NA MCHANGA HAROUB, WMJJWW-PEMBA
IMEELEZWA kuwa, uanzishwaji
wa jukwaa la wanawake wajasiriamali, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua
changamoto zinazowakabili akina mama hao, katika shehia mbali mbali Zanzibar.
Hayo yameelezwa na
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Siti Abass Ali,
wakati akizungumza kwa nyakati tofauti, na wajasiriamali wanawake wa wilaya nne
za Pemba.
Alisema pamoja na
juhudi kubwa inayochukuliwa na Serikali katika kumuendeleza mwanamke, lakini
bado imeonekana kuna baadhi ya maeneo yamekuwa ni kikwazo kufikia maendeleo
yaliokusudiwa.
Alieleza kuwa,
pamoja na hayo, anaamini uanzishwaji wamajukwaa hayo, inaweza kuwa endelevu,
ili kuwainua kiuchumi wanawake na hatimae taifa kwa juma.
Mkurugenzi huyo
alifahamisha kuwa, uwepo wa majukwaa hayo kutatoa fursa kwa akina mama, kupata
chombo madhubuti cha kuzungumza pamoja na kuwa na sauti moja wanapotafuta dawa
ya changamoto zao.
Mkurugenzi Siti aliwasisitiza
akina mama, kuitumia fursa ya kukaa pamoja na kuhamasishana kujiunga na vikundi
vya ushirika, ili kila mwanamke afikiwe na fursa hiyo.
Aidha Mkurugenzi
huyo amewataka akina mama hao wajasiriamali kujiweka tayari kuchagua viongozi
walio imara ambao wataweza kusimamia vyema majukwaa hayo kwa maslahi yao na taifa
kwa ujumla.
“Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeaamua kuanzisha majukwaa hayo,
kwa lengo la kuinua vikundi vya wanawake wajasiriamali, kwa kutoa fursa ya
kukaa pamoja na kuzungumza mahitaji yao,’’alifafanua.
Akizungumzai uendelevu
wa zoezi la kuanzisha majukwaa hayo ya wanawake, alisema linaendelea katika
wilaya zote za Zanzibar, na litahusisha vikundi vyote vya wanawake ambavyo
vimesajiliwa na visivyo sajiliwa.
Katika hatua
nyengine Mkurugenzi huyo amewataka waratibu wa wanawake wa shehia, kuhakisha
kila mwanamke anakuwa mnufaika wa uwepo wa majukwaa hayo, kwani Serikali
imedhamiria kuwafikia wanawake wote bila kujali sehemu anayotoka.
Kwa upande wao
wanawake hao wajasiriamali wameishukuru Serikali kupitia Wizara hiyo, kuona
umuhimu wakuweka majukwaa hayo, ili wapeleke malalamiko.
Walisema, kwani
mara nyingi wamekuwa wakifikwa na misuko suko ya utendaji kazi, ikiwemo
kukosekana kwa ardhi ya kudumu ya kilimo kwa wajasiriamali wanaolima mboga
mboga, jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi zao.
"Tunashkuru
kuona sasa tutakuwa na eneo la kutoa malalamiko yetu, maana binafsi
nishawahamasisha wanawake, tukaanza kilimo cha mboga mboga lakini ardhi haikuwa
ya kwetu, hivyo baada ya mavuno, tulitakiwa kuikabidhi kwa muhusika,’’walisema.
Mwisho
Comments
Post a Comment