka 2024, uwanja wa mpira wa
Birikau shehia ya Michungwani, wilaya ya Chake chake Pemba, mara baada ya kuizindua
barabara ya Kijangwani- Birikau, yenye urefu wa kilomita 4.2, ikiwa ni shamra
shamra za miaka 60 ya mapinduzi Zanzibar.
Alisema, kwa vile ujenzi wa miundombinu ya barabara za
kisasa, ni miongoni mwa matunda ya mapinduzi, hivyo serikali anayoingoza imedhamiria
kufanya jitihada za makusdi, za kuimarisha miundombinu hayo, katika maeneo ya
mijini na vijijini kwa Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa, malengo hasa ya serikali ni kuziimarisha barabara zote zilizopo na kujenga nyingine mpya, katika maeneo ambayo barabra hazijafika, ili kuimarisha mtandao wa barabara hapa Zanzibar.
Dk. Mwinyi alisema Zanzibar yote inamtandao wa barabara usiozidi
kilomita 1,344, na wakati anagia madarakani, kulikuwa na wastani wa asilimi 40 ya
barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami, na asilimia 60, zilizobakia
zilikuwa na kifusi na udongo.
‘’Lakini serikali hii ya awamu ya nane, iliamua kuweka
mkakati imara na madhubuti, wa kuimarisha mtandao wa barabara, kwa kuzijenga
barabara za mjini na vijijini, ili zipitike na wananchi waendeleza miradi yao
ya kiuchumi,’’alifafanua.
Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Hussein Ali Mwinyi, alifahamisha kuwa, Zanzibara inapoadhimisha miaka 60 ya
mapinduzi, na miaka mitatu ya serikali ya awamu ya nane, kwa mipango hayo imefanikiwa.
Alieleza kuwa, mipango na mikakati iliyowekwa sasa,
inatekelezwa kwa vitendo nchi nzima, na tayari wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi, imeshaingia mikataba na makapuni mbali mbali, kwa ajili ya ujenzi wa bara
bara hizo.
‘’Kwa mfano, kampuni kutoka Uturuki, imedhamiria
kuzijenga barabara za ndani, kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 275
kwa Unguja na Pemba, ambazo baadhi yao ujenzi umeshaanza,’’alifafanua.
Aidha alifafanua kuwa, tayari serikali imeshaingia
mkataba na kampuni moja, kwa ajili ya ujenzi wa barabara kuu zenye urefu wa
kilomita 130, ikiwemo ya Chake chake- Mkoani, Tunguu- Makunduchi, pamoja na
Fumba- Kisauni, ambapo mkataba umeshainiwa kati ya serikali na Mkandarasi.
‘’Kwa sasa serikali, inaendelea na utaratibu wa
kukamilisha ulipaji wa fidia kwa majengo na vipando, ili ujenzi huo uanze
wakati wowote kuanzia sasa,’’alieleza.
Alifahamisha kuwa, mbali na hatua hizo, tayari serikali
imeshatiliana mkataba na kampuni ya ‘CCECC’ kwa ajili ya ujenzi wa barabara zote
za mjini Unguja, zenye urefu wa kilomita 100.
Aidha alisema, mazungumzo yanaendelea, baina ya serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya watu wa China, kwa ajili ya ujenzi wa bara
bara, zenye urefu wa kilomita 277, zilizoko Unguja na Pemba.
‘’Kama serikali ya awamu ya nane, itafanikiwa kukamilisha
ujenzi wa barabara hizo, itakuwa tumejenga kilomita 800, wakati mtandao wa barabara
hapa Zanzibar, ni kilomita 1,300,’’alifafanua Dk. Mwinyi.
Katika hatua
nyingine, Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi, aliipongeza taasisi ya Zanzibar Milele Foundation, kwa mchango
wa shilingi milioni 982, walazozitoa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya
Kijangwani- Birikau.
Alisema, jumuia za aina hiyo, ndizo zinazofaa kuungwa
mkono na kuigwa na nyingine, ili kuhakikisha wanashirikiana kwa vitendo, na
serikali, katika mipango na mikakati ya kuijenga nchi.
Alieleza kuwa, taasisi hizo ilianza ujenzi wa barabara
hiyo kwa uwekaji wa kifusi tabaka tatu, ujenzi wa daraja ndogo ‘culvert’ pamoja
na misingi ya kupitisha maji ya mvua.
‘’Kama kuna shirika lisilo la kiserikali hapa Zanzibar,
ambalo linafanyakazi kubwa na ya kupigiwa mfano, katika kuisadia jamii na
serikali, ni Milele Ifraji Foundation,''alifafanua.
Wakati huo huo Rais huyo wa Zanzibar, amewaonya madereva
nchini, kuacha kuendesha mwendo wa kasi, kwani unaweza kuzaa majanga yanayoweza
kuepukika.
Alisema, barabara ni kichecheo kikubwa cha maendeleo, na kisigeuzwe
chanzo cha ajali kwa mwendo kasi, ambapo aliwaomba askari wa usalama barabarani,
kusliimamia jambo hilo.
Kwa upande wake Katibu wa wizara ya Ujenzi, Mawasiliano
na Uchukuzi Zanzibar Khadija Khamis Rajab, alisema barabara hiyo yenye urefu wa
kilomita 4.2, imejengwa na serikali kwa kushirikiana na taasisi za Milele na
Ifraji Foundation.
Alieleza kuwa, barabara hiyo, imejumuisha barabara zilizokwenda
kwenye vijiji vya Tondooni urefu wa mita 560, kijiji cha Kiwandani urefu kilomita
wa 440, Makaange mita 100 na barabara iliyongia skuli ya Birikau, yenye urefu
wa mita 200.
Katibu mkuu huyo alifafanua kuwa, ujenzi wa barabara hiyo,
ulianza Febuaru 3, mwaka 2021, baada ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata
ufadhili, kutoka kwa taasisi za Milele na Ifraji Zanzibar Foundetion, kupitia
ofisi ya Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba.
‘’Uwekaji wa lami wa barabara hii, kazi hiyo
ilikamilishwa Wakala wa barabara Zanzibar, kwa kutumia fedha za serikali,
kupitia Mfuko wa Barabara Zanzibar, na ina upana wa mita 5.5,’’alifafanua.
Barabara hiyo ambayo imegharimu shilingi bilioni 1.411,
ambapo kati ya fedha hizo, shilingi mlioni 982 zimetolewa na taasisi hizo, na
shilingi milioni 429.6 zimetolewa na serikali, ambapo itakuwa na uwezo wa
kupitwa na gari zenye uzito usiozidi tani 10.
Mapema Waziri wa wizara hiyo, Dk. Khalid Salum Mohamed,
alisema ndani ya kipindi kifupi cha serikali ya awamu ya nane, wamedhamiria
kujenga kilomita 854 za barabara kwa kiwango cha lami, Unguja na Pemba.
‘’Kwa kisiwa cha Pemba pekee, tunazo wastani wa kilomita 371,
ambazo zinaendelea na ujenzi wake, kupitia kampuni mbali mbali, ambapo kwa muda
mfupi ujao, Pemba itang’ara,’’alieleza.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud,
alisema kazi ya ujenzi wa barabara hiyo imekamalika, sasa ni jukumu la wananchi
kuitunza.
Mwisho.
Comments
Post a Comment